MADEREKA AJIBIWA KUHUSU MAKONDA, ADAIWA ANAJITOA UFAHAMU, ASIWARUBUNI WANANCHI, AWAAMBIE UKWELI
3 Novemba, 2023
Hivi karibuni nimeona clip ya Wakili Peter Madereka akielezea maoni yake kuhusu agizo la Chama cha Mapinduzi kwa Kada wake, Mhe Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 kuhusu kumaliza migogoro ya ardhi nchini.
Madereka anajitoa ufahamu tu. Anajua kuwa:
1. Serikali, kwa mujibu wa Katiba yetu, huundwa na Chama cha siasa kilichoshinda uchaguzi. Mzazi hapa ni Chama na Serikali ni mtoto.
2. Chama ndicho kinachagua wagombea wake wa uchaguzi Mkuu. Wanaomba ridhaa ya Chama ili kugombea nafasi mbali mbali za uchaguzi ili kuunda Serikali.
3. Chama ndicho kinaingia kwenye mkataba wa kuongoza nchi, kwa kupitia wakala wake, yaani SERIKALI. Chama ndicho kinaongoza nchi kupitia wakala wake, yaani Serikali. Ni vema hili likaeleweka vizuri.
4. Hivyo, Chama kinaunda Serikali yake na kuikabidhi ilani yake kwa ajili ya utekelezaji. SERIKALI INATEKELEZA ILANI YA CHAMA ambayo ndio mkataba baina ya Chama na Wananchi waliokipa Chama ridhaa ya kuongoza nchi.
5. Afrika Kusini, wakati Rais akiwa Thabo Mbeki na Mwenyekiti wa Chama cha ANC akiwa Jacob Dzuma/Zuma au JUMA huku kwetu, Thabo aliposhindwa kuitekeleza vema ilani ya Chama cha ANC, walimuondoa madarakani. Chama ndicho chenye mkataba.
6. Hapa kwetu, kuondoa sintofahamu hiyo na kuongeza kasi ya utekelezaji wa ilani, Rais anapewa Uenyekiti wa Chama. Anavaa kofia mbili.
7. Makonda ni Mwenezi. Ni Msemaji wa Chama, mbali na Mwenyekiti na Katibu Mkuu. Mfano, kuwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, hakumfanyi Rais au Waziri Mkuu kutotoa taarifa au maelekezo. Hivyo, Mwenezi wa CCM anapotoa maagizo, yana baraka za Chama. Haongei yeye, kimeongea Chama kwa vile yeye ndiye mdomo (wa kusemea) wa Chama. Haongei ya kwake. Bwana Yesu alisema, akishapaa Mbinguni, atatutumia Roho Mtakatifu, naye HATAONGEA YA KWAKE BALI ATAKAYOSIKIA, maana yake yale atakayoambiwa, Yohana 16:13. Iwapo angeongea ya kwake, leo Makonda angeshachukuliwa hatua.
8. Baada ya maelekezo ya CCM kwa Mhe Waziri Mkuu, wakati Wakili Madereka anajitokeza hadharani kumlaani Mhe Makonda, kwa vile aliyeyatoa ni yule wasiyemtegemea, Mhe Waziri Mkuu yeye anafahamu, wanakutana (PM na Mwenezi au Serikali na CCM), PM anaiambia CCM/Makonda kuwa maagizo ya CHAMA nimeanza kuyatekeleza tangu jana. Na akatoa mwelekeo wa utekelezaji wa kutatua na kumaliza migogoro ya ardhi nchini.
Jana tarehe 2/11/2023, nikiongea na Afisa ardhi anayeshughulikia mradi wa viwanja vya Halmashauri ya Musoma Vijijini, Esther William Karatibu, kule Suguti Kwikonero, anakiuka taratibu na nilipomwambia nitalalamika kwa Mhe Said Mtanda, Mkuu wa Mkoa wa Mara, akanijibu kwa jeuri sana, “Mkuu wa Mkoa atanifanya nini miye, kamwambie.” Nilipomwambia kuwa yeye yu Mtumishi wa umma na anapaswa kuzingatia masharti ya utumishi wa umma, anasema “utumishi wa umma kitu gani, mimi ninajisimamia mimi kama mimi,” nikagundua ninaongea na wale wale wazua migogoro ya ardhi anaowasema Mhe Makonda.
9. Hivyo, Chama hakiwezi kwenda kusimamia utatuzi wa migogoro ya ardhi, KINAIAGIZA SERIKALI YAKE, wakala wake wa kutawala, kutekeleza hilo. Balozi Polepole pia aliifanya kazi hiyo. Alisikiliza migogoro ya ardhi na malalamiko mengine na KUWAELEKEZA viongozi wa Serikali kushughulikia kero hizo.
10. Madereka, kwa tafsiri ya Mkuu wa Mkoa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kumuweka ndani Makonda kama mwenezi, ndio, inawezekana kabisa. Anaweza akamwagiza RPC akamkamata. Lakini awe tayari kwa kitakachomtokea yeye baada ya kufanya hivyo. Ni sawa na Mzazi kukukabidhi silaha na watu wake ili uwalinde halafu wewe unaigeuza kwake. Ni mjinga tu ndiye anayeweza kufanya hivyo.
Humility au unyenyekevu kwa kiongozi ni tunu. Mhe Waziri Mkuu amesikia maelekezo ya Chama kupitia kwa Msemaji wake. Bila kuangalia aliyeyatoa ni nani, PM amekuwa na hekima, kama MTENDAJI, ameyapokea na kuanza kuyashughulikia mara moja. Anaelewa kuwa, ni CCM iliyoingia kwenye mkataba na wananchi wa kuwaongoza. Na yeye ni sehemu muhimu ya wakala wa utekelezaji wa Mkataba huo ambao ni ilani ya uchaguzi.
Ili upewe tena ridhaa, wananchi watataka kujua, mkataba baina yetu na CCM umetekelezwa kwa kiasi gani? Ndio maana hatua hii ya CCM kupitia maagizo aliyeyatoa Mwenezi Makonda, ni muhimu sana na ya msingi kabisa.
Akina Wakili Madereka wasijitoe ufahamu na kuwapotosha watu. Watanzania ni werevu na wanafahamu kuwa, WALIICHAGUA CCM KUWAONGOZA. CCM IKAWEKA WAKALA WAKE, SERIKALI, ILI KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA MKATABA BAINA YAKE NA WANANCHI. CCM NDIYO IMEUNDA SERIKALI NA INAISIMAMIA IUTEKELEZE KWA USAHIHI, KABLA YA KURUDI KUOMBA RIDHAA TENA. CHAMA NDIYE MZAZI NA SERIKALI NI MWANAYE.
AS-SALAAM ALEYKHUM,
JUMMAH MUBARAK ALLAHUMMA.
MAANDALIO MEMA YA SABATO KESHO NA DOMINIKA JUMAPILI.
AMINA🙏🏾
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇