LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 20, 2023

PROF MBARAWA ATOA TAADHARI WIZI WA VIFAA VYA WAKANDARASI KAGERA


Lydia Lugakila, Ngara


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amewatahadharisha wananchi wa wilaya za Ngara na Biharamlo mkoani Kagera watakaopata fursa ya kufanya kazi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya lami Lusahunga hadi Rusumo yenye km 92 itakayogharimu shilingi bilioni 153.5  kuwa waadilifu na kutofanya wizi wa saruji na vifaa mbali mbali.


Barabara hiyo ambayo ilikuwa imejengwa kwa kiwango cha lami ilikuwa imeishaharibika na kujaa mashimo kutokana na kutumiwa na magari makubwa ya mizigo yanayotoka nchi za Rwanda, Burundi, DRC Congo na kwenda bandari ya Dar es salaam na ambapo imekuwa ikisababisha ajali za mara kwa mara na hivyo kutengenezwa kwake itakuwa faraja kwa watumiaji wa barabara hiyo.


Prof. Mbarawa aliyasema hayo jana wakati akiwa mgeni rasmi katika hafla ya utiaji saini mkataba wa barabara ya rami kati ya serikali na mkandarasi wa ujenzi  kutoka China Civil Engeneering Constraction Coperation (CCECC) yenye urefu wa km 92 kutoka Lusahunga wilaya ya Biharamlo hadi Rusumo wilaya ya Ngara ambayo itagharimu sh 153 bilioni.


Amesema, amekubali ombi la mbunge wa jimbo la Ngara kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndaisaba Ruhoro la kuwapatia kazi za mwanzo katika mradi huo wananchi wa Ngara lakini akatoa angalizo kuwa wawe waadilifu na akatolea mfano mradi wa Reli wa Mwanza ambao wafanyakazi walikuwa wakiimba vifaa mbalimbali na hivyo kuihujumu serikali.


“Mbunge ameomba kazi itakapoanza wananchi wa hapa wapate kazi hizi naomba niwahakikishie ndugu zangu kwamba tutamwelekeza mkandarasi kwamba kazi za mwanzo ambazo zinaweza kufanywa na wananchi wa hapa wapewe wao, Mbunge tunakuhakikishia kuwa hilo tutalifanya ili wananchi waweze kupata ajira na wao waweze kupata riziki kwenye mradi huu, lakini wale watakaopata fursa ya kufanya kazi kwenye mradi huu naomba muwe waadilifu tumeshuhudia kule Mwanza kwenye mradi wa reli kuna watu wanaiba saruji, mafuta na mambo mengine ya hovyo ninaamini watu wa Ngara na Kagera kwa ujumla ni wastaarabu hamtafanya mambo ya hovyo” Alisema Prof Mbarawa.


Aidha ameutaka uongozi wa mkoa na wilaya kutoa ushirikiano kwa mkandarasi ili kazi hiyo imalizike mapema na barabara iweze kuendelea kutumika.


Kwa upande wake mtendaji mkuu wa wakala wa barabara nchini (Tanroads) Logatus Mativila amesema serikali iliona umuhimu wa kutoa fedha za  kujenga barabara hiyo kutokana na kutumia fedha nyingi kwenye kukarabati ambapo katika kipindi cha miaka mitatu zilitumika sh 33 bilioni.


Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutafungua fursa mpya za kibiashara na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali na hivyo kukuza uchumi kwa wananchi wa maeneo hayo na Tanzania kwa ujumla na itachochea shughuli za kiuchumi kama vile usafirishaji wa mazao ya chakula na biashara, mazao ya misitu, uvuvi na katika shughuli za utalii katika mbuga za Taifa za Burigi na Rubondo mikoa ya Kagera na Geita, muda wa utekelezaji wake ni miezi 24.


Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila amewataka wananchi mkoani humo kuona umuhimu wa kuzalisha kiasi cha kutosha cha chakula kwa kuwa fursa za usafirishaji zitakuwepo na wao wataweza kuongeza uchumi  binafsi na wa Taifa kwa ujumla kwa  kuuza nchi jirani za Rwanda, Burundi na DRC Congo.


Justina Ndailagije mkazi wa kijiji cha Benako  amesema ujenzi wa barabara hiyo utamsaidia kuongeza kipato chake katika biashara ya mama ntilie anayofanya katika kituo cha magari makubwa ya mizigo yayayokwenda nje ya nchi kwani madreva wa magari hayo watakuwa yanasafirisha mizigo kwa wingi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages