Na HEMEDI MUNGA
WAFANYABIASHARA nchini Tanzania waaswa kuwaonea
huruma waumini wa dini ya kiislamu wanaotarajia kuianza ibada adhimu ya swaumu
ya Mwezi wa Ramadahani badaa ya kuandama kwa mwezi au kukamilika kwa siku 30 za
mwezi wa Shabani mwaka huu.
Wametakiwa kutopandisha bei au ikiwezekana
kupunguza bei za bidhaa mbalimbali kwa lengo la kuwawekea wepesi waumini hao
watakapokuwa katika ibada hiyo.
Akizungumza na waumini wa dini hiyo waliofika
katika viwanja vya Msikiti Mkuu wa Bakwata jijini Dar es Salaam jana, Mufti Mkuu
wa Tanzania, Dk. Abubakar Zuber bin Ali anawaasa wafanyabiashara kuwa na huruma
hasa katika kipindi hichi cha ibada tukufu ya funga.
Aidha, anasema haitakiwi kwa mtu yoyote hata kwa
wafanyabiashara kutengeneza ughali katika bidhaa anazoziuza sio tu katika Mwezi
huu Mtukufu hata katika miezi mingine.
‘’Nasaha na usia wangu kwa wafanyabishara wote
wawahurumie wafungaji wa Mwezi wa Ramadhani ambao hupata mashaka na tabu ya
kushinda njaa na kiu halafu bidhaa zikawa ghali, wafanye huruma ya kupunguza
bei ya bidhaa wanazoziuza kwa lengo la kuwafanyia wepesi wafungaji hao,’’ anaasa.
Mbali na hilo, anawataka waumini kujiandaa kuupokea
Mwezi wa Ramadhani kwa bashasha na kuamini kuwa ndio chuo cha kuwajenga kuwa
watu wema na wenye maadili katika jamii.
Akinukuu maneno ya Mtume Muhammad (S.A.w), Dk. Zuber
anasema kuwa mtu yeyote atakayefurahi kwa kuingia Mwezi wa Ramadhani inamuwajibikia pepo kutokana na furaha yake.
‘’Ni jambo la kwanza kwa Muislamu Mwezi wa
Ramadhani unapoingia ibakie kuwa kwake ni furaha na kufunga kwa kutekeleza
masharti, adabu, sunna na nguzo zake,’’ anausia.
Pia, anawataka kujifundisha kuwa na tabia njema kwa
sababu Mwezi huo hufundisha waumini kuwa na subra, uvumilivu, upendo,
kuwakaribisha watu, kuwa wakarimu na kutoa sadaka kwa lengo la kutafuta swawabu
zake.
‘’Ni kipindi ambacho muumini anatakiwa kijitosa katika
mambo ya kheri na ukarimu huku akiwa ni mtu mwema atakaye dumu hivyo baada ya
Mwezi wa Ramamdhani kuondoka,’’ anaongeza Mufti huyo.
Akiongea katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Da awa na
Tablighi Ofisi ya Mufti wa Tanzania, Arif Surya anasema Mufti Abubakar Zuber
bin Ali anazindua ugawaji wafutari kwa familia takribani 550.
Aidha, anaongeza kuwa katika familia hizo kila
mmoja amefanikiwa kupata mchele kilogramu 20, mafuta ya korie lita tano,
maharage kilogramu tano, unga wa sembe kilogramu tano na sukari kilo tatu.
‘’Inshaallwah zoezi hili, amefungua Mufti hapa
litaendelea katika mikoa mbalimbali ikiwemo Unguja na Pemba,’’ anasema Surya.
Halikadhalika, anasema wanampango wa kugawa tende
kwa sababu kula tende wakati wa kufungua
baada ya kufunga ni mwenendo wa Mtume Muhammad (S.A.W), hivyo watu wasile tende
kama chakula bali wale kwa kuzingatia sunna.
Kwa upande wake mmoja wa waumini waliopata futari
hiyo, Salimu Liyaga anasema anafurahi
kupata msaada huo na kumuomba Mungu awalipe badala wale wote waliotoa msaada
huo.
Anasema, anaamini kuwa futari hiyo itawasaidia yeye
na familia yake yenye watu saba katika kipindi hichi cha mwezi wa Ramadhani.
Naye Mkazi wa Kiwalani jijini hapa, Naima Khatibu anatoa
shukrani na pongezi kwa Mufti wa Tanzania kwa kuanzisha Ofisi hiyo amabyo
imefanikisha wao kupata msaada wa futari.
‘’Tunamuombea kheri Mufti wetu na viongozi wote
waliotoa futari hii kuwa na afya njema na wapate badala kwa lengo la kuendelea
kuwakumbuka wao,’’ anaomba Naima.
Ibada ya Swaumu ya Mwezi wa Ramadhani ni moja
katika nguzo tano za Uislamu ambapo muislamu aliokuwa na akili timamu,
aliobaleghe na mwenye afya njema anawajibika kufunga.
Ni ibada ambayo hufungwa siku 30 au 29 ya kila
mwaka inapofika Mwezi wa Ramadhani.
Mufti Mkuu wa Tanzania, Dk. Abubakar Zuber akiwasili katika viwanja vya Msikiti Mkuu wa Bakwata jijini Dar es Salaam leo katika zoezi la kugawa futari kwa waumini 550, kulia kwake ni Mkurugenzi wa Da awa na Tablighi Ofisi ya Mufti wa Tanzania, Arif Surya . (Picha na Hemedi Munga)
Mufti Mkuu wa Tanzania, Dk. Abubakar Zuber katikati akimgawia futari Naima Khatibu kushoto punde baada ya kuwagawia futari waumini 550 waliofika katika viwanja vya Msikiti Mkuu wa Bakwata jijini Dar es Salaam leo, kulia ni Mkurugenzi wa Da awa na Tablighi Ofisi ya Mufti wa Tanzania, Arif Surya . (Picha na Hemedi Munga)
Mufti Mkuu wa Tanzania, Dk. Abubakar Zuber katikati
akimgawia futari Salimu Liyaga kushoto punde baada ya kuwagawia futari waumini
550 waliofika katika viwanja vya Msikiti Mkuu wa Bakwata jijini Dar es Salaam
leo, kulia ni Mkurugenzi wa Da awa na Tablighi Ofisi ya Mufti wa Tanzania, Arif
Surya . (Picha na Hemedi Munga)
Baadhi ya waumini waliogaiwa futari toka kwa Mkurugenzi wa Da awa na Tablighi Ofisi ya Mufti wa Tanzania, Arif Surya punde baada ya ugawaji wa futari hiyo kwa familia 550 katika viwanja vya Msikiti Mkuu wa Bakwata jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Hemedi Munga)
Mkurugenzi wa Da awa na Tablighi Ofisi ya Mufti wa Tanzania, Arif Surya akiwaasa waumini hao kuupokea Mwezi wa Ramadhani na kufunga kikamilifu kwa kuwa wamepatiwa futari punde baada ya ugawaji wa futari hiyo kwa familia 550 katika viwanja vya Msikiti Mkuu wa Bakwata jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Hemedi Munga)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇