Mtama, Lindi
Wananchi wa vijiji kumi vya kata ya Mandwanga na Mnara, Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi, watanarajia kuondokana na changamoto ya huduma ya maji safi na salama katika maeneo yao baada ya Kanisa la Anglikana Doyasisi ya Masasi kuanza ujenzi wa miradi mitano ya maji itakayogharimu zaidi ya Sh. bilioni 1.4.
Katibu Mtendaji wa Doyasisi hiyo Joyce Liundi amesema, Kanisa linatekeleza miradi hiyo kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita ya kutatua changamoto ya maji na kutekeleza kwa vitendo dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
Liundi amevitaja vijiji vitakavyonufaika na miradi hiyo kuwa ni Malungo, Mnazimmoja, Nyundo 1, Nambahu, Chiuta, Mikongi Mandwanga, Lindwandwa vilivyopo kata ya Mandwanga na Mkanga 11 na Chikombe Kata Mnara.
Ameishukuru serikali kwa kuwaunga mkono katika utekelezaji wa miradi hiyo na wananchi wa vijiji hivyo kwa kukubali kutoa maeneo yao bure hali iliyowezesha kutekeleza miradi bila ya vikwazo vya ulipaji fidia.
Ametoa mwito kwa wananchi wa vijiji vilivyopata miradi hiyo kuhakikisha wanatunza maeneo yaliyopitiwa na miradi, kulinda miundombinu na vifaa vinavyoletwa kwa ajili ya ujenzi ili waweze kunufaika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mtama George Mbilinyi, amelishukuru Kanisa la Anglikana Doyasisi ya Masasi kuunga mkono jitihada za serikali kwa kujenga miradi ya maji katika vijiji ambavyo kwa muda mrefu havina huduma ya maji ya bomba.
Alisema, miradi hiyo inayotekelezwa chini ya ufadhili itatimiza azma ya serikali ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi wa Halmashauri hiyo umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao na kumtua mama ndoo kichwani.
Mbilinyi,ameagiza kuongezwa nguvu kazi katika ujenzi wa miradi hiyo ili ikamilike haraka na wananchi waanza kupata huduma ya maji safi na salama kwenye makazi yao.
Amewataka wananchi wa vijiji hivyo, kuhakikisha wanatunza miradi hiyo inayojengwa mahususi ili kuwapunguzia muda wa kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji muda ambao wangeweza kuutumia katika shughuli nyingine za maendeleo.
Aidha, amewapongeza wananchi waliokubali kutoa maeneo yao kupisha ujenzi wa miradi ya maji ambapo amewaomba kuendelea kushirikiana na serikali na wadau wa maendelea katika kutatua baadhi ya changamoto zilizopo katika maeneo yao.
Awali Mhandisi wa maji wa Doyasisi hiyo Olaph John alisema, katika awamu ya kwanza miradi inayotekelezwa ni mitano ambayo ni mradi wa maji Nambahu- Nyundo 1, Chiuta-Mikongi na Mandwanga-Lindwandwali.
Alisema, miradi hiyo ilitarajia kukamilika mwezi huu, lakini walishindwa kukamilisha kwa muda uliopangwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo mvua kubwa zinazoendelea kunyesha, hata hivyo itakamilika mwishoni mwa mwezi ujao.
Olaph alitaja miradi mingine miwili ya Mnazi Mmoja-Malungo na Mkanga 11-Chikombe ambayo tayari imefanyiwa upembuzi itaanza kutekelezwa haraka iwezekavyo ili wananchi wa vijiji hivyo wapate huduma ya maji safi na salama.
Kaimu Afisa Mtendaji Kata ya Mandwanga Aletu Kambona alisema, adha ya maj safi na salama katika kata hiyo ni kubwa na kwa sasa wananchi wanalazimika kutumia maji ya mito na vyanzo vingine vya asili ambavyo maji yake siyo safi na salama.
Afisa usafi wa mazingira wa Kanisa la Anglikana Doyasisi ya Masasi George Mgaza, akitoa taarifa zinazochukuliwa kabla na wakati wa ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa na Kanisa hilo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi George Mbilinyi (kulia), wakati wa ziara ya wakuu wa idara wa Halmashauri ya Mtama kutembelea utekelezaji wa miradi ya maji.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇