Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Cheng Mingjian, wakijadiliana masuala mbalimbali yanayohusu kuimarisha na kudumisha urafiki na udugu, kati ya CCM, Serikali zake mbili na Serikali ya China, kwa upande mwingine.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Ijumaa, Juni 9, 2023, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi, Lumumba, jijini Dar Es Salaam, pande zote hizo mbili zilihakikishiana umuhimu wa kuendelea kuboresha na kudumisha urafiki na udugu huo wa muda mrefu, na kuuboresha kadri ya mahitaji ya muda, mazingira na nyakati za sasa, kwa maslahi ya wananchi wa pande zote mbili na maendeleo ya nchi za Tanzania na China.
Katibu Mkuu Ndugu Chongolo na Mhe. Balozi Mingjian, pia walizungumzia umuhimu wa pande hizo mbili kuendelea kutengeneza fursa za kubadilishana uzoefu katika masuala ya elimu – mafunzo, biashara, uwekezaji, uongozi, utawala, mapambano dhidi ya rushwa na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kwa kuweka mbele ushirikiano unaoweka mbele unufaikaji ulio katika misingi ya usawa na maendeleo ya watu wa pande zote mbili.
“Nchi za Tanzania, kama ilivyo vyama vinavyoongoza katika nchi hizi, kwa maana ya Chama Cha Mapinduzi na Chama Cha Kikomunisti cha Watu wa China (CPC), vivyo hivyo kwa Serikali zinazoundwa na vyama hivi, Serikali ya China na Serikali za CCM, ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni pande mbili ambazo zimekuwa na urafiki ambao sasa ni udugu wa muda mrefu, katika shida na raha.
“Na kwa namna hadhi ya ushirikiano wa pande hizi ilivyoongezeka na kupanda, hasa kufuatia ziara ya kihistoria ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini China, baada ya mwaliko wa Mhe. Xi Jinping, Rais wa China, ni muhimu kuendelea kukutana na kuzungumza ili kuboresha, kuimarisha na kudumisha ushirikiano wetu katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kupeaana fursa za mafunzo ya uongozi kwenye mambo mbalimbali, kuangalia uhusiano wa kibiashara na hata watu wa pande zote mbili,” amesema Katibu Mkuu Chongolo.
Kwa upande wake, Balozi wa China, Mhe. Mingjian alimhakikishia Ndugu Chongolo kuwa Nchi na Serikali ya China anayoiwakilisha hapa nchini, inauchukulia urafiki na udugu wa pande hizo mbili kuwa wa kipekee na iko tayari kuendelea kuuenzi na kuudumisha kwa ajili ya manufaa ya watu wa Tanzania na China.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇