Na Lydia Lugakila,
Karagwe.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera Julius Kalanga Laizer amekerwa na kitendo cha Polisi kutoa kibali kwa mtuhumiwa wa ubakaji kwenda Nchini Uganda kwa madai ya kumpeleka mtoto wake shule ikiwa alitakiwa kulipoti Polisi huku akiagiza kufanyika uchunguzi na kuwabaini Askari Polisi walioshiriki kutoa kibali hicho kwa mtuhumiwa aliyembaka mtoto wa miaka 10 Mwanafunzi wa Darasa la tano.
Dc Laizer alitoa kauli hiyo Januari 25, 2024 katika kikao cha Baraza la Madiwani cha Robo ya pili kwa mwaka 2023/2024 kilichofanyika katika ukumbi wa Angaza Wilayani humo.
Mkuu huyo wa Wilaya Alisema kuwa Jeshi la Polisi Wilayani humo linapaswa kujitathimini juu ya majukumu yao ikiwa ni kutokana na tukio la kikatili kama hilo lililotokea Januari 2, 2024 na kisha mtuhumiwa kufikishwa Polisi ambapo alipata taarifa mnamo Januari 9 mwaka huu hali iliyoonyesha viashiria vya vitendo vya Rushwa.
"Polisi ifuatilie suala hili kwa haraka na kwa ukaribu na mazingira yanaonyesha kulikuwa na majadiliano na kilichonisikitisha mtu anakamatwa amepewa dhamana na siku ya Jumatano anaenda Polisi kuomba ruhusa kupeleka mtoto wake shule Nchini Uganda ile hali alitakiwa kuonekana kituo cha Polisi siku ya ijumaa sikubaliani na hili" alisema Dc Laizer.
Kufuatia hali hiyo Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama Wilayani humo kufuatilia na kuona kulikuwa na ulazima gani kwa mtuhumiwa wa ubakaji kwenda nje ya Nchi huku akitaka vyombo hivyo kufanya kazi na kuwabaini mara moja kama wapo waliohusika na hatua kali kuchukuliwa dhidi yao.
Aidha amemuagiza Mkuu wa Polisi kushirikisha taasisi zote kabla ya maamuzi kutolewa na kumtaka kesi zote za ukatili wa Kijinsia zilizo kwenye Kata ziondolowe na kufikishwa mahakamani.
Aidha nao Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe baada ya taarifa ya Serikali wameungana kwa pamoja kukemea vitendo vya ukatili vinavyojitokeza na kuvitaka vyombo vya Dola kutowaruhusu kwa haraka watuhumiwa wa matukio ya ubakaji na ulawiti kwani kuachiwa haraka itapelekea Wananchi kuanza kujichukulia Sheria mikononi.
Viongozi hao wameamua kuungana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kamati ya ulinzi na usalama ili kudhibiti vitendo vya ubakaji kwa watoto kama walivyozuia na kudhibiti mauaji ya watu wenye Ualibino.
Wakijadiliana kwa pamoja madiwani hao akiwemo Diwani wa Kata ya Chonyonyo Anord ,Jane Bilalo diwani viti maalum Nyakasimbi,Zidna Murshid wa Kata ya Kituntu na Rongino Willbard kutoka Kata Chanika wamekemea vikali na kusema ipo haja ya Wananchi kuungana na serikali kuanza ujenzi wa bweni la Wanafunzi katika kila tarafa ili kutokomeza na kukomesha vitendo vya ukatili na ubakaji kwa watoto.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Wallece Mashanda katika ufunguzi wa kikao hicho alisema kuwa vitendo vya mimba za utotoni,Ubakaji na Ulawiti vimekuwa changamoto na ni suala la aibu kwani wanaofanya vitendo hivyo vinapaswa kudhibitiwa mara moja.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇