Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi na watendaji wa Serikali kuzisoma na kuzielewa vyema taarifa za rushwa na za ukaguzi wa hesabu za Serikali ili ziwasaidie kujitathmini.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo mara baada ya kupokea taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika hafla iliyofanyika Ikulu.
Aidha, Rais Samia amesema taarifa hizo hizo zinasaidia kusimamia na kuimarisha utawala bora na kuhakikisha udhibiti na usimamizi wa rasilimali za Serikali unafanywa kikamilifu.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ameitaka Mamlaka ya Bandari kufanya kazi na sekta binafsi ili kuimarisha mifumo ya TEHAMA ya ukusanyaji fedha ambapo itasaidia kudhibiti upotevu mkubwa wa fedha unaotokea bandarini.
Rais Samia pia amegiza kufanyiwa tathmini kwa Mashirika ya Umma yaliyopata hasara na kuyafuta Mashirika ambayo hayana tija kwa taifa kwa kuwa Mashirika hayo yanatumia gharama kubwa lakini hayaleti faida kwa Serikali.
Katika ripoti ya CAG jumla ya Halmashauri 14 nchini zimepata hati zenye mashaka zikiwemo Halmashauri ya Jiji la Arusha, Babati, Bahi, Geita, Kilindi, Mbinga, Musoma, Nkasi, Nyasa, Simanjiro, Songwe, Sumbawanga Manispaa pamoja na Ushetu iliyopata hati mbaya.
Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2021/2022, kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere, Ikulu Jijini Dar es salaam, leo Machi 29, 2023.
Rais Samia Suluhu Hassan, akipokea Taarifa ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Kamishna wa Polisi Salum Hamduni, Ikulu Jijini Dar es Salaam, leo Machi 29, 2023.
Rais Samia Suluhu Hassan, akizungumza baada ya kupokea Taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa Fedha wa 2021/2022 na Taarifa ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ya mwaka huo wa fedha, Ikulu Jijini Dar es Salaam, leo Machi 29, 2023.
Baadhi ya Viongozi waliohudhuria hafla hiyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇