CCM Lumumba, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kudumisha uhusiano na urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na Urusi katika kuboresha maeneo ya uwekezaji, biashara na uchumi, kwa manufaa ya nchi hizo.
Balozi Dk. Nchimbi amesema hayo alipofanya mazungumzo na Balozi wa Urusi hapa nchini Balozi Andrey Avetisyan, aliyemtembelea Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba Jijini Dar es Salaam, leo Februari 22, 2024.
Katika mazungumzo hayo pamoja na kurejea kumbukumbu za uhusiano wa muda mrefu wa Tanzania na Urusi, tangu wakati wa kupigania uhuru na baada ya uhuru, ambao mwaka huu unafikisha miaka 62, walizungumzia maeneo ambayo yanaweza kufanyiwa kazi na Serikali, chini ya uongozi wa vyama vinavyoongoza nchi hizo, Chama Cha Mapinduzi na United Russia, mtawalia.
Kwa upande wake, Balozi Avetisyan, mbali ya kumpongeza na kumtakia kila la heri Balozi Dk. Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu, ameelezea uhusiano wa muda mrefu wa Urusi kwa Tanzania na nchi za Afrika, tangu wakati wa kupigania uhuru na baada ya uhuru, ambapo ilikuwa mojawapo ya nchi za mwanzo kuitambua Tanganyika huru.
Alisisitiza kuwa chini ya uongozi wa Rais Vladimir Vladimirovich Putin, na mazingira mazuri ya uwekezaji, biashara na uchumi ya Tanzania chini ya Rais Dk. Samia, Urusi iko tayari kuendelea kuenzi na kuimarisha uhusiano utakaonufaisha pande zote mbili.
Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza na Balozi wa Urusi hapa nchini Balozi Andrey Avetisyan, aliyemtembelea Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba Jijini Dar es Salaam, leo Februari 22, 2024.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇