| Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Silvanus Kwembe, akizungumza wakati wa tamasha maalumu kwa watu wanaoishi na ulemavu, tamasha la Usiku wa Mwangaza. |
NA VICTOR MAKINDA:MVOMERO, MOROGORO
Wito umetolewa kwa jamii kote nchini kutokwepa wajibu wa
kuwahudumia watu wanaoishi na ulemavu sambamba na kuhakikisha kuwa kundi linapata mahitaji mbali mbali ya msingi ikiwa
ni pamoja na elimu na ujuzi utakao wawezesha kujimudu wenyewe.
Wito huo umetolewa na
Makamu wa Askofu, Jimbo
katoliki la Morogoro, Padre Silvanus
Kwembe, wakati alipokuwa akizungumza kwenye tamasha maalumu la kutoa hamasa kwa
jamii kujali mahitaji ya watu wenye ulemavu linalojukana kama tamasha la la
Usiku wa Mwangaza lililofanyika kijijini Mvomero wilayani Mvomero mkoani
Morogoro jana.
Padre Kwembe alisema kuwa jamii kwa ujumla haipaswi kukwepa
jukumu la kuwahudumiwa watu wenye ulemavu na kuuacha mzigo huo kwa wazazi pekee
bali inatakiwa kila mmoja ajione kuwa anao wajibu wa msingi wa kuwahudumia watu
wenye ulemavu sambamba na kuwapenda na kuwajali.
“ Kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kutoa mchango wake
kuwahudumia watu wenye mahitaji maalum kwa kuwa ustawi wa kundi hilo unategemea
upendo wetu na namna tunavyojitoa kwao kuwasaidia kupata mahitaji muhimu ka
ajili ya ustawi wao”. Alisema.
Aliongeza kusema kuwa
watu wanaoishi na ulemavu wanakumbana na
changamoto nyingi, ikiwemo kukosa elimu, huduma duni za afya, chakula na
maradhi huku baadhi yao wakiwa wanyanyapaliwa hata na ndugu wa karibu.
Mwasisi wa Taasisi ya EMFERD , Josephine Bakhita, akizungumza kwenye tamasha la Usiku wa Mwangaza
“Hakuna ibada njema zaidi ya
kuwajali wahitaji. Watu wenye ulemavu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waumini wa dini zote
na madhehebu yote, kwa pamoja tunapaswa kuishi kwa kujaliana na kusaidia,
kipekee kuwasaidia wenzetu ambao maumbile yao yana mapungufu kwa kugawana nao
kile tulichojaaliwa kukipata ili nao wafurahie maisha.” Alisema Padre Kwembe.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye tamasha hilo la Usiku
wa Mwangaza, wazazi wenye watoto wanaoishi na ulemavu walisema kuwa
wanakabiliwa na changamoto nyingi kwenye malezi ya watoto hao hususani watoto
wenye ulemavu wa viungo na akili,
ikiwemo ukosefu wa huduma za afya
sambamba na huduma maalumu za mazoezi
kwa ajili ya urekebishaji wa viungo.
“ Sisi tunaoishi vijijini tunaiomba serikali ituletee huduma
za mazoezi kwa watoto wetu wenye ulemavu kwani hospitali ambazo zinatoa huduma
hizo zipo mbali sana.” Anaeleza Jakline
Paulo mmoja ya wazazi mwenye mtoto anayeishi na ulemavu.
Anaongeza kusema
kuwa sambamba na changamoto ya kukosa
huduma za mazoezi kwa ajili ya mtoto wake pia anakabiliwa na umaskini mkubwa wa
kipato kwa kuwa muda mwingi anautumia kumlea mtoto huyo na kukosa muda wa
kwenda shamba kulima na kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali.
Baadhi ya watoto wenye ulemavu wakiwa katika tamasha hilo.
Akizungumza wakati wa tamasha hilo, muasisi wa taasisi ya
EMFERD, taasis inayoshughulika na kulea watoto wenye ulemavu wa akili na
viungo, Josephine Bakhita, ambayo ndiyo iliyoandaa tamasha hilo la Usiku wa
Mwangaza kwa kushirikiana na Parokia katoliki ya Mtakatifu Aloyce Gonzaga
Mvomero, alisema kuwa pamoja na mambo mengine taasisi yake inasadia watoto
wanaoishi na ulemavu kwa kuwapa huduma
ya elimu na mazoezi kwenye vituo vyake na nyumbani.
Taasisi ya EMFERD kwa
kuzingatia umuhimu wa huduma ya mazoezi
kwa watoto waliozaliwa na ulemavu pamoja na huduma nyingine, tunatoa huduma za
mazoezi ambapo mtaalamu wetu huwatembelea majumbani kwenye vijijiji vilivyo
pembezoni na kuwapatia huduma hiyo
muhimu ya urekebishaji.”
Bakhita anaongeza
kusema kuwa uhaba wa wataalam wa huduma hiyo sambamba na ufinyu wa rasilimali
fedha unaikwamisha taasisi yake
kulifikia kundi kubwa la wahitaji.
“ Wahitaji ni wengi,
watoa huduma ni wachache hivyo, tunaomba
serikali, watu binafsi na taasisi
mbali mbali kushirikiana na taasisi ya
EMFERD kuhakikisha kuwa huduma ya
mazoezi kwa watoto wanaoishi na ulemavu
wa viungo na akili inatolewa ili kuwawezesha watoto hao kujimudu wenyewe na
kupunguza mzigo mkubwa wa malezi kwa wazazi wao” Anasema Josehine Bakhita.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇