Sehemu ya wamachinga.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, ametoa onyo kwa mgambo wa Jiji wanaowanyanyasa wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga kwa kuwamwagia bidhaa zao kwani hayo sio maagizo ya Serikali na kufanya hivyo ni kukiuka haki za wafanyabiashara hao.
Hayo yamesemwa wakati wa uzinduzi wa kituo cha daladala kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria kwenye soko kuu la machinga complex lililopo eneo la Bahi Road Jijini Dodoma.
Kituo hiki kinachopokea daladala kutoka pande zote za Jiji la Dodoma, kimezinduliwa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alilotoa wakati alipowatembelea wafanyabiashara hao na kuzungumza nao hivyo walipata fursa ya kufikisha ombi hilo na huu ni utekelezaji wake.
“Kinachofanyika hapa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali. Sitoi kibali kwa mgambo kutumia nguvu kwa wafanya biashara kwani haya sio maelekezo ya Serikali.
Tusipige watu wala kunyang’anya bidhaa zao ingawa bado sheria zetu zinatutaka tusifanye biashara kwenye maeneo yasiyoruhusiwa. Lililotuleta hapa ni uzinduzi wa Kituo cha Daladala, tunakwenda kushuhudia daladala zote zikianzia hapa.
LATRA na Polisi endeleeni kushirikiana kupanga kila daladala inayopaswa kuingia hapa” Amesema Mhe. Senyamule
Kadhalika, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe ametoa pongezi kwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwani Dodoma imepata fursa ya kutafsiri maono yake kwa hafla hii.
“Dodoma tumepata fursa ya kutafsiri maono ya Mhe. Rais kwa tukio hili. Namshukuru kwa kuona umuhimu wa Serikali kuwatambua wafanyabiashara hawa. Ninyi ni kiungo maalumu katika kuhudumia wananchi wa Dodoma, viongozi wa daladala wametupa ishara kwamba wanajitambua nah ii ndio Dodoma tunayoitaka, yenye utaratibu” Amepongeza Dkt. Mwamfupe
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bw. Joseph Mafuru, amesema kuwa wameyatekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu ikiwemo hili la kuweka kituo cha daladala katika soko hili, kuweka taa za barabarani katika eneo hili kwani hapa wafanyabiashara wanafanya shughuli zao mpaka majira ya usiku pia kwa sasa wanatekeleza agizo kuwapatia mikopo wafanyabiashara hao.
Pia Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti na Usafirishaji wa Nchi kavu Tanzania (LATRA) Bw. Ezekiel Emmanuel, amesema kuwa wameanza kuhamisha daladala zote kutoka kituo cha sabasaba kwa kushirikiana na wadau wote wanaohusika na usafirishaji na takribani daladala 850 yanatarajiwa kutoa huduma kwenye kituo hiki kipya na wao kama mamlaka husika wanasimamia uratibu huo.
Ameongeza kuwa LATRA wanaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Jiji kuboresha huduma hii kwa kutoa matangazo kwa njia ya magari kupita mitaani yakiwa na vipaza sauti kuwaelekeza wananchi juu ya matumizi sahihi ya njia hizi zinazoingia na kutoka sokoni hapo.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇