JUMLA ya watoto elfu sabini na tisa wenye umri wa miaka mitano hadi miaka kumi na nne, wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa kichocho na na ugonjwa wa minyoo katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, anaripoti Respice Swetu.
Akizungumza wakati wa kikao cha maandalizi ya utoaji wa chanjo hizo, mratibu wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu Hussein Pengu amesema, chanjo hizo zitawahusu watoto wote wenye umri wa miaka mitano hadi umri wa miaka kumi na nne walio shuleni na walio nje ya shule.
Ameongeza kuwa, ili kupata takwimu sahihi za watoto watakaopatiwa chanjo hizo, utaratibu wa kuwaingiza katika rejesta maalumu utatumika.
"Kutakuwepo na rejesta za aina mbili, rejesta moja itatumika kwa ajili ya watoto walio shuleni na rejesta ya pili itatumika kwa watoto walio nje ya shule', amesema.
Pengu amevitaja vituo vitakavyohusika katika utoaji wa chanjo hizo kuwa ni shule za msingi na kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Zoezi hilo lililopangwa kufanyika Novemba 24, linaratibiwa kwa ushirikiano wa idara ya afya na idara ya elimu katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu,
Ili kufanikisha zoezi hilo, afisaelimu msingi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu, Elestina Chanafi, amewataka walimu kutoa ushirikiano wa kutosha wakati wa zoezi hilo.
'Kama ilivyo ada hasa katika utoaji wa dawa za kichocho, watoto watatakiwa kula shuleni, kila shule iandae chakula cha watoto kulingana na mazingira yake', amesema.
Sanjali na halmashauri ya wilaya ya Kasulu, zoezi hilo linatekelezwa katika halmashauri zote nane za mkoa wa Kigoma.
Utoaji wa chanjo hizo pia unafanyika kwenye halmashauri za mikoa ya Mwanza na Kagera zilizo na kiwango kikubwa cha maambukizi ya magonjwa hayo.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇