Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Katani Tanzania (TSB) Saddy Kambona katika mkutano na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma Agosti 16,2023.
Kambona amesema baada ya katani yetu kupimwa ughaibuni ikabainika kuwa katani ya Tanzania ina sukari mara dufu kuliko katani inayozalishwa Mexico.
Amesema baada ya kubainika hivyo wakajitokeza wawekezaji ili wajenge kiwanda nchini cha kuzalisha sukari, mpango ambao hata hivyo haujafanyika.
Kambona ameelezea historia ya zao hilo kama ifuatavyo:
Itakumbukwa kuwa zao la mkonge lina historia ndefu nchini. Ni zao ambalo liliingizwa Nchini Mwaka 1893 na Mtafiti wa kilimo raia wa Ujerumani anayefahamika kwa jina la Dkt Richard Hindolf ambaye alichukua mbegu za Mkonge kutoka Mji wa Yucatan Nchini Mexico.
Nchini Tanzania zao hili lilianzia Wilayani pangani Mkoani Tanga na baadaye kuenea katika mikoa ya Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara, Kilimanjaro, Arusha na maeneo mengine.
Mkonge ulikuwa unalimwa na wakulima wakubwa pekee waliokuwa wanamiliki mashamba makubwa (Estates/Plantations). Hakukuwa na wakulima wadogo wa Mkonge.
Uzalishaji wa Mkonge uliongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia mwaka 1964 Tanzania iliweza kuzalisha takriban Tani 230,000 na kuongoza Duniani kwa uzalishaji wa zao la Mkonge.
Kipindi hicho Mkonge
ulikuwa unachangia takriban 65% ya fedha za kigeni nchini kabla ya uzalishaji
kuanza kuporomoka kuanzia mwaka 1970 ambapo hadi kufikia Mwaka 1997 uzalishaji
wa Mkonge kwa Mwaka ulikuwa ni tani 19,000 tu.
Mwaka 2019 Serikali ililiingiza zao la mkonge katika orodha ya mazao ya kimkakati na kufanya zao hilo kuwa zao la saba la kimkakati. Mazao mengine ya kimkakati ni Pamba, Tumbaku, Kahawa, Korosho, Chai, Michikichi.
Zao la Mkonge
likaingizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025 ambamo limewekwa lengo
la kuongeza uzalishaji kutoka tani 36,000 zilizokuwa zinazalishwa kwa Mwaka
2020 hadi kufikia tani 80,000 kwa Mwaka, ifikapo Mwaka 2025.
Serikali ikaongeza lengo na kuiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania kuhakikisha kuwa uzalishaji unaongezeka hadi kufikia tani 120,000 kwa Mwaka, ifikapo Mwaka 2025/2026.
Hatua za Serikali kuliingiza zao la mkonge kwenye orodha ya mazao ya kimkakati ilitokana na ukweli kwamba mahitaji na soko la mkonge limezidi kuimarika duniani.
Hii ni kutokana kugundulika kwa matumizi
mapya ya Mkonge na uzalishaji wa bidhaa mpya zitokanazo na mkonge kama vile vifaa
vya ujenzi(gypsum boards, Matofali,mbao, mabati, vigae), Sukari ya Mkonge,
Pombe ya Mkonge, Karatasi maalum, Bio Gas, mbolea, Chakula cha mifugo , urembo,
mabodi ya magari n.k.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇