Na Mwandishi Maalum, Dar es Salaam
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kupokea ndege ya kwanza ya mizigo Boeing 767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54 kwa mara moja ili kutatua changamoto za wafanyabiashara za usafirishaji wa mizigo duniani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa Mkutano wa mwaka 2022/23 wa wadau wa ATCL wa Usafirishaji Mizigo, Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu, amesema ujio wa ndege hiyo utawezesha wawekezaji na wafanyanyabiashara waliokuwa wanalazimika kupeleka mizigo yao nje ya nchi kupitia ndege za nchi jirani sasa hawata lazimika kufanya hivyo.
Kuhusu mahitaji ya soko duniani amesema kwa mujibu wa Ripoti ya Soko la Usafirishaji wa Mizigo ya 2023, ukubwa wa soko la mizigo limekua kutoka $191.01 bilioni mwaka 2022 kufikia $199.09 bilioni kwa mwaka 2023 kwa kiwango cha ukuaji wa kila mwaka (CAGR) cha 4.2% na ukubwa wa soko la usambazaji wa mizigo unatarajiwa kukua hadi $224.78 bilioni mwaka 2027 kwa kiwango cha CAGR ya 3.1%.
Mchechu amesema Tanzania inaingia rasmi kwenye historia ya biashara ya ndege ya mizigo ambayo sio tu kwa Afrika Mashariki bali kwa ngazi ya kimataifa. Haya yamepatikana ndani tu ya miaka miwili (2) tu ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Hakika, Serikali imewekeza ATCL sambamba na Mpango wake wa Maendeleo pamoja na Ilani yake ya Uchaguzi ili kuwezesha ukuaji wa uchumi, kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na biashara nchini ambapo biashara ya mizigo inakuwa kwa kasi duniani,” alisisitiza.
Mchechu amefafanua kwamba hapo awali mfanyabiashara alilazimika kupoteza siku kadhaa kwa ajili ya kupitishia mizigo yake kwenye nchi zingine ambapo kwa sasa itabaki historia tu. Ameeleza uwekezaji unaofanywa ATCL unalenga kukuza uchumi na unaendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na wafanyabiashara ili kukuza pato la ndani (GDP).
Mchechu amewataka ATCL kuendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wao ili kutatua changamoto zinazoweza kukwamisha ufanisi wa biashara hii pamoja na kusimamia maslahi mapana ya pande zote yaani wadau na Serikali.
Katika Mkutano huo uliohusisha wafanyabiasha pamoja na wawakilishi kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali, Msajili wa Hazina amesema Ofisi yake ina wajibu wa kusimamia mashirika yote nchini likiwemo ATCL ili kuhakikisha yanajiendesha kimkakati kupitia uwekezaji mkubwa unaofanya na Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi amesema Tanzania inatarajia kupokea ndege hiyo mapema mwezi Aprili, 2023 ambayo itatua changamoto ya usafirishaji mizigo hapa nchini. Awali ATCL ilikuwa ikitumia ndege abiria kusafirisha mizigo zilikuwa na uwezo wa kubeba tani chache sana kulinganisha na uhitaji wa soko la mizigo.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa Mpango wake Maalum wa Biashara, ATCL inajivunia kwa kutoa huduma za uhakika, salama na endelevu za ubora wa juu duniani kote. Kwa sasa ATCL ina ndege 12 na imefanikiwa kupanua mtandao wake hadi kufikia vituo 14 vya safari za kitaifa, 8 za kikanda na 2 za mabara. Vituo hivi, vinavyotoa huduma za usafirishaji wa abiria, mizigo na vifurushi.
Ameongeza kuwa kupitia Mkutano huo wa Wadau wa Mizigo, ATCL itakusanya maoni sahihi kutoka chanzo halisi yatakayowezesha kuondoa kero na urasimu kwenye biashara ya Mizigo.
“Yapo mambo yanayotakiwa kufanyiwa maboresho hasa yenye urasimu lakini yapo ambayo ni ufuataji wa sharia za kulinda usalama wa uendeshaji wa biashara hii. Katika kikao hiki wadau watajadili na kukubaliana masuala ya kufanyiwa kazi na kuweka malengo. Lakini pia tutaambizana ukweli kwa wafanyabiashara ambao hawafuati sharia ambazo kimsingi ni kwa faida ya pande zote mbili,” alisema.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇