LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 1, 2023

VIONGOZI WA DINI KAGERA WATAMANI RC FATMA MWASSA AANZE NA HAYA SUGU.


Na Lydia Lugakila, Bukoba.

Viongozi wa dini na madhehebu katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera wamekutana na kujadiliana na mkuu wa Mkoa wa Kagera Bi Fatma Mwassa huku shauku yao ni kutamani na kuona baadhi ya kero zilizoonekana sugu kwa muda mrefu zinafanyiwa kazi ili Mkoa huo uinuke haraka kiuchumi.


Viongozi hao wa Dini Wakiongea katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Mkoa huo wamesema wanaamini kuwa kiongozi huyo atajifunga mkanda na kutenda miujiza kwa kuazia alipoishia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Albert John Chalamila kwa kuanza na kero ya Stendi, Soko, upanuzi wa mji wa Bukoba, kumwondolea mkulima wa Kijijini makato na kodi katika kilimo, kuona namna ya kuwaondoa Wanyama aina ya Ngedere wanaoonekana maeneo ya mjini na kushambulia mazao ya Wananchi, pamoja na suala la uchafu utokanao uvunaji wa Senene na  mmomonyoko wa maadili kwa vijana.


Viongozi hao wa dini akiwemo Sheikh wa Mkoa wa Kagera Harouna Kichwabuta wameiomba Serikali kumfikilia mkulima wa Kijijini kwa kumpunguzia makato na kodi na kuwa mkulima hawezi kuendelea akiwa anakatwa na kukosa uhuru katika bidhaa zake ikiwa ni pamoja na kumfungulia mipaka ili apate kusafirisha bidhaa zake ili kujipatia kipato.


Sheikh Kichwabuta ameiomba pia Serikali kuona namna ya kurudisha na kuheshimisha somo la dini ili lifundishwe tena kama awali shuleni na mtihani wa somo hilo uingizwe katika orodha ya mitihani ya kitaifa na kumfanya anayelifaulu kupewe kipaumbele hali itakayosaidia kuwa na wasomi wenye maadili mema na kuondokana na maovu yanayoonekana kwa sasa ikiwemo mapenzi ya jinsia moja.


Naye Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania K.K.K.T Dayosisi ya Kaskazini Maghari Abedinergo Keshomshahara ameiomba Serikali kuona namna ya kufukuza Wanyama aina ya Ngedere kwani uchumi hauwezi kwenda mbele wakati mnyama huyo anaharibu kwa kuvuna mazao yakiwa machanga shambani huku akiweka ombi la upanuzi wa mji na kupatikana kwa uwanja Mkubwa wa ndege ili kuruhusu watalii wengi kuja Kagera kiutalii.


Kwa upande wake Padre Samweli Muchunguzi amemuomba Mkuu huyo wa Mkoa kuanza na muujiza wa kwanza wa Wanakagera kupata Soko la kisasa na Stendi nzuri ili uchumi wa Mkoa huo upande huku akisisitiza kuwepo namna nzuri  ya uvunaji wa Senene kwa kutumia mitambo ya kisasa kwani njia ya mabati inayotumika inachafua mji kutokana na Moto, moshi na uchafu mwingine unaotokana na senene hao.


Aidha akijibu hoja mbali mbali za Viongozi hao mkuu wa Mkoa huo Bi Fatma Mwassa ameahidi kuyafanyia kwa kuanza haraka na suala la kurudisha maadili kwa kulipambania suala la somo la dini kufundishwa mashuleni na kuwa ni vyema waandaliwe walimu wa masomo hayo wawepo muda wote.


Katika hatua nyingine mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa Wanakagera kupata soko na stendi suala hilo limezingatiwa Stendi itajengwa kwa kupitia mradi uitwao TACTIC unaotekeleza miradi hiyo katika Halmashauri 45 Tanzania ambazo zimegawanywa  katika makundi matatu ambapo awamu ya kwanza wanatekeleza katika Halmashauri 12 katika na bajeti ya mwaka 2023/2024 Manispaa ya Bukoba itaingia kwenye bajeti kundi la pili katika Halmashauri 15 ambayo utekelezaji wake ni mwaka 2024/2025 na kuwa kwa sasa hakuna fedha zilizotengwa kwa ajili ya kujenga soko bali kuna fedha kidogo ambazo wameanza nazo katika kujenga Stendi na kuahidi kuwa vyote hivyo vitakamilika.


RC Fatma Mwassa amesema atahakikisha anaondoa vikwazo na kero zinazowasumbua wananchi huku akikiri kuwa uchumi wa Kagera bado ni mdogo sana na mizunguko wa biashara sio mzuri.


Ameongeza kuwa Kuna baadhi ya masuala yaliyoyumba kipindi cha katikati na kuwa wataongeza nguvu katika utalii kwa kufungua Barabara zote, kuinua shughuli za uvuvi, na kuwa na  kilimo cha mazao yenye thamani huku upanuzi wa Bandari ukiendelea.


Hata hivyo amesisitiza Ushirikiano na kuwahimiza wakulima wa Kahawa kuongeza nguvu kuzalisha na kuahidi kuwa watakuja wataalam kutoka SUA ili wapime udongo na kufanya mabadiliko ili kilimo kiwe chenye tija zaidi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages