LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 12, 2024

KUFUNGWA KWA MPAKA RWANDA NA BURUNDI NANI ATAUMIA?


 Katika hotuba yake ya kufunga mwaka jana, Rais Evariste Ndayishimiye alidokeza kuwa nchi hiyo inaweza kufunga tena mipaka yake na Rwanda na uamuzi huo ulianza kutekelezwa jana Alhamisi.

Wakati huo Ndayishimiye alisema: “Tunakumbuka furaha waliyokuwa nayo Wanyarwanda walipoliona tena Ziwa Tanganyika, walipata tena mukeke [Samaki wa ziwa Tanganyika], na sasa nchi ya Rwanda imerudisha mambo nyuma.

"Tulichoamua ni kwamba sasa tutachukua hatua zote ili Warundi wasiuliwe tena na wahalifu."

Mamlaka ya Burundi imeishutumu Rwanda kwa kulisaidia kundi la RED-Tabara kuvuruga usalama na kuua watu nchini Burundi katika mashambulizi ya hivi karibuni, Rwanda ilikanusha shutuma hizo.

Uamuzi mpya wa kufunga mpaka sio uamuzi pekee uliochukuliwa na Burundi. Waziri wa utawala na usalama nchini Burundi, Martin Nigetes, katika mkutano na mamlaka katika jimbo la Kayanza, alisema kuwa Wanyarwanda hawahitajiki nchini Burundi.

Akasema: “...Hatuhitaji watu wao wenyewe, na wale waliokuwa hapa kwenye ardhi hawatakikani”.

Sio uamuzi uliofurahiwa

Warundi na Wanyarwanda waliozungumza na BBC kuhusu uamuzi huu walionyesha kuwa ingawa mamlaka ya Burundi ina sababu za kuchukua uamuzi huu, wanaona kuwa ni hatua ya kurudi nyuma.

Mwaka mmoja uliopita, Mrundi Aimé Claude Nkurunziza alianzisha upya biashara kati ya Kigali na Bujumbura kupitia njia ya ardhini, baada ya miaka mingi ya kutofanya kazi kwa sababu ya hali ya uhusiano kati ya serikali hizo mbili.

Katika ujumbe wake kwa BBC Idhaa ya Maziwa Makuu akiwa Bujumbura alisema: "Mambo yalianza kwenda vizuri, sasa tazama. Hii haifaidi mtu yeyote, usalama ni sawa, lakini serikali zote mbili zinajali jinsi tunavyoishi. Nadhani haitakiwi kufungwa tena.”

Honorine Gatesi, anayeishi katika jiji la Huye kusini mwa Rwanda, pia anasema karibuni alianza kusafiri hadi Ngozi nchini Burundi kuwatembelea wanafamilia wake.

Aliiandikia BBC: “Sasa mimi pia nimenyimwa haki ya kuwatembelea binamu zangu, hawawezi kuja hapa na hatujui hii itachukua muda gani. Imepita zaidi ya miaka mitano tangu tulipowaona jamaa zetu mara ya mwisho. Ni jambo la kusikitisha.”

Kati ya 2015 na 2022, Burundi ilifunga mpaka wake na Rwanda

Katika mitandao ya kijamii, wengi wameeleza kuwa kufungwa kwa mipaka kunawaumiza watu wanaofanya biashara zaidi, pamoja na uchumi kwa ujumla.

Kati ya mwaka 2015 na 2022, Burundi ilifunga mpaka wake na Rwanda, raia wa Burundi anayevuka kwa njia ya ardhini aliruhusiwa kwenda Rwanda kwa kibali cha maandishi kutoka kwa serikali.

Safari za ndege za Rwandair pekee hadi Bujumbura hazikusitishwa wakati huo, na watu walioweza kukata tiketi waliendelea na safari kati ya nchi hizo, jambo ambalo wengine walisema kuwa kufunga mipaka ya nchi kavu ni kuwakandamiza wanyonge badala ya wenye nguvu kutokana na sababu za kukosekana kwa utulivu.

Bado haijajulikana ikiwa uamuzi mpya wa kufungwa kwa mpaka unawaathiri tu wale wanotumia usafiri wa magari.

Watawala wa Burundi wanasema wanachoweka mbele ni usalama wa watu nchini humo, na wanaituhumu Rwanda kuwa wanaouvuruga usalama wake wanatoka huko shutuma ambazo serikali ya Rwanda inazikanusha.

Mzozo wa muda mrefu

Mzozo wa hivi majuzi kati ya serikali ya Gitega na Kigali ulianza mwaka wa 2015 baada ya wale waliojaribu kuipindua serikali ya Rais wa zamani Pierre Nkurunziza walioongozwa na Jeneral Godfroid Niyombare kukimbilia Rwanda.

Niyombare ni mmoja wa viongozi wa mamlaka ya Burundi wanaoendelea kusema kuwa Rwanda haitaki kumkabidhi ili ashtakiwe na mahakama nchini Burundi. Mwaka jana, Rais Ndayishimiye aliiambia BBC: "Wakati wote ambapo hawajakabidhiwa kwetu tatizo bado halijatatuliwa."

Rwanda haikanushi kuwahifadhi baadhi ya watu waliojaribu kufanya mapinduzi Burundi waliotoroka mwaka 2015, na mamlaka ya Burundi inasema kuwa mazungumzo ya kuwakabidhi mwaka jana "yalikuwa yameendelea sana".


Jenerali Niyombare, chanzo kikuu cha mzozo kati ya nchi hizo mbili tangu 2015

Wiki iliyopita, katibu mkuu wa chama tawala nchini Burundi CNDD-FDD RĂ©vĂ©rien Ndikurio, aliwaambia waandishi wa habari: “Tulidhani yameisha, tungeona imebaki ndege au gari tu, lakini baadaye tukaona zimesimama."

Rwanda haijasema lolote kuhusu hili, haijabainika ikiwa ni kweli ilitokea, au kwa nini iliisimamisha. Kinachojulikana ni kwamba kumekuwa na mazungumzo tangu 2022 kati ya wawakilishi wa nchi hizo mbili, na uhusiano huo ulionekana kuwa mzuri, hadi hivi karibuni.

Shambulio la RED-Tabara ni tatizo nchini DRC

Katika vita vya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, serikali ya Gitega ilishutumiwa kwa kutuma wanajeshi kwa siri kusaidia vikosi vya serikali ya Kinshasa kupambana na waasi wa M23. Huku serikali ya Kigali ikisemekana kulisaidia kundi la M23. Watawala wa Burundi walikanusha hili, sawa na Rwanda ilivyokanusha.

Ni ripoti ya hivi punde tu ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa inayosema kuwa majeshi ya nchi hizi mbili yanapigana upande wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baadhi ya wachambuzi wanahusisha hali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na mdororo wa kurejeshwa kwa uhusiano kati ya Burundi na Rwanda, pamoja na kurudi nyuma kwa mazungumzo ya kurejesha uhusiano.

Shambulizi la mwezi uliopita la RED-Tabara liliwaua raia nchini Burundi na wengine wanasema ndio chanzo cha mambo kufika hapo walipo leo.

Je hatma ni ipi?


Kati ya 2015 na 2022, mipaka ya nchi hizi ilipofungwa, mashirika ya kiraia yalikomesha shhughuli zao, baadhi ya wafanyabiashara kwenye mipaka walifilisika na kufunga biashara zao.

Wataalamu wa masuala ya uchumi wamesema kuwa huu ni mgogoro mkubwa zaidi katika historia ya hivi karibuni ambao umekuwa na athari mbaya sana kwa watu wa Rwanda na Burundi.

Kuna hofu kubwa kwamba hali itazidi kuwa mbaya tena ikiwa hakuna kitakachofanyika ili watu wa nchi hizi zinazoonekana kuwa maskini sana waweze kufanya biashara.

Katika mtandao wa Facebook, Kevin Mugabo aliandika: “Hii ni moja ya ishara ya jinsi mkoa wetu ulivyo nyuma. Je, suala la kisiasa katika ngazi hii linawezaje kuwanyima watu wa nchi haki zao za msingi?”

Carine Ivy katika X (zamani Twitter) alisema: "Viongozi wetu wanapaswa kuweka masilahi ya kisiasa kando na kufikiria juu ya masilahi ya watu."

Fabien Igiranez kwenye X pia alisema: "Ikiwa tatizo la Congo halitatatuliwa, ni vigumu kwa CPGL kupata amani".

Honorine Gates aliiambia BBC: "Waathiriwa wa haya yote ni sisi wachache. Watawala wote hao hawana haja ya kuvuka Akanyaru[mpaka wa Burundi na Rwanda], sisi ndio tunaohitaji."

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages