LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 16, 2023

WRRB YATAJA MAFANIKIO LUKUKI TANGU KUANZISHWA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI


Mkurugenzi Mtendaji wa BODI ya usimamizi wa Stakabadhi za ghala (WRRB) Asangye Bangu akizungumza ,wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za bodi hiyo mbele ya waandishi wa habari leo Februari 15,2023,jijini Dodoma.


Na Richard Mwaikenda, Dodoma

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imetaja mafanikio lukuki tangu kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghalani ikiwemo ongezeko la bei za mazao, mapato ya mkulima na mapato ya 
Serikali kwa wastani wa asilimia 200% kutokana na urasimishaji, ongezeko la uzalishaji wa mazao kwa wastani wa asilimia 12% kwa mwaka,kichecheo cha ubora wa mazao yanayofikishwa sokoni,


Mafanikio mengine ni upatikanaji wa takwimu sahihi za mazao yanayopita kwenye Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, ongezeko la mapato ya uhakika kwa Serikali Kuu na Serikali Mitaa na kukuza huduma za fedha vijijini,kufanikisha uanzishaji wa Soko la Bidhaa Tanzania.

Mafanikio hayo yametajwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Asangye Bangu alipokuwa akielezea utekelezaji wa majukumu ya Bodi katika mkutano na vyombo vya habari Februari 15, 2023 kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma.

Aidha, Mkurugenzi huyo amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Mfumo 2007/08 hadi 2020/21 ukuaji wa uzalishaji umekuwa ukiongezeka kwa wastani wa 12% kwa mwaka ikilinganishwa na ukuaji wa 2% kwa mwaka kabla ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

"Kwa mfano katika zao la Korosho mara baada ya kuanzishwa kwa Mfumo palikuwa na ongezeko la asilimia 164% la bei kutoka Ths 350.00 msimu wa 2006/07 hadi kufikia Tsh 925.00 msimu wa 2007/08 mwaka wa kuanza wa Mfumo; katika miaka minane tokea kuanzishwa kwa Mfumo 2007/08 hadi 2014/15 wastani wa ongezeko la bei kwa mwaka ulikuwa 25% kulinganisha na ongezeko la bei miaka minane kabla ya kuanzishwa kwa Mfumo la 12% kwa mwaka kaunzia mwaka 1998/99 hadi 2006/07," amebainisha Bangu

Mkurugenzi huyo amesema kuwa ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknojia Bodi imekuwa ikishirikiana kwa karibu na kuhamasisha bodi ya TEHAMA kukamilisha mifumo mipya na kuhamishia huduma za Bodi hiyo kwenda kidijitali.

Aidha, Bodi imeendalea juhudi za kuboresha Mfumo uliokuwepo wa kizamani wa Usimamizi wa ghala, ambapo kushirikiana na Bodi ya TEHAMA inakuja na Mfumo mpya wenye kuweza kurahisisha kazi za
maandalizi ya taarifa, utoaji stakabadhi na udhibiti wa matukio ghalani hivyo kupunguza muda wa michakato na kuongeza ufanisi na usalama wa mzigo.

"Majaribio ya Mfumo wa Maombi ya Leseni Mtandaoni
yamefanyika na mapendekezo ya maboresho yamepelekwa kwa programmers kwa ajili ya kufanyiwa kazi,"amesema Bangu

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) ni taasisi chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara iliyoundwa kwa Sheria Namba 10 ya 2005 na Marekebisho Kifungu 4 Sura 339 R.E. 2016 iliyopewa majukumu chini ya Kifungu 5 (a-j) ikiwemo kutoa leseni kwa waendesha ghala, meneja dhamana na wagakuzi wa ghala;

 kuchapa and kuidhinisha vitabu vya Stakabadhi za Ghala, kusajili na kuingiza taarifa za wadau muhimu wa mfumo, kuwakilisha nchi katika masuala ya taifa na kimataifa yahusuyo Mfumo wa Stakabadhi za Ghala pamoja na majukumu mengine kama taasisi itakavyoelekezwa na Mhe. Waziri wa Viwanda na Biashara.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages