LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 11, 2023

WAHARIRI WALIPOPEWA UNDANI WA MCHAKATO NA MANUFAA UWEKEZAJI BANDARI

Na Joe  Nakajumo
KILA uchao, ni bandari! bandari ! Ni bandari gani hiyo? Ni bandari zilizo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (Tanzania Port Authority - TPA).

Tanzania kuna bandari 90 katika bahari ya Hindi na maziwa yakiwemo Victoria,Tanganyika na Nyasa, na zote zipo chini ya usimamizi waTPA.Katika Bahari ya Hindi kuna bandari kwenye mabano(20), ziwa Victoria(30), ziwa Tanganyika(25) na ziwa Nyasa(15).

Ili kuleta ufanisi kwa lengo la kuongeza mapato na kuchangia kwa kiwango kikubwa bajeti ya serikali, Tanzania ilibidi ikune kichwa kuona namna gani huduma za bandari  hasa ya Dar es Salaam zitaimarishwa.

Uimarishwaji bandari ya Dar es Salaam ni jambo la msingi kwa sababu ni kitovu kinachohudumia mizigo ya nchi jirani  zinazopakana na Tanzania zisizokuwa na  bandari ambazo ni pamoja na  Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda, Uganda na eneo la mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo amvalo pia linategemea zaidi  bandari za Tanzania.

MCHAKATO WA UWEKEZAJI
Katika kutafuta ufumbuzi wa kuimarisha huduma za bandari hasa ya Dar es alaam, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba 25, mwaka jana 2022, ilisaini makubaliano kati yake na serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano, Tanzania na UAE, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Mwanasheria mbobezi katika sheria za Kimataifa Hamza Johari, mchakato wa kutafuta namna ya kuimarisha ufanisi bandari za Tanzania hasa ya Dar es Saaam ulianza mwaka 2018.

Kufuatia makubaliano, kati ya nchi hizi, UAE iliitambulisha kampuni ya nchini mwake ya DP World ambayo ina uzoefu mkubwa wa kuendesha bandari katika nchi mbali mbali duniani zikiwemo za Ulaya.

Hivyo, makubaliano ya Tanzania na UAE  ndio yaliyoweka msingi wa Mamlaka ya Bandari  Tanzania na DP World kuanza majadiliano ya kina kuhusu mikataba ya kufanya biashara kati ya pande hizo mbili.

MIKATABA KAMILI BADO
Mikataba ya kati ya TPA na DP World bado haijafikiwa, watalamu wa pande zote mbili wako katika mchakato wa kuitengeneza kwa maslahi ya pande zote, lakini upotoshaji mkubwa umeonekana kutokea baada ya hatua hizo za awali au za msingi katuka majubaliano ya uendelezaji bandari.

Katika upotoshaji uliozuka, baadhi ya watu hasa wanasiasa wa vyama vya upinzani wamelivalia njuga suala hili kwa kuudanganya umma wa Tanzania kwamba bandari ya Dar es Salaam inauzwa.

BANDARI  HAIUZWI
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ambae alisaini makubaliano kwa niaba ya serikali amekuwa akirudia mara kwa mara kuwahakikishia Watanzania kuwa bandari haiuzwi, haiuzwi, haiuzwi. Kwa upande wa serikali ya UAE, aliyetia saini alikuwa Ahmed Mohamed.

Katika mkutano wake na wahariri wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika Julai 14, katika hoteli ya Hyatt Kilimanjaro, mjini Dar es Salaam, Waziri Mbarawa alisema serikali ya Tanzania iliingia makubaliano na serikali ya UAE, kuendeleza bandari sio kuuza bandari.

Alifafanua kwamba makubaliano yanahusu kuendeleza kiwango cha ufanisi katika bandari ya Dar  es Salaam.

UFANISI  UPO CHINI
”Hali ya ufanisi wa bandari za Tanzania iko chini na bandari ya Dar es Salaam utendaji wake ni wa kiwango cha chini.”

Waziri alieleza kwamba katika bandari ya Dar es Salaam, mzigo unapakuliwa kwa siku tano kutoka kwenye meli, wakati viwango vya kimataifa unatakiwa upakuliwe kwa siku moja.

Profesa, alisema changamoto kubwa ni kukosekana mifumo  ya kisasa ya TEHAMA na kwamba gharama ya meli kusubiri nangani nje ya bandari ni sh. milioni 58 kwa siku.

LENGO LA SERIKALI
“Lengo la serikali ni kupunguza muda wa meli kusubiri, kupunguza muda wa kushusha makasha na kupunguza gharama za usafirishaji mizigo kwenda nje,” aliwaeleza Wahariri.

Mbarawa alisema DP World ina uwezo mkubwa wa uendeshaji bandari na yenyewe inamiliki meli 400, na lengo la kutaka kuitumia kampuni hii ni kuleta mapinduzi ya uchumi.

“Biashara ya bandari ina ushindani mkubwa, hivyo lazima kuwe na mtandao mkubwa,” alieleza Waziri na alizitaja baadhi ya bandari ambazo zinaendeshwa kwa kukodishwa kuwa ni Mombasa (Kenya), Walvis Bay (Namibia), Lobito (Angola), Tema (Ghana), na Morocco.

Waziri aliwafahamisha wahariri kuwa kampuni zinazoendesha bandari duniani ni kumi tu na DP World inashughilikia asilimia 10 ya biashara ya mizigo duniani.

UFAFANUZI WA MWENYEKITI
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano, Johari, alisema kazi ya kutafuta njia ya kuleta ufanisi katika bandari haijaanza jana wala juzi, ilianza miaka  kadhaa iliyopita mwaka 2018. Upembuzi yakinifu ulifanywa ili serikali iweze kupata mapato mazuri.

Alisema ufanisi wa utendaji wa bandari utachangia kiasi kikubwa katika bajeti ya serikali. Kwa sasa asilimia 37 ya bajeti ya serikali inatoka bandari ya Dar es Salaam

Johari alisema ukomo wa utendaji wa DP World utawekwa katika mikataba ya biashara itakayosainiwa kati  yake na TPA.

DP World itasajiliwa hapa nchini  na hisa asilimia 35 zitamilikiwa na wazawa  na kwamba bandari haijauzwa bali itakodishwa kama ilivyokuwa kwa TICTS ambayo ni kampuni ya Hong kong, China na Watanzania walikuwa na hisa ndani yake.

TICTS  iliingia mkataba wa kuendesha kitengo cha makasha bandari ya Dar es Salaam kuanzia mwaka 2000  na ulimalizika Disemba mwaka jana 2022.

ASILIMIA NANE
Kampuni ya DP World itapewa kuendesha asilimia nane tu ya shughuli zote za Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Johari alisema uwekezaji katika kuimarisha ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam, utaleta tija kwa sababu, nchi jirani Rwanda tayari imefungua bandari kavu nchini mwake yenye uwezo wa kuhifadhi makasha 50,000.Kampuni ya DP World ndio inayoendesha bandari hiyo.

Reli ya mwendo kasi (SGR) itakapoanza itasaidia kuongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam, kwa sababu itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo tani milioni 25 kwa mwaka.

Hivi sasa inajengwa na kipande cha kilomita 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kimekamilika na vipande vingine, kutoka Morogoro hadi Makutopora vinaendelea kujengwa.

SGR itakuwa kiungo cha usafiri wa haraka kati ya Tanzania na nchi jirani magharibi  zinazotumia bandari ya Dar es Salaam kupitishia mizigo yake.

HAKUNA ATAKAYEPOTEZA KAZI
Kwenye kikao hicho cha Waziri na wahariri, watendaji wa TPA, walieleza kwamba hakuna mfanyakazi wa bandari atakayepoteza kazi. ”TPA kuna  bandari kadhaa na hata hapo bandari ya  Dar es Salaam kuna nafasi za kazi.”

Ilielezwa kwamba makubaliano kamili  yanayohusu mikataba ya biashara ya ukodishaji kwa mwekezaji huenda yakakamilika katika kipindi cha miezi mine ijayo.

Juni  10, mwaka huu wa 2023, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliridhia Azimio la ushirikiano na UAE kuhusu uwekezaji wa bandari utakaofanywa na kampuni ya DP World.

Takwimu walizowasilishwa kwa wahairiri kuhusu utendaji wa bandari ya Dar es Salaam, zinaonyesha kuwa mapato  kwa mwaka 2021 yalikuwa sh. trilioni 7.6 ambapo  inakadiriwa yafikie sh. trilioni 26 mwaka 2030 na ajira zifikie watu 71,907 mwaka 2032/33 kutoka ajira  zipatazo 28,000 mwaka 2021.

Historia ya Dubai ambako  ni makao ya DP World, inaonyesha kuwa  kabla ya mwaka 1960, Dubai ilikuwa jangwa tupu, lakini sasa ni moja ya majiji  bora lenye utajiri mkubwa duniani.

Mafuta kwa  maana ya petroli yaligunduliwa, lakini petroli sio chanzo kikubwa cha mapato cha Dubai kwa sababu mapato yanayopatikana kutokana na petrol ni aslimia tano tu.

Chanzo kikubwa cha mapato Dubai ni biashara. Dubai ni kitovu cha biashara duniani.

Utawala wa Dubai ulifanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kuifanya kuwa kituo cha biashara.

Mwaka 1990 kulikuwa na jengo moja tu refu (sky scraper), kwa takwimu za mwaka 2020 kulikuwa na sky scraper 148 na majengo mengine marefu 917.

Moja ya sky scraper ni jengo la Burja  Khalifa lenye urefu wa mita 830 na jengo lingine refu Dubai ni Creek Tower mita 1,300 ujenzi wake ulianza mwaka 2016 na ulipangwa kukamilika mwaka 2021. Lakini kutokana na kuzuka ugonjwa wa Uviko 19 duniani, ujenzi ulisimama mwaka 2020.

Tanzania bara (Tanganyika) ambayo  ilipata uhuru kutoka udhamini wa Uingereza, Desemba 9, 1961, ina somo la kujifunza kutoka Dubai kuhusu kasi ya ukuaji uchumi.

Sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam.

Imeandikwa na Joe Nakajumo, Mhariri wa Habari  mstaafu wa Uhuru Ublications Ltd, Namba yake Whatsapp ni  0784291434 na email nakajumoj@gmail.com)

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages