Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Hospital ya Royal Polyclinic iliyopo eneo la Mnazi mmoja, jijini Dar es Salaam, Jumapili, Julai 16 2023 itatoa bure huduma ya kupima tezi dume kwa mashine ya kisasa badala ya kutumia kidole kama ambavyo imekuwa ikifanyika kupima maradhi hayo.
Mmoja wa viongozi wa Hospitali hiyo iliyofunguliwa mwaka jana, Mohammed Nassoro amesema mbali na huduma hiyo ya kupima tezi dume itakuwepo pia fursa ya wananchi kupimwa bure magonjwa mengine kama Sukari, Presha, Joto, Uzito, Urefu na BMI kwa lengo la kuisaidia jamii.
"Sisi baada ya kubaini kuwa watu wengi wamekuwa wakisita kupimwa ugonjwa huu wa Tezi Dume kutokana na kadhia ya upimaji wa kutumia kidole katika njia ya haja kubwa, tumefanya jitihada hadi kupata mashine ya kisasa ya kupima tena kwa mda mfupi sana, hivyo wananchi wanaohisi kuwa na ugonjwa huo waje bila hofu", alisema Nassoro.
Alisema, mbali na upimaji wa tezi dume, Sukari, Presha, Joto, Uzito, Urefu na BMI, siku hiyo watakuwepo pia Madaktari Bingwa kutoa huduma, ambao aliwataja kuwa ni Daktari bingwa wa matatizo ya uzazi na magonjwa ya wanawake(OBS/Gynacologist), Daktari Bingwa wa watoto (Pediatrician), Daktari bingwa wa meno na kinywa (Dentist) na Daktari bingwa wa mfumo wa mkojo (Urologist).
Wengine ni Daktari bingwa wa matatizo ya ndani ya mwili (Physician) na Daktari wa kawaida (General Practitioner) na Wataalamu wa chakula na Lishe (Nutritionist).
Alisema, pamoja na hayo, pia Hospitali itapata nafasi ya Kuchangia Damu kupitia Shirika la Damu la Taifa ambao watakuwepo siku hiyo na kwamba upimaji magonjwa na huduma zote utaanza asubuhi hadi saa 9 Alasiri.
Kiongozi wa Hopsitali hiyo amesema atakayehitaji maelezo zaidi wanaweza kuwasiliana kupitia simu 0653 663 333 au 0777 663 333 au kwa kufuatilia taarifa kupitia kurasa za Kijamii za Instagram/ @royalpolyclinicdar.
Hospitali ya Royal Polyclinic iliyopo karibu na taa za kuongozea magari eneo hilo la Mnazi Mmoja, ilifunguliwa na Meya wa Jiji la Dar es Salaam Omar Kumbilamoto Julai 09, 2022 na kwa mujibu wa uongozi, hadi sasa inatoa huduma bora za kuaminika.
Dk.Bolonja Msangi wa Hospitali ya Royal Polyclinic akiandaa mashine ya kisasa ya kupima tezi dume katika Hospitali hiyi, Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam, leo. Mashine hiyo ndiyo itakayotumika kupima bure ugonjwa huo kwa wananchi watakaojitoza. (Picha na Bashir Nkoromo)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇