Upanga, Dar es Salaam
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye ni Mkurugenzi wa Tisha Mama Foundation Janeth Mahawanga, amemshukuru na kumpongeza sana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo amekuwa akiwezesha makundi ya Vijana na kinamama kiuchumi na kuahidi hatokuwa nyuma katika kumuunga mkono Rais kupitia Taasisi yake hiyo ya Tisha Mama Foundation na Ofisi ya Mbunge.
Amesema, ni katika kutokuwa nyuma kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia, ndiyo sababu Tisha Mama Foundation na Ofisi yake ya Mbunge imekuwa ikitoa mchango mkubwa kuhakikisha kituo cha Mafunzo ya Uchoraji kwa Mabinti na Vijana cha Don Bosco kinasimama imara na kinakwenda kuleta tija kubwa kwa kuibua vipaji kwa wengine.
Mbunge Mahawanga ambaye amekuwa kila mara akionyesha juhudi za kuinua jamii hasa Mabinti, vijana na kinamama, alisema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akizindua Program ya Sanaa ya Uchoraji kwa Mabinti na Vijana katika Kituo cha Don Bosco, Upanga jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi huo ulikuwa wa kishindo kwa kuhudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wakiwemo Madiwani wa Viti Maalum katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Diwani Kata ya Mbezi Juu, Meneja wa Miradi Benki ya CRDB Baraka Kiyalo, Viongozi wa Serikali za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na wadau mbalimbali wa masuala ya uwezeshaji kiuchumi Mabinti, wanawake na Vijana.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mbunge Mahawanga aliwataka Mabinti na Vijana wenye vipaji na mawazo ya maendelo katika mkoa wa Dar es Salaam, kujitokeza ili Taasisi hiyo ya Tisha Mama Foundation iweze kuwasaidia kugeuza vipaji na mawazo yao kuwa fursa ya kujikwamua kiuchumi.
Mbunge Mahawanga aliahidi kuwa kila watakaojitokeza atakuwa nao bega bega kuwasaidia hadi kufikia lengo lake kubwa la kuhakikisha mabinti na vijana wanajikomboa kiuchumi kupitia fursa zinazopatikana ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Aidha Mbunge Mahawanga alionyesha furaha yake na kueleza namna ambavyo Tisha Mama Foundation ilivyoona kipaji cha pekee cha Uchoraji cha Binti Mhellepu Shillingi na hivyo kumpa Tuzo ambapo sasa amekuwa Mwalimu na sehemu ya Mabinti wengine ambao wameanza kupatiwa mafunzo ya uchoraji.
Alisema mabinti hao wengine ambao wameanza kupatiwa mafunzona na kufikia katika hatua nzuri hadi Aprili mwakani (2024) watakuwa wamehitimu na bila shaka watakwenda kuwa chachu ya kuwasaidia Mabinti wenzao na vijana kwajumla.
Meneja Miradi wa Benki ya CRDB, Kiyalo, alimpongeza Mbunge Mahawanga kwa jitihada za Tisha Mama Foundation katika kusaidia jamii hasa Mabinti, Vijana wa kiume na Wanawake na kusema benki hiyo ipo tayari kusaidia jamii kupitia taasisi hiyo ili kufanikisha ndoto zao na kuwafanya wanufaike na fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo mikopo isiyo na riba ya 'Imbeju'.
Hali kadhalika, Madiwani wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na waliipongeza Tisha Mama Foundation hususan Mbunge Mahawnga kwa jitihada kubwa zinazofanyika kuwasogeza karibu na fursa na kuwataka wasichana hao walioanza kupata mafunzo hayo kueneza fursa hiyo kwa wenzao wengine.
Madiwani hao waliahidi kushirikiana bega kwa bega na Mbunge Mahawanga sanjari na Taasisi ya Tisha Mama Foundation kwenye maeneo yao kuibua vipaji mbalimbali vya Mabinti na Vijana na kuangalia namna bora ya kuwawezesha.
Mkufunzi wa Uchoraji Mhellepu kwa upande wake aliishukuru Tisha Mama Foundation kwa kuwawezesha kimafunzo na kwamba dhamira yao ni kuwa wachoraji wakuwa wa kimataifa na kutumia vipaji vyao kuwa fursa ya ajira katika maisha yao.
Alihitimisha Mkuu wa Kituo cha Don Bosco Upanga, Father Peter Mkechura, akisema kituo hicho kinaishukuru Tisha Mama Foundation kwa kuwa mdau muhimu kusaidia Mabinti hao kutimiza ndoto zao na kuomba jamii kusaidia watoto wenye vipaji kuonyesha taranta walizonazo.
Habari Picha👇
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Tisha Mama Foundation Janeth Mahawanga akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Tisha Mama Foundation Janeth Mahawanga (mwenye fulana nyeusi) akifurahi na Mabinti wanaopata mafunzo ya Uchoraji Kituo cha Don Bosco, wakati wa hafla hiyo.Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Tisha Mama Foundation Janeth Mahawanga (katikati-walioketi) akiwa na baadhi ya viongozi mwishoni mwa hafla hiyo.




No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇