LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 26, 2024

BI SALOME KOMBA NA FAMILIA YAKE KUJENGA JENGO LA KISASA LA MAKUMBUSHO YA KAMPTENI KOMBA, KULIZINDUA FEBRUARI 28, 2024, LITASHEHENI NYIMBO ALIZOIMBA NA HISTORIA YAKE

Na Bashir Nkoromo, Mbezi Beach
Jumamosi mchana, Februari 28, 2015, aliyekuwa nguli wa kutunga na kuimba nyimbo za kwaya Kapteni John Komba alihitimisha safari yake duniani baada ya kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 61.

Ikiwa sasa ni miaka tisa tangu Kapeni Komba atangulie mbele za haki, hapana shaka ataendelea kukumbukwa kwa mengi, hasa mchango alioutoa katika kutunga na kuimba nyimbo mwanana tangu akiwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na baadaye Tanzania One Thetre (TOT) akiwa Mkurugenzi wa kundi hilo la hamasa la Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ni Kapteni Komba ambaye Wabunge wengi walikuwa wakishinda kwenye chaguzi kwa msaada mkubwa wa sauti yake, marais wengi wa hapa nchini hadi wa baadhi ya nchi za jirani ikiwemo Malawi wakati wa Uchaguzi uliomuweka Bakili Muluzi madarakani nao pia walinufaika na mchango wa sauti ya Komba na hivyo kushinda nyadhifa hizo katika Chaguzi.

Komba aliyezaliwa mwaka 1954, Lituhi, Mbinga mkoani Ruvuma na kupata elimu katika shule ya msingi Lituhi, Mbinga, Ruvuma kati ya mwaka 1962 na mwaka 1968 kabla ya kujiunga na sekondari ya Songea Boys kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1974, hakika alikuwa ni msanii wa kipekee ambaye ni katika wale ambao husemwa pengo lake halitazibika.

Moja ya nyimbo zilizoacha alama ya Kapeni Komba, ni ule wimbo wa maombolezo ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere mwaka 1999, wimbo huo kila uliposikika ulilifanya taifa lizidi kuzizima kwa sauti yake nzito iliyofanya mambo mawili ambayo ni nadra sana kwenda sanjari, yaani ya kuhuzunisha na kufariji.

Wimbo huo ulikuwa ni kazi aliyoifanya kwa haraka sana mara tu baada ya kifo cha Nyerere kutangazwa. unaweza ukadhani labda kwa vile Mwalimu aliugua kwa muda mrefu hivyo kumpa muda wa kujiandaa kuutunga, ukifikiri hivyo utakuwa unakosea sana, maana Komba huyo Mwaka 1986 mwezi Oktoba, alitunga wimbo wa kifo cha aliyekuwa Rais wa Msumbiji Samora Machel muda mfupi tu baada ya rais huyo kufariki kwa ajali ya ndege nchini Afrika Kusini.

Hakika Komba aliyekuwa pia Mbunge wa Mbinga Magharibi alijaaliwa sauti yenye hamasa ambayo inapoanza tu kusikika ni lazima utaisikiliza na kuruhusu ujumbe kupenya kwenye masikio yako bila kujali kuwa unampenda au humpendi, anakuudhi au kukufurahisha.

Kapten Komba alianza kujiingiza katika masuala ya muziki tangu akiwa shule ya msingi nyumbani kwao Litui, Mbinga mkoani Ruvuma, kandokando ya ziwa Nyasa kwa kufundishwa kuimba na mapadri wa kizungu.

Alipoingia sekondari akapewa jukumu la kuwa kiranja wa starehe na utamaduni kutokana na kuonyesha kipaji na uwezo mkubwa kwenye fani mbalimbali za burudani, kama vile kwaya, jiving na ngoma za kienyeji.

Alipohitimu masomo yake ya sekondari, mwaka 1975, alijiunga na Chuo cha Ualimu Kleruu, Iringa alikotwaa cheti cha Daraja ‘A’ cha taaluma hiyo, kabla ya mwaka 1976 kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kwenda Mafinga, Iringa kwa mujibu wa sheria.

Akiwa Mafinga Komba akakutana na Brigedia Jenerali Mosses Nnauye ambaye alikihusudu kipaji chake na kuamua kukiendeleza kwa kumwimbisha zaidi kwenye magwaride na nyimbo nyingine mbalimbali za kijeshi, akawa akitunga nyimbo na kuimba, huku Nnauye akipiga kinanda.

Brigedia Mosses Nnauye
Mwaka 1977 alikwenda kufundisha shule ya msingi Gangilonga, mkoani Iringa lakini mwaka uliofuata, 1978 Nnauye akamfuata na kumpeleka Mondoli, katika Chuo Cha Jeshi na kuhitimu mafunzo na kutunukiwa nyota moja na alipotoka hapo akapokewa moja kwa moja na vita ya Kagera.

Mwaka 1980 alichaguliwa kuwa kiongozi wa kikundi cha jeshi cha sanaa za maonyesho, ambako alisafiri nacho katika nchi za Zimbabwe, Msumbiji, Kenya, Zambia, Libya, Seychelles na Urusi na akaanza kujipenyeza kwenye siasa mwaka 1987 pale alipoamua kugombea nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo alishinda na kudumu nayo hadi mwisho wa uhai wake.

Mwaka 1988 CCM ilimpeleka barani Ulaya kusomea elimu ya siasa kwa miaka miwili, na kuibuka na stashahada. Mwaka 1992 akaamua kufanya maamuzi magamu, akaacha kazi ya jeshi na kuamua kuitumikia CCM na moja kwa moja akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa kundi jipya la Tanzania One Theatre (TOT) lililoanzishwa mahsusi na CCM kwa ajili ya kuhamasisha wana CCM lakini pia kukabiliana na changamoto za ujio wa siasa za vyama vingi.

Kazi ya kwanza kabisa ya Komba katika TOT ikazaa wimbo 'CCM Nambari Wani' ambao hadi leo hii bado ni nguzo kubwa ya Chama Cha Mapinduzi katika mikutano ya kampeni za kisiasa na hadi ndani ya vikao muhimu vya chama.

Mwaka 2005 Komba aliyeacha mjane Bi Salome Komba na watato 10, akagombea ubunge jimbo la Mbinga Magharibi kwa tiketi ya CCM na kushinda, nafasi ambayo pia ameitumikia hadi kifo chake.

Komba hakuwa mtu wa makuu, alicheka na kutaniana na kila mtu, binafsi nilibahatika kuwa karibu naye, na kwa kwelie kuna wakati nilimkera, lakini bado hakunikimbia, alichokuwa akikifanya ni ‘kunichana’ bila kupepesa macho baada ya hapo kisirani kinamwisha na maisha yanaendelea.

Sasa kama ambavyo husemwa kwamba 'kilio huanza na mwenyewe', katika kuienzi historia ya Kampeni John Jomba, Mjane wake Bi Salome Komba kwa kushrikiana na familia yake wamendaa  kujenga jengo la kisasa la Makumbusho kumuenzi ambalo litaitwa Kapteni John Komba Museum.

Bi Salome Komba amesema, jengo hilo la Kisasa litajengwa nyumbani kwa Hayati Komba, Mbezi Beach kwa Komba, eneo la Tangibovu na humo zitawekwa nyimbo zake zote alizoimba Kapteni Komba enzi za uhai wake, sanjari na historia ya maisha yake ambayo vitahifadhiwa katika CD na Flash.

Bi Salome Komba amesema, maandalizi yameipamba moto, kwa ajili ya uzinduzi wa jengo hilo la Makumbusho ambayo utafanyika mwezi ujao wa Februari 28, mwaka huu, ikiwa ni kuadhimisha siku ambayo Komba alifariki dunia Februari 28, 2015.

"Kufuatia umuhimu wa tukio hili tunakaribisha kila Mtanzania mwenye upendo wa hayati Kapteni Komba kuchangia sh. 2,000 tu, kupitia mitamdao ya simu ambayo namba zake tutazitangaza baadaye.

Pia katika makusanyo yetu kiasi kitakachobaki baada ya ujenzi wa makumbusho, tutawapatia wanamuziki waliokuwa na Kapeni Komba tangu JKT, JWTZ na TOT na ambao wameshatangulia mbele za haki tutawasaidia wajane wao", amesema Bi Salome Komba.

Kampten John Komba akiimba enzi za uhai wake.
 
Rais Mstaafu (sasa), Dk. Jakaya Kikwete alipokuwa akimfariki Bi Salome Komba Mjane wa Kampteni John Komba siku ya kuaga mwili wa marehemu katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages