LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 26, 2024

MBUNGE KAMONGA AWAPONGEZA WALIMU, WANAFUNZI KUTOKOMEZA UFAULU WA SIFURI LUDEWA


 Na Richard Mwaikenda, Dodoma


Mbunge wa Jimbo la Ludewa Mhe.Joseph Kamonga, ametoa salamu za pongezi kwa walimu na wanafunzi kwa matokeo mazuri na mafanikio yaliyopatikana  kwa shule za Jimbo hilo, katika *Mkakati wa Kutokomeza Sifuri* katika shule za sekondari.


Mhe.Mbunge Kamonga,ametoa pongezi hizo kufuatia matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) Januari 25,2024,ambapo ufaulu wa wanafunzi ndani ya Jimbo la Ludewa umeongezeka na baadhi ya shule kutokuwa na ufaulu wa daraja sifuri. 


Pongezi hizo zimetolewa na mbunge huyo katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma Januari 26, 2024,alipohojiwa na mwandishi wa habari hii, aliyetaka kujua hali ya matokeo ya kidato cha nne katika Wilaya ya Ludewa.


Kampeni hiyo ya Mkakati wa Kutokomeza ufaulu wa sifuri kwa shule za serikali Ludewa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo kwa matokeo ya sasa ya kidato cha nne ya mwaka 2023 waliopata sifuri ni wanafunzi 25 tu, wakati mwaka 2022 walikuwa 94. 


Hivyo, mhe. Mbunge amewapongeza sana walimu, wazazi, wanafunzi pamoja na wadau wengine wote wa elimu kwa ushirikiano mkubwa katika sekta ya elimu na hatimaye sasa Ludewa inapata matokeo yenye tija kwa Vijana. 


"Nawapongeza sana walimu, wanafunzi, wazazi na wadau wote wa elimu kwa ushirikiano mkubwa na hatimaye sasa shule zetu zimeanza kutokomeza ufaulu wa daraja Sifuri. Hakika nawashuru Sana na hongereni Sana."


 Hata hivyo, mbunge huyo aliyeanza kuongoza jimbo hilo mwaka 2020, amewaomba wana_Ludewa hasa wazazi kuendelea kushikamana na walimu kuwaendeleza vijana kielimu maana elimu  ndio urithi pekee wa Mtoto. 


Pamoja na Pongezi hizo, Mhe.Mbunge Kamonga hakusita kutoa shukrani nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania_ Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia pamoja na kuongeza walimu  mwaka hadi mwaka na kutoa fedha nyingi kwenye Sekta ya Elimu.


Tangu Mhe.Kamonga aanze kuliongoza jimbo hilo mwaka 2020 hadi sasa Serikali inayoongozwa na Rais Samia imepeleka jimboni humo fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa 140, mabweni 17, maabara 19, matundu ya vyoo 115, walimu 65 kwenye shule za sekondari za serikali 20 zikiwemo mpya 3 zilizojengwa kipindi hiki, maktaba 2 na vyumba vya tehama 2.


 Aidha,Kamonga ameitaka jamii kutambua mchango wa serikali na kuendelea kuwapa ushirikiano walimu kwa kuwapatia malezi mazuri wanafunzi ili kujenga kizazi kijacho chenye maadili ya kitanzania.


Vilevile ametoa wito kwa uongozi wa Wilaya ya Ludewa kuongeza kasi ya ujenzi wa mabweni na madarasa kidato cha tano na sita ili shule nyingi zaidi zianzishe vidato hivyo na kuongeza chachu ya maendeleo ya elimu wilayani humo. 


Hivi karibuni mbunge huyo ametoa mifuko 150 ya saruji, mabati yanayotosha kuezeka madarasa mawili na ofisi moja ya walimu kwenye kata za Iwela na Kilondo ambazo hazikuwa na shule za sekondari za kata ili ziweze kujengwa.


Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ludewa, ametenga fedha za ujenzi wa madarasa mawili na ofisi kwenye shule ya Ruhuhu ili ipunguze msongamano wa wanafunzi Sekondari ya Manda ambayo pia watoto wanaotoka vijiji vya Ngelengele, Kipingu na Ilela watapunguziwa umbali mrefu waliokuwa wakitembea kufuata elimu ya sekondari katika Kijiji cha Nsungu.


 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages