Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe, Adam Malima (wa tatu kulia), akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Tawi jipya la Benki ya NMB Dumila lililopo mkoani Morogoro, wengine katika picha ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka (wa tatu kushoto), Afisa Mkuu Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa pili kulia), Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya NMB, Rahma Mwapachu (kulia), Meneja Uendeshaji Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dodoma, Lilian Silaa (kushoto) na wa pili kushoto ni Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango.Meneja Tawi la NMB Dumila, Innocent Kato alimwelezea Mhe, Adam Malima kuhusu huduma zilolewazo na Tawi la NMB Dumila baada ya uzinduzi rasmi.
Sehemu ya wageni waalikwa Waliohudhuria uzinduzi wa Tawi la NMB Dumila.
Wananchi wa Mji wa Dumila wilaya ya Kilosa wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kati ya kilometa 35 hadi 70 kufuata huduma za kibenki, baada ya benki ya NMB kufungua tawi la NMB Dumila.
Akizungumza katika uzinduzi
wa tawi hilo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert
Mponzi amesema wananchi wa Dumila na vijiji vinavyoizunguka walikuwa
wakilazimika kusafiri umbali wa kilometa 35 kwenda Mvomero kufuata huduma za
kibenki wakati kwenda Gairo kilometa 50, Kilosa kilometa 69 na Turiani kilometa
70.
Ameongeza kuwa,kufunguliwa
kwa tawi hili inafanya NMB kuwa na matawi 231 nchi mzima na kuendelea kuongoza
kwa kuwa na matawi mengi kuliko benki yoyote hapa nchini na kuishi maana halisi ya kauli mbiu
yao ya NMB Karibu yako.
Mgeni rasmi katika ufunguzi
huo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima amesema, benki hiyo inawafikia
wananchi wengi na kuwaomba wananchi kutumia benki hiyo, kwa sababu Dumila ina
shughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo kilimo na ufugaji.
Mhe. Malima amesema, uwepo wa
tawi hilo katika Mji wa Dumila utaongeza tija kwa wakulima kupata mikopo ya
kilimo lakini na wafugaji kupata mikopo ya kunenepesha mifugo, ili jamii
inayoizunguma benki hiyo kunufaika kihuduma na kubadilika kiuchumi kwa mitaji
yao kukua kwa sababu, Dumila sasa ni Mji wenye shughuli nyingi za kiuchumi kwa
kukuza biashara zao.
Mhe.Malima alisisitiza kuwa
Dumila ni miongoni mwa miji ya kibiashara unaokua kwa kasi na kwamba ukubwa wa
mtandao wa NMB, uimara wake kimapato na huduma rafiki kwa wateja, vinaenda
kuneemesha na kuwastawisha kiuchumi wafanyabiashara, wajasiriamali, wakulima na
wafugaji wa kada zote watakaotumia fursa hiyo.
Alimaliza kwa kuipongeza NMB kwa lengo lake la kukopesha kiasi cha Sh. Bilioni 1 kwa wajasiriamali, wafanyabiashara, wakulima na wafugaji kwa mwaka wa kwanza, huku akiwataka wana Dumila, Kilosa na Morogoro kwa ujumla, kuchangamkia fursa za ujio wa tawi hilo alilolitabiria kuwa kinara kimafanikio kuliko matawi yote ya mkoa huo.
Wakati huohuo, Benki ya NMB
kupitia sera yake ya uwajibikazi kwa jamii, imetumia fursa hiyo kutoa meza 30
na viti 30 kwa ajili ya walimu wa Shule ya Sekondari ya Sokoine na madawati 53
kwa shule ya Msingi Kwadoli vyote vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 11.




No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇