Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Rais Samia Suluhu Hassan atakutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye anawasili Jijini Dar es Salaam, leo Alhamis Aprili 27, 2023, kutafanya ziara ya kikazi ya siku mbili hapa Nchini Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na Serikali imesema, jana kwamba Rais Kagame atawasili na Ujumbe wake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) leo na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Stergomena Tax (Mb.).
"Akiwa nchini, Mheshimiwa Rais Kagame atakutana na kufanya mazungumzo na Mwenyeji wake, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Ikulu Jijini Dar es Salaam, leo Aprili 27, 2023 na baada ya mazungumzo viongozi hao watazungumza na Waandishi wa Habari kuelezea yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo hayo.
Tanzania na Rwanda zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliodumu kwa muda mrefu ambapo nchi hizi mbili zimekuwa zikishirikiana kwenye sekta mbalimbali za kimkakati ikiwemo biashara na uwekezaji, nishati, uchukuzi, elimu na utamaduni. Kufanyika kwa ziara hii ni ishara nzuri ya kuendelea kuimarika kwa uhusiano wa kidugu baina ya mataifa haya kwa maslahi mapana ya pande mbili", imsema taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇