LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 29, 2024

KUMBUKIZI YA MIAKA 9 YA KIFO CHA KAPTENI KOMBA KUFANYIKA FEBRUARI 28, WADAU WAOMBWA KUTOA MICHANGO KUFANIKISHA YATAKAYOJIRI SIKU HIYO KUMUEZI, INJINIA JULIANA AAHIDI KUCHANGIA MILIONI 2, ATOA LAKI PAPO HAPO

Na Bashir Nkoromo, Official CCM Blog, Mbezi Beach kwa Komba.
HEKAHEKA za maandalizi ya kumuenzi aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mkurugenzi wa Tanzania One Theatre (TOT) Kapteni John Komba, tangu afariki dunia, wadau wameombwa kutoa mchango ili kufanikisha matukio yatakayojiri siku ya kumbukizi hiyo Februari 28, 2024, ikiwa ni miaka tisa tangu aage dunia.

Akizungumza leo Tangi Bovu, Mbezi Beachi kwa Komba, Jijini Dar es Salaam, Kiongozi wa Familia Mjane wa Marehemu Kapteni Komba,  Salome Komba amesema Kumbukizi hiyo inafanyika Februari 28, 2024, ikiwa ni tarehe na mwezi aliofariki Kapteni John Komba ambaye alifariki dunia siku ya Jumamosi, Februari 28, 2015.

Mama Salome Komba akasema, yapo mambo mbalimbali yatajiri siku hiyo lakini makubwa zaidi ni mawili ambayo Familia imeamua imuunge mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na serikali kwa  kwa kumla kusapoti matibabu ya watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa wa moyo na kujenga Makumbusho ya kisasa ya Kapteni John Komba (Captain Komba Museum).

"Familia imeamua imuunge mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daktari Samia Suluhu Hassan, pamoja na serikali yake kwa jumla, kwa kusapoti matibabu ya watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa wa moyo.

Lakini naomba niweke wazi kwamba hatumuungi mkono kwa sababu ni Rais, hapana, pamoja na kuwa Rais wetu, tunamuunga mkono kwa sababu ya Moyo wake wa Upendo na Utu alionao yeye binafsi", akasema Mama Salome Komba na kuongeza;
 
"Mimi na familia tunakumbuka Kapteni Komba alipokuwa anaumwa sana, Rais Dk. Samia, yeye ndiye alikuwa miongoni mwa Viongozi wa kwanza kabisa kufika kumpa pole. Wakati ule nadhani alikuwa ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais - Masuala ya Muungano".

Mama Salome Komba akasema, "Familia imeamua kuwagusa watoto wenye ugonjwa wa moyo kwa sababu pia ya kumuenzi Kapteni Komba, maana kama mnavyojua na yeye alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo hadi kufikwa na mauti".

Kuhusu Familia kujenga Makumbusho ya Kapteni Komba, Mama Salome Komba alisema, Familia inafanya hivyo kwa sababu maisha ya Kampteni Komba yalikuwa ni ya kuacha Alama wakati wote.

"Kapteni Komba, alifanya mambo mengi makubwa kwenye taifa hili, ambayo tusipoyahifadhi na kuyatunza vizuri, tutayapoteza na vizazi vya sasa na baadaye havitapata kuyajua na kujifunza. 

Kwa sababu hiyo sisi Familia tukaona umuhimu wa kutengeneza 'Captain Komba Museum' ambapo hapo vizazi na vizazi watapata Historia yake kwa undani, Harakati zake, Uongozi wake, Tenzi za nyimbo zake mbalimbali na mambo mengi yamuhusiyo pamoja na maisha yake ya Uzalendo kwa Taifa lake", akasema Mama Salome Komba.

Mama Salome Komba alisema kumbukuzi itakayofanyika Februari 28 mwaka huu siyo ya kwanza bali ni mwendelezo wa kumbukizi ambazo Familia imekuwa ikizifanya tangu Hayati Kapteni Komba alipofariki dunia  Februari 28, 2015.

"Kila tarehe 28 ya mwezi wa pili, tumekuwa na utaratibu wa kuadhimisha siku ya Kumbukizi ya Kifo cha Kapteni Komba na tumekuwa tukifanya hivyo kwa namna tofauti tofauti ili mradi siku hii isipite bila kufanya kitu cha alama kwa watu na Jamii kama alivyopenda kufanya yeye Mwenyewe. Maisha yake yote alijitoa kwa ajili ya kuwatumikia watu, Serikali na Chama chake", akasema Mama Salome Komba.

Alisema, mwaka 2016 ambao ulikuwa wa pili baada ya kifo cha Kampeni Komba, familia ilifanya uzinduzi wa Kitabu 'MAISHA YA MZALENDO JOHN DAMIANO KOMBA', uzinduzi ambao Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Awamu ya Nne Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.

Kitabu hicho chenye kurasa 58, Dibaji yake iliandikwa na Mzee Rashid Mfaume Kawawa mwaka 2002, na kimesheni mwa kutosha historia karibu yote ya Marehemu John Komba.

Mwaka 2018, Harison Mwakyembe wakati huo akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, aliweka jiwe la msingi la Makumbusho ya Kaptain John Komba na mwaka jana 2023, Familia ilijenga Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi alilokuwa akiishi Kapteni Komba. tawi hilo lilifunguliwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam Abbas Mtemvu.

Akihitimisha, Mama Salome Komba, alisema; "Mwisho kabisa tunaomba tunaiomba Serikali, Chama Cha Mapinduzi na Watanzania wote Wazalendo, wenye mapenzi mema kwa nchi, Mashabiki wa Kapteni Komba na Wote watakaouguswa na 'Movement' hiii ya Kijamii yenye malengo mazuri watuunge mkono.

Mama Salome Komba aliwaomba watakaoguswa kulisapoti tukio hilo la Kumbukizi ya miaka 9 ya kapteni Komba kuiunga mkono familia kwa kutuma michango kupitia Benki ya NMB, namba 22510095134 -  Kikundi cha Captain Komba Museum.

Mama Salome Komba alisema Familia pia ipo tayari kupokea mchango au ushauri, hivyo atakayeguswa atumie na namba za simu 0754260881 - Salome Andrew Komba (VODA), 0715260881 Salome Andrew Komba (TIGO) au 0784260881 salome Andrew komba (AIRTEL).

Alisema, tangu hekaheka za maandalizi zianze tayari wadau na wenye mapenzi mema na kapteni Komba wameshaanza kutoa michango yao ya mawazo na fedha taslimu katika kufaninisha yote yaliyopangwa yakamilike.

Katika mkutano wa leo na Waandishi wa habari mdau mmoja aliyewahi kuwa kiongozi wa serikali katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara moja Injinia Juliana Pallangyo aliitikia mwito wa Familia ya Kapteni Komba na papo hapo akamkabidhi Mama Salome Komba fedha taslimu sh. 100,000 na kuahidi kutoa mchango mwingine wa sh. milioni 2.

"Kwa dhati kabisa leo nitatoa sh. lakini moja (100,000) na pia naahidi nitachangia sh. milioni 2. hii ni kwa sababu nimeguswa kutokana na kuutambua mchango mkubwa alioukuwa akiutoa Kapteni Komba katika maeneo na ngazi mbalimbali kupitia utunzi na uimbaji nyimbo zilizohamasisha uzalendo, mshikamano huku zikiburudisha watu wa rika zote bila kujali itikadi zao za kisiasa", akasema Injinia Juliana.

Pia katika mkutano huo alihudhuria mmoja wa Wasanii wa TOT ambaye alikuwa akiimba sauti ya pili kuunguruma pamoja na sauti ya kwanza ya Kapteni Komba, ambaye alieleza umahiri wa Kapteni Komba ulivyoweza kuinua wasanii wengi ndani na nje ya TOT hivyo kufanya aendelee kukumbukwa.

"Hakika Kapteni Komba alikuwa mwimbaji mahiri maana baada ya kifo chake, sote tuliokuwa tumebaki TOT kulijaribu kuiga sauti yake, lakini hakuna aliyeweza kuziba pengo". akasema Corbinian Mkinga.

Salome Komba, Mjane wa hayati Kapteni John Komba akizungumza na Waandishi wa Habari, nyumbani kwake, Mbezi Beach kwa Komba, Tangi Bovu jijini Dar es Salaam, leo Januari 29, 2024. Kulia ni Elias John Komba, kitindamimba wa Hayati Komba.
Salome Komba, Mjane wa hayati Kapteni John Komba akizungumza na Waandishi wa Habari, nyumbani kwake, Mbezi Beach kwa Komba, Tangi Bovu jijini Dar es Salaam, leo Januari 29, 2024. Kulia ni Elias John Komba, kitindamimba wa Hayati Komba na kushoto ni Corbinian Mkinga aliyekuwa akiimba sauti ya pili kuunguruma na sauti ya kwanza ya Kapteni Komba katika kundi la Tanzania One Theatre (TOT).
Salome Komba, Mjane wa hayati Kapteni John Komba akionyesha Kitabu 'MAISHA YA MZALENDO DAMIANO JOHN KOMBA' kilichozinduliwa na Rais wa Awamu ya Nne Dk. Jakaya Kikwete katika kumbuzi ya Kapteni Komba mwaka 2016. Kulia ni Elias John Komba. Abdallah Kaniki wa ITV akisoma kitabu 'MAISHA YA MZALENDO JOHN DAMIANO KOMBA'
Corbinian Mkinga aliyekuwa akiimba sauti ya pili kuunguruma na sauti ya kwanza ya Kapteni Komba katika kundi la Tanzania One Theatre (TOT), akizungumza machache kuhusu Hayati Kapteni Komba.
Salome akimtambulisha Eliasi John Komba kwa waandishi wa habari.
Mdau Injinia Juliana Pallangyo akimkabidhi Mama Salome Komba fedha taslimu sh. 100,000 na kuahidi kutoa mchango mwingine wa sh. milioni 2.
Injinia Juliana Pallangyo akizungumza.
Nyumbani kwa Hayati John Komba.

©2024 Official CCM Blog/Bashir Nkoromo

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages