NA VICTOR MAKINDA, KILOMBERO
Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro, kimeiomba serikali kujenga miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji kwa ajili ya kukuza uzalishaji wa zao la mpunga na miwa wilayani hapa.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kilombero, Mohamed Msuya, wakati akizungumza na na CCM BLOG, Mji Mdogo wa Mang’ula wilayani Kilombero.
Msuya alisema kuwa wilaya hiyo imejaaliwa ardhi kubwa yenye rutuba na ifaayo kwa kilimo cha mazao ya aina mbali mbali hususani Mpunga na miwa huku changamoto ikiwa ni ukosefu wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji.
“ Wilaya ya Kilombero imejaaliwa kuwa na ardhi yenye rutuba, watu wenye ari ya kufanya kazi, changamoto ni ukosefu wa miundombinu ya umwagiliaji hali inayopelekea wakulima kulima kilimo kisicho na uhakika wa kuuvuna kwa kutegemea misimu ya mvua.” Alisema Msuya.
Msuya alisema kuwa karne hii ya Sayansi na Teknolojia, kutegemea mvua kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo, sio tu kunapunguza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara bali pia kunafifisha kasi ya maendeleo.
“Ninamuomba Mwenyekiti wangu wa Taifa wa Chma Cha Mapinduzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Kilimo inayoongozwa na kijana supavu,mwanamikakati, Hussein Bashe, itujengee miundombinu ya Kilimo cha umwagiliaji kwani vyanzo vya maji vipo vya kutosha, ardhi ipo na watu wenye jitihada za kufanya kazi wapo.” Anasema Msuya.
Msuya anaongeza kusema kuwa Kilombero ikijengewa miundombinu ya umwagiliaji ni wazi kuwa itakuwa kitovu kikubwa cha uzalishaji wa mazao yatakayokuza uchumi wa watu wa Kilombero na kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.
Katika hatua nyingine Msuya alisema kuwa CCM wilayani Kilombero ipo imara na inaendelea kutekeleza ilani kwa vitendo huku ikijiandaa kikamilifu kuelekea uchaguzi wa serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika mwaka 2024.
“ CCM Kilombero ni moja yenye umoja na mshikamano, tumevunja makundi yote na kwa sasa viongozi wa chama wanawasimamia vyema viongozi wa serikali kuhakikisha kuwa ilani ya chama inatekelezwa kwa vitendo hatua inayotuhakikishia ushindi katika chaguzi zijazo.” Anasema Mohamed Msuya.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇