RC SERUKAMBA AHITAJI EKARI MILIONI MOJA SINGIDA
Na HEMEDI MUNGA
MKOA wa Singida umejipanga kuongeza ukubwa wa mashamba yatakayotumika kulima zao la alizeti kutoka ekari 631,931 hadi kufika ekari milioni moja (1,000,000) kwa kutumia wakulima wadogo, wakati, wakubwa na vikundi kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mafuta ya alizeti nchini.
Matarajio hayo, ameyasema Mkuu wa Mkoa huo, Peter Serukamba wakati akizungumza katika Mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Halmashauri ya Ikungi leo mkoani hapa.
RC Serukamba anasema zao la alizeti ni moja kati ya vitambulisho vya mkoa huo, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anaongeza eneo la kilimo cha zao hilo.
Aidha, anatoa njia ya kuhakikisha matarajio hayo yanafanikiwa kwa kuwashirikisha viongozi wa kata, vijiji na maofisa kilimo kuhamasisha wakulima kuongeza maeneo ya kulima zao hilo.
Hata hivyo, Serukamba anasema jiji la Dodoma linakuwa kwa kasi, hivyo ni fusra kwa mkoa wa Singida uliojirani na jiji hilo kuzalisha mazao mengi ikiwemo mafuta.
Halikadhalika, anaeleza kufunguka kwa barabara ya Singida Mbeya, Singida Arusha mpaka Tanga kunaongeza soko na ukuaji mkubwa wa mkoa huo.
Pia, anasema mkoa huo unatarajia kuwa na wakulima wa aina tatu ifikapo msimu wa kilimo 2024.
Anafafanua kuwa kutakuwa na wakulima wadogo, wakulima wakati na wakulima wakubwa wa zao la alizeti, hivyo kutosheleza mahitaji ya soko ambalo hadi hivi sasa bado linahitajika.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa anampongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ikungi Justuce Kijazi kwa sababu alitenga eneo kubwa takribani ekari elfu 50 kwa lengo la kutekeleza mradi wa kilimo cha pamoja ambao unatekelezwa na Wizara ya Kilimo kwa vijana ‘’build better Tomorrow’’.
Katika kuhakikisha mpango huo unakamilika, utaratibu wa uchambuzi wa kina utaanza kwa lengo la kujenga miundombinu ya umwagiliaji.
Aidha, Serukamba anawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani hapo kutumia fedha walizopewa kwa tija kabla ya kufika Juni 30, mwaka huu kwa lengo la kuhakikisha haibaki fedha yoyote.
Mkutano wa ALAT ulihudhuriwa na Wenyeviti wa Halmashauri sita, madiwani wawili kutoka katika kila Halmashauri na Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizungumza katika Mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Halmashauri ya Ikungi leo mkoani hapa. (Picha kwa hisani ya ofisi ya mkuu wa mkoa)
Wenyeviti wa Halmashauri sita, madiwani wawili kutoka katika kila Halmashauri na Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa wa Singida wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Peter Serukamba leo katika Mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Halmashauri ya Ikungi leo mkoani hapo. (Picha kwa hisani ya ofisi ya mkuu wa mkoa)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇