Na Lydia Lugakila, Kagera
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert John Chalamila amemuagiza Mkuu mpya wa Wilaya ya Bukoba mhe, Erasto Yohana Siima kuhakikisha anatatua mabishano yaliyopo Manispaa ya Bukoba ya Mkoani humo ya kulipa au kutolipa leseni za biashara huku akitaka Msako uanze mara moja ili waliokaidi wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert John Chalamila ametoa kauli hiyo baada ya kuongoza viapo kwa Wakuu Wapya Watatu Miongoni mwa Wanne walioteuliwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Januari 30, 2023 katika ukumbi wa Mkoa huo.
Chalamila amemtaka Mkuu wa Wilaya Bukoba kuanza na Majukumu yakiwemo kuhakikisha anaodoa mabishano yaliyopo ya kulipa au kutolipa leseni za biashara kwa wafanyabiashara kutokana na kukiukwa kwa ahadi ya makubaliano ya kuwa leseni hizo ziwe zimelipwa hadi kufikia Desemba 30, 2022.
"Nakuagiza anzeni Msako kwa mtu yeyote ambaye hajalipa leseni za biashara hapa wasinitanie nipo hapa kwa mujibu wa sheria najua upole ukizidi ni Ujinga" alisema Rc Chalamila.
Sambamba na hayo pia amemtaka Mkuu huyo wa Wilaya ya Bukoba kuhakikisha Watoto wanaotakiwa kwenda shule kidato cha kwanza wanakwenda Shule, na wale walioachishwa shule na kuolewa wafuatiliwe na wahusika wakiwemo wazazi wachukuliwe hatua
Ameongeza pia kumtaka Mkuu huyo wa Wilaya Kushughulika na kuona namna ya kuongeza pato la manispaa, kurudisha haraka mahusiano kati ya Chama Tawala na Serikali baada ya kuonekana mahusiano hayo yameyumba.
Aidha amemtaka kusimamia miradi ya naendeleo kwa ufanisi, kutatua migogoro katika eneo lake na kutambua wajibu na mipaka yake.
Aidha Walioapishwa ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Yohana Siima, Mkuu wa Wilaya Karagwe Mhe. Julius Kalanga Laiser na Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Abeli Mwendawile Nyamahanga huku Mkuu wa Wilaya mteule wa Kyerwa Bwn. Maganga kutokuwepo ukumbini wakati wa tukio hilo.
Wengine waliohudhuria Hafla hiyo ya kuapishwa ni pamoja na Mkuu wa Wilaya mpya wa Biharamulo Mhe. ACP Advera John Bulimba, Mkuu wa Wilaya Missenyi Kanali Willson Christian Sakulo, Mkuu wa Wilaya ya Ngara Kanali Mathias Kahabi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya, Wakurugenzi, Makatibu Tawala wa Wilaya, Viongozi wa Dini na Viongozi w Taasisi mashirika na Kampuni.
Hata hivyo mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Mkuu huyo wa Wilaya kwa kushirikiana na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani humo kuhakikisha anasambaratisha vijiwe vya Kahawa manispaa ya Bukoba pamoja na kutokomeza ulevi unaofanyika Asubuhi muda wa kazi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇