NA JOE NAKAJUMO
MAPINDUZI Matukufu ya Zanzibar, Ijumaa ya tarehe 12 Januari, juma hili, mwaka huu wa 2024, yalitimiza miaka 60.
Ni ushahidi wa wazi kwamba idadi kubwa ya Wazazibari hawakuwa wamezaliwa wakati Mapinduzi yanatokea usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili ile ya Januari 12, mwaka 1964.
Hata hivyo, ni jambo la kujivunia, kwa sababu, kizazi cha leo, kinazidi kuyaenzi Mapinduzi kwa kuyalinda, kuyadumisha na kuyaendeleza kwa kuimarisha huduma za jamii na uchumi.
SABABU ZA MAPINDUZI
Mapinduzi ya mwaka 1964, yalidhamiria kuondoa chuki, ubaguzi, utesaji na kuweka misingi imara ambayo utaendeleza mipango ya maendeleo ya nchi na ndio maana kuna kauli mbiu ya ‘Mapinduzi Daima. ’Januari 12, mwaka 1964 ndiyo siku sahihi ambayo Zanzibar ilipata uhuru wake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali iliamua kuyafanya maadhimisho ya mwaka huu kwa kauli mbiu isemayo,”Miaka 60 ya Mapinduzi Zanzibar: Tuimarishe uchumi, uzalendo, amani na maendeleo ya Taifa letu.”
Shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi zilianza tangu mwishoni mwa mwaka jana. Wananchi na viongozi wameshirikiana kufanya kazi za ujenzi wa Taifa katika maeneo mbalimbali ya visiwani, Unguja na Pemba.
Viongozi, wakiongozwa na Rais Dk. Mwinyi, walikuwa na shughuli nyingi kila siku kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi katika vijiji, wilaya na mikoa yote mitano ya Zanzibar.
MIAKA MITATU YA DK.MWINYI
Katika kipindi cha miaka mitatu tangu Rais Dk. Mwinyi alipoanza kuiongoza Zanzibar, mwaka 2020, hatua kubwa ya maendeleo imefikiwa katika sekta za huduma za jamii na uchumi.
Miradi mingi ya sekta ya afya, elimu, maji, miundombinu ya bararabara na uendelezaji wa uchumi wa buluu umekuwa ukipewa kipaumbele kila uchao.
Elimu ni miongoni mwa sekta zenye mafanikio kwani uimarishaji wa miundombinu ya elimu umefanywa kwa kujenga shule mpya 62 za ngazi mbalimbali.
Mara tu baada ya kushika hatamu ya kuiongoza Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi, ilifuta ada kwa shule na vyuo vyote Zanzibar kwa tangazo lililotolewa Septemba 23, mwaka 1964.
Ilifanya hivyo kwa kutambua kuwa elimu ni haki ya msingi ya kila Mzanzibari na kwamba elimu itatolewa bure kwa wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote. Kabla ya Mapinduzi, elimu ilikuwa inatolewa kwa ubaguzi na mtoto wa mnyonge hakuwa na haki ya kupata elimu.
SHULE ZA GHOROFA
Rais Dk. Mwinyi katika shamrashamra za miaka 60 ya Mpinduzi, Januari 3, mwaka huu, aliweka jiwe la msingi la Shule ya Msingi ya ghorofa Maziwang’ombe, wilaya ya Micheweni, mkoa wa Kaskazini Pemba. Shule ina ghorofa tatu na ina madarasa 41 ikiwa imegharimu Sh. bilioni 6.2 na zote zimetolewa na serikali.
Alisema serikali inaendelea na ujenzi wa shule mpya za ghorofa katika maeneo 25, Unguja na Pemba na tayari shule za ghorofa zimejengwa Gamba, Kojani na Tumbatu.Lakini pia pamoja na kujenga majengo ya shule,Rais alisema mwaka huu wanakusu dia kuajiri walimu 1,500.
Kwa upande wa huduma za maji, Serikali ya Mapinduzi ipo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa miradi mikubwa ya maji safi na salama, Unguja na Pemba.
Miradi hiyo inahusu ujenzi wa matangi 25 yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 134 na mradi wa pili ni wa ujenzi wa matangi 10 yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10.
NYUMBA KWA WAFANYAKAZI
Sekta ya afya nayo inatiliwa mkazo, serikali imejenga hospitali 10 za wilaya kwa Unguja na Pemba zikiwa na vifaatiba na magari ya kubebea wagonjwa.
Akiweka jiwe la msingi ujenzi wa nyumba za wafanyakzi katika hospitali ya Abdallah Mzee, mkoani Pemba, Rais Dk. Mwinyi, alisema serikali itajenga nyumba za wafanyakazi wa sekta ya afya katika hospitali zote za wilaya.
Nyumba zingine zitajengwa katika hospitali za Kinyasini wilaya ya Wete, Vitongoji,wilaya ya Chakechake na Micheweni kwa upande wa Pemba
Unguja, nyumba za wafanyakazi wa hospitali zitajengwa Kitogani wilayani ya Kusini, Pongwe wilaya ya Kati, Pangatupu, wilaya ya Kaskazini B na Kivunge wilaya ya Kaskazini A.
UCHUMI WA BULUU
Kwa sekta ya uchumi, serikali inaendelea kutekeleza miradi mbali mbali katika uchumi wa buluu. Miradi hiyo ni pamoja na uvuvi, mashamba ya kufugia samaki nakilimo cha mwani,
Mara tu alipoingia madarakani, Rais Dk. Mwinyi alitangaza Uchumi wa Buluu na akaunda wizara mahsusi ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Aboud Suleiman Jumbe ametaja baadhi ya mafanikio katika eneo la uchumi wa buluu. Amesema uchumi wa buluu umepata mafanikio makubwa ikiwemo sekta ya uvuvi. Pato lake la Taifa limekuwa kufikia asilimia 6.3 kutoka asilimia 4.
Zanzibar ilikuwa inazalisha tani 8,000 zenye thamani ya sh. milioni 205. Sasa zinazalishwa tani 38,000 hadi 61,794 zenye thamani sh. bilioni 491.3.
Biashara ya zao la mwani imeongezeka kutoka tani 8,000 za thamani ya sh.bilioni 5 hadi kufikia tani 12,594 zikiwa na thamani ya sh.bilioni 10.
Katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya Rais Dk. Mwinyi, wajasiriamali wamewezeshwa kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.Serikali imejenga vituo vya wajasiriamali kila wilaya na kuwapatia mikopo nafuu. Wavuvi wadogo na wakulima wa mwani wamepatiwa mikopo na vifaa.
UFANISI WA PBZ NA ZRA
Benki ya Watu wa Zanzibar (Peoples Bank Zanzibar –PBZ) imefanya kazi kwa mafanikio mwaka jana wa 2023, kwa kuingiza faida ya sh.bilioni 78 ikilinganishwa na faida y ash.bilioni 22 iliyopatikana mwaka 2022.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ, Said Mohammed Said, amesema PBZ imepata mafanikio kwa kasi,mwaka 2020 ilikuwa na matawi 29 na yameongezeka hadi kufikia 46, mwaka jana.Matawi 35 Zanzibar na 11, Tanzania Bara.
Upande wa makusanyo ya kodi pia kumekuwa na ufanisi.Kamishna wa Mamlaka ya Mapato
Zanzibar (ZRA), Yusuph Juma Mwenda amesema kipindi cha Julai hadi Novemba 2023, ZRA ilikusanya sh.bilioni 288.2 na kuvuka makadirio ya sh.bilioni 206 yaliyowekwa.
HOTELI ZA NYOTA TANO
Sekta ya utalii ndiyo njia kuu ya uchumi na mapato kwa Zanzibar na serikali inaendelea kukaribisha wawekezaji kwa ujenzi wa hoteli za kitalii za hadhi ya nyota tano na zaidi.
Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla mwezi uliopita katika shamrashamra kuelekea kilele cha miaka 60 ya Mapinduzi,aliweka jiwe la msingi la mradi wa hoteli ya Mada yenye hadhi ya nyota tano iliyopo Michanvi Kae,Mkoa wa Kusini Unguja.
Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Sharif Ali Sharif, amesema mradi wa hoteli ya Mada utagharimu dola milioni 30 na kutoa ajira zaidi ya watu 250.
Rais mstaafu wa Awamu ya Sita, Zanzibar, Amani Karume amefungua hoteli ya YCONA ECO LUXURY RESORT katika mfululizo wa sherehe za miaka 60 ya Mapinduzi. Hoteli hiyo ipo Uroa, wilaya ya Kati,Unguja.
Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, alisema katika kipindi cha miaka mitatu, ZIPA imetekeleza zaidi ya miradi 200 na kuwekeza zaidi ya sh.bilioni 14.3 kwa Mkoa wa Kusini Unguja na ajira 3,000 zimepatikana.
Sharif alisema wanatarajia kujenga hoteli kubwa ya nyota saba katika kisiwa cha Pemba na kukodisha visiwa 16 kwa uwekezaji.
Mapinduzi yameleta mageuzi ya uchumi na maisha ya wananchi wa visiwani,Unguja na Pemba na yamewapa funzo Wazanzibari kujenga uzalendo na kushirika miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha mada ya kujenga misingi ya uzalendo kwenye kongamano kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi,Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Dk. Abdulrahamid Yahya Mzee, alisema miradi mingi ikiwemo ujenzi wa nyumba za makazi Michenzani,zilijengwa na wananchi kwa kujitolea.
Dk. Mzee alisema, Rais wa Awamu ya Kwanza, Sheikh Abeid Amani Karume, aliwaongoza mamia ya wananchi katika ujenzi wa nyumba hizo na zilizopo vijijini eneo la Bambi.
Amewataka vijana waliozaliwa baada ya Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964, kushiriki shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba.
Your Ad Spot
Jan 18, 2024
Home
featured
siasa
MAPINDUZI YA ZANZIBAR HAYAKUBAKI HISTORIA BALI YAMEKUWA CHACHU YA KUIMARISHA NA KUUPAISHA UCHUMI WA VISIWA HIVYO
MAPINDUZI YA ZANZIBAR HAYAKUBAKI HISTORIA BALI YAMEKUWA CHACHU YA KUIMARISHA NA KUUPAISHA UCHUMI WA VISIWA HIVYO
Tags
featured#
siasa#
Share This
About Bashir Nkoromo
siasa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇