LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 14, 2023

MWENYEKITI CCM WILAYA KILOMBERO APIGA MARUFUKU UTOZAJI WA TSH1000 KWA GUNIA KUTOKA SHAMBA KUJA NYUMBANI

Na Dismas LYASSA

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kilombero, ndugu Mohamed Msuya ameagiza kusitishwa mara moja agizo la Halmashauri ya Wilaya Mlimba linalowataka wananchi kulipia Tsh1000 kwa gunia la mazao hata kama linatolewa shambani kuletwa nyumbani kwa mkulima.

 Wiki iliyopita ofisi ya Mkurugenzi wa Mlimba ilitoa maagizo ikiwataka maofisa watendaji katika Halmashauri ya Wilaya Mlimba kuhakikisha wanafuatilia mapato ikiwamo kuhakikisha kila gunia la mazao linatozwa Tsh1000 hata kama linatolewa shambani kuletwa nyumbani kwa mkulima kwa matumizi ya chakula.

 Agizo hilo lilileta malalamiko mengi kwa wananchi, jambo lililosababisha Mwenyekiti huyo wa CCM kuitisha kikao cha dharura cha chama na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba akiwamo Mkurugenzi na madiwani wake waliopitisha tuzo hiyo.

 Katika mkutano huo madiwani walisema suala hilo lilipitishwa kwenye kikao chao cha Oktoba mwaka jana na kwamba walikubaliana baadae wangewasilisha mpango huo kwenye chama, kitu ambacho hawakufanya, badala yake wamelipeleka moja kwa moja kwa wananchi kwa utekelezaji bila hata kuwa na mikutano na wananchi.

“Mpango huo hauna baraka kutoka kwa chama wala wananchi, nazuia usiendelee,” alisema Msuya, huku baadhi ya madiwani wakishindwa kufafanua hasa namna gani walipitisha mpango kama huo.

Wananchi wamekipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kusimamia Serikali na kujali wananchi, huku baadhi yao wakiomba ofisi ya waziri mkuu kuangalia upya ofisi ya Mkurugenzi inavyofanya shughuli zake na namna inavyoshirikiana na baadhi ya madiwani katika kuendesha mambo yake bila ridhaa ya chama tawala wala wananchi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages