Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Zaitun Msofe akitoa maelekezo ya Serikali katika mkutano wa baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa.
Na Lydia Lugakila
Kyerwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera Zaitun Msofe ametaka hatua kali za kisheria zichukuliwa kwa wale wote wanaojihusisha na uharibifu wa vyanzo vya maji katika sehemu mbali za Wilaya hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Meneja wa wakala wa Usambazaji maji na usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Kyerwa mhandisi Shukrani Tungaraza kuwasilisha taarifa ya maji katika kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri hiyo huku akibainisha baadhi ya sehemu zilizoonekana kukithili katika uchafuzi wa vyanzo vya maji.
Mhandisi Tungaraza alisema mradi wa maji Kagenyi Omukalinzi chanzo chake kimechafuliwa na watu wanaochenjua madini hali iliyosababisha mradi kusimama.
"Mradi wa maji Chanyangabwa eneo la kwenye chanzo kuna shughuli za ufugaji, mifugo inaingia kwenye chanzo na kuharibu chanzo hicho hali hii ikiendelea itasababisha kukauka kwa vyanzo vya maji ambavyo vimejengwa kwa thamani kubwa ya fedha za serikali" alisema Meneja huyo wa Ruwasa Kyerwa.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Zaitun Msofe alikiri kuwepo uharibifu wa vyanzo vya maji katika kata ya Songambele na kuwa hayuko tayari kuona hali hiyo ikiendelea na kuahidi kulibeba suala hilo na kulifanyia kazi mara moja huku akiwasisitiza madiwani wa Halmashauri hiyo kuwa makini katika hilo kwa kusimamia ili kuokoa vyanzo hivyo.
Hata hivyo upande wake Mbunge wa Jimbo la Kyerwa Innocent Seba Bilakwate alisema kuwa Serikali inasisitiza sana kulinda vyanzo vya maji ikiwa kuendea kunufaika na maji safi na salama huku akiwahimiza Wananchi kutunza vyanzo vilivyopo na vile vya zamani kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇