LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 24, 2023

MWANGWI WA ZIARA YA MWENEZI WA CCM SOPHIA MJEMA TANGA, ASEMA UJENZI WA CCM ISIWE IYENAIYENA TU, AIACHIA MAKOVU CHADEMA

Na Bashir Nkoromo, aliyekuwa Tanga
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi Sophia Mjema, Jumatatu ya Februari 20, mwaka huu alihitimisha ziara yake ya Siku tatu katika mkoa wa Tanga baada ya kuianza Jumamosi Februari 18.

Katika ziara hiyo ambayo Mjema aliambatana na Katibu wa NEC, Idara ya Oganaizesheni Issa Ussi (Gavu) na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Hamoud Abuu Jumaa, japo ilikuwa ya siku chache lakini ilionyesha kuwa yenye mafanikio ya kutosha katika kukagua Utekelezaji wa Ilani ya CCM na kukijenga Chama chenyewe.

Ni ziara ambayo ilipata hadhi ya kusisimua kwa kuwa viongozi wa Chama, Serikali na Wabunge baadhi mkoani Tanga nao walishiriki ziara hiyo bega kwa bega wakiongozwa na Mkuu wa mkoa huo Omary Mgumba.

Baada ya kupokea eneo la Mkata, Mjema na msafara wake walienda Handeni ambako moja kwa moja alianza kupiga kazi kwa kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM na pia kuzungumza na Wanachama wa CCM na Wananchi kwa jumla waliofurika katika mikutano ya hadhara.

Hapo akakagua Hospitali ya Mkata ambayo ujenzi wake unafanyika ikiwa ni katika Utekelezaji wa Ilani ya CCM, baada ya kuridhika na hatua iliyofikiwa katika ujenzi Mjema akaagiza Hopsitali hiyo ianze kutoa huduma ifikapo mwisho wa mwezi ujao wa Machi.

Sanjari na agizo hilo alimuagiza Mganga Mkuu wa Wialaya ya Handeni atume maombi  kwenda Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto ili Hospitali hiyo iweze kupatiwa Watumishi muhimu wanaohitajika wakiwemo wataalamu wa mifupa, ICU.
 
Kuhusu Hospitali hiyo Mjema hakuishia hapo, alienda mbali zaidi kwa kuwataka TANROADS  kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa Barabara ya kuingilia hospitali kutoka barabara kuu ili kupunguza hatari ya usalama wa wananchi.

Mchakamchaka wa ziara yake Handeni ulimfikisha Mabanda ambako alifanya mkutano wa Shina, hapo katika eneo la kuimarisha uhai wa Chama na Utekelezaji wa Ilani ya CCM akawataka Viongozi  wa CCM na wale wa Serikali ngazi zote kufanya vikao na Wananchi ili kuwaeleza yanayofanywa na Serikali.

Aliwaagiza katika kufanya mikutano hiyo na wananchi viongozi hao wahakikishe wanakuwa na taarifa sahihi za miradi ikiwemo mapato na matumizi na kuzisoma kwenye mikutano hiyo.

Katika ziara hiyo Mjema alibaini pia kuwepo kwa changamoto ya migogoro ya ardhi na kubaini kuwa sehemu kubwa ya migogoro hiyo inasababishwa na viongozi wa ngazi za mwanzo ambao wamekuwa wakijitwalia madaraka ya kuwa wauzaji viwanja na mashamba.

Kufuatia kubaini hilo Mjema aliwaonya Viongozi hasa wa Serikali za mitaa kuacha kujiingiza katika mambo ya uuzaji mashamba na viwanja kwa kuwa hiyo siyo kazi yao na pia kufanya hivyo ni kuwa chanzo cha migogoro ya Ardhi.
 
Mjema alimwagiza Mkuu wa mkoa wa Tanga Omary Mgumba na wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia kwa karibu suala la ardhi ili kukomesha migogoro ikiwemo baina ya Wakulima na Wafugaji.

Aidha Mwenezi Mjema aliangazia changamoto ya Barabara ya Handeni –Turiani ambayo alisema, ni lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kuondoa changamoto zilizoko kwenye barabara hiyo.

Kuhusu mradi wa mashamba ya kilimo, Mjema aliwataka vijana kuuchangamkia kwa kuwa lengo la mradi huo ni kukabiliana na changamoto ukosefu wa ajira kwa vijana, lakini akasisitiza kwamba ili vijana waweze kushiriki kikamilifu kwenye mradi huo lazima viongozi wawahamasishe na kuwaelekeza namna ya kuyapata mashamba hayo.

"Katika kufanikisha mradi huu Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Sh. bilioni 900, lengo likiwa ni kuwezesha wananchi hasa vijana waweze kutengewa mashamba ambayo pamoja na kuyapata watakuwa na viatilifu, mbolea na mfumo wa umwagiliaji.

Sasa changamoto ipo kwa vijana hawa katika namna ya kuomba mashamba haya, wengine hawataweza kuingia mitandaoni kuyaomba, hivyo naagiza Mkuu wa mkoa na Wakuu wa Wilaya mjipange ili kuratibu vema namna ambayo hawa vijana watakuwa wanasaidiwa kujaza maombi", akasema Mjema.

Akiwa bado yupo Handeni, siku hiyo hiyo, Mjema alifika Kata ya Msomera na kukagua Mradi wa Mnada wa Mifugo, hapo akasisitiza kuwa ili mradi huo uwe chanya unatakiwa uwe 'One Stop Center' kwa maana ya kila huduma iwepo kama, mifugo yenyewe, jokofu, vifungashio na ikiwezekana kiwepo hata kiwanda kidogo cha kusindika nyama.
 
Mjema, Serikali  itatoa mikopo kwa wafugaji kwa minajri ya kufuga kisasa zaaidi ili kuinenepesha iuzwe kwa thamani kubwa zaidi.

Kuhusu suala la mikopo, Mjema aliwaagiza Viongozi wahakikishe wanatoa elimu ya mikopo ya asilimia 10 kwa Wanawake na Vijana pamoja na mifuko mingine ili Wananchi wa Msomera waweze kupata mikopo kwa kuwa mikopo hiyo imewekwa na Serikali kwa ajili ya kusaidia wananchi kuinuka kiuchumi.

LUSHOTO
Siku ya pili ya ziara yake, Mjema alikuwa Wilaya ya Lushoto ambako asubuhi alifika kukagua maendeleo ya Ujenzzi wa Jengo la Huduma ya Mama na Mtoto iliyopo Lushoto mjini, ambapo baada ya kukagua maeneo mbalimbali na kuelezwa changamoto kadhaa nako alitoa maelekezo.

Hapo alimwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya ya Dk. Lushoto Godftey Andrew kutuma maombi ya watumishi muhimu wanaohitajika na kwamba yeye pia ameshawasiliana na Waziri Ummy Mwalimu na waziri huyo ameahidi kulifanyia kazi.

"Jengo hili la Huduma za Mama na Mtoto hata Katibu wetu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo alishafika kulikagua na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake, hivi sasa linapendeza na lipo katika hali ya kuweza kutoa huduma, hivyo DMO na viongozi wengine hakikisheni sasa linaanza kutoa huduma mapema iwezekanavyo", alisema Mjema.
 
Hapo pia Mjema alielezwa changamoto kuhusu kinamama wa Lushoto kukosa mikopo kwa kipindi kirefu hivyo akaagiza viongozi wa Serikali na Watendaji hasa Afisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanaweka mfumo mzuri wa kutoa elimu juu ya mikopo ya Halmashauri ili  wananchi wasaidiwe na wapewe mikopo hiyo.
 
Kuhusu changamoto za maji na barabara Lushoto, Mjema alitoa maelekezo kwa watu wa maji na TARURA  kuleta mpango wao wa kuondoa changamoto za maji na barabara wilayani humo ikiwa ni mojawapo ya kutekeleza Ilani ya CCM.
 
Akijibu ombi la Mkuu wa mkoa Omary Mgumba aliyemba Mwenyekiti wa CCM Rais Samia kutembelea Wilaya hiyo, Mjema alisema ombi hilo atalifikisha na bila shaka Rais atalipokea kwa mikono miwili maana anawapenda na kuwathamnini Wana Lushoto.

"Mheshimiwa Katibu Mwenezi, tangu pale ulipokuwa Mkuu wa Wilaya hii (zaidi ya miaka kumi iliyopita ), Lushoto haijawahi kutembelewa na Rais, sasa wana Lushoto tunayo mawili, sisi tumfuate Rais huko Ikulu Dodoma au Dar es Salaam, au aje yeye, maana tunamhitaji sana kumuona na kuzungumza naye", akasema Mgumba.

Aidha Mjema aliaelekeza kutafutiwa ufumbuzi wa mapema kuhusu ombi walilotoa Wananchi wa Lushoto
kupatiwa Ofisi ya CCM ya wilaya, kupatiwa gari kwa ajili ya usafiri kulingana na jiografia ya wilaya hiyo na
Upungufu wa watumishi wa kila kada katika Halamshauri ya Lushoto.

KIWANDA CHA CHAI MPONDE
Baada ya kukagua jengo hilo la Huduma za Mama na Mtoto Mjema alikatisha milima na mabonde ya Lushoto hadi akafika kukagua kiwanda cha kushindika majani ya Chai cha Mponde ambacho Serikali imekiweka chini ya usimamizi wa Mfuko wa PSSSF na WCF kwa muda.

Alieleza kuridhishwa na maendeleo ya Kiwanda hcho, kisha akasema Serikali itatafakari kuona namna ya  kuwapa hisa Wakulima wa chai ili kuwa sehemu ya kiwanda hicho, na pia itaweka bei elekezi ya zao la chai , pamoja na utaratibu wa ruzuku kwa wakulima wa zao hilo kama Mbunge wa Bumbuli Januari Makamba alivyoomba.

MKUTANO WA HADHARA TANGA MJINI
Baada ya mchakamchaka wa siku hiyo ambayo ilikuwa ya pili katika ziara yake, hatimaye Mjema aliingia Tanga mjini na kufanya mkutano mkubwa wa hadhara ambao ulihudhuriwa na maelfu ya Wananchi.

Hakika mkutano huo ulikuwa wa kipekee sana kwa kuwa ndiyo uliodhhirisha kuwa CCM bado ni chama pendwa katika mkoa wa Tanga.

Kabla ya kuzungumza, baada ya kukaribishwa jukwaani na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajab Abdallah, Mjema alimkaribisha Waziri wa Nishati Januari Makamba ambaye alipanda jukwaani na kueleza Serikali ilivyojipanga kutatua changamoto ya Umeme na Maji Tanga mjini.

Makamba alisema, kukatika mara kwa mara umeme Tanga mjini kunatokana na Shirika la Umeme (TANESCO) kuwa katika kazi ya kubadilisha mfumo wa ugavi wa umeme hasa nguzo ambazo zimechakaa kutokana na kuwepo kwa miaka mingi.

Baada ya kurejea jukwaani Mjema lianza kwa kuwafunda wanachama wa CCM namna bora ya kukiimarisha Chama. "Ndu zangu wana CCM na Wapenzi wa CCM, siasa za sasa ni za kidigitali, kwa hiyo lazima mjue kwamba sasa hatuwezi kuijenga CCM kwa iyena iyena tu. Hapana, lazima kila mwana CCM kwa nafasi yake ajue wajibu wake asibweteke na kudhani chama kitajijenga chenyewe.

Lazima kila mmoja awe mstari wa mbele kueleza kazi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Chama Cha Mapinduzi katika utekelezaji wa Ilani, na kwa kweli Rais Samia amefanya makubwa hivyo mazuri ya kusema yapo katika ngazo zote tangu vitongoji, Kata, Wilaya na mikoa", akasisitiza Mjema.

Kwa upande mwingine, ziara ya Mjema, ambayo aliikamilisha na kufanya majumuisho kesho yake Jumatatu, iliacha imeweka pigo kwa chama cha CHADEMa baada ya wanachama wake zaidi ya 30 kutangaza kukihama na kujiunga na CCM.

Wanachama hao waliokuwa wa Chadema walitangaza kuhamia CCM katika Mkutano huo uliofanyika Tanga mjini na kupokewa na Mwenezi Mjema. "karibuni sana, hapa CCM ndipo ambako kuna siasa za kistaarab na za Kidemokrasia zaidi, huko mlikuwa mmepotea", akasema Mjema.

Wakizungumzia kuhamia kwao CCM, Wanachama hao walisema, kwa nyakati tofauti kwamba wameamua kuhama kutokana na kukerwa na tabia ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kuwa mroho wa madaraka na mkandamiza demokrasia badala ya kuikuza.

"Sisi baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais Samia hasa katika kulinda na kukuza demokrasia nchini na pia kujenga uchumi wa nchi, tumeamua tuje kumuunga mkono", akasema Kiongozi wao Grace Joseph Mtote.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi Sophia Mjema akihutubia Wana CCM na Wananchi kwa jumla waliohudhhuria kwa maelfu katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Tanga Mjini, Jumapili Februari 20, 2023.

Wana CCM na Wananchi kwa jumla wakimsikiliza Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi Sophia Mjema, katika mkutano huo.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi Sophia Mjema, akimsikiliza Mganga Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Dk.Godfrey Andew (kushoto) alipotembelea na kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Jengo la Huduma ya Mama na Mtoto iliyopo Mjini Lushoto. Pamoja naye ni Mjumbe wa NEC, Idara ya Oganaizesheni Issa  Ussi (Gavu) Mkuu wa mkoa wa Tanga Omary Mgumba na kulia ni Mjumbe wa NEC kupitia Jumuiya ya Wazazi Haoud Abuu Jumaa.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi Sophia Mjema, akizungumza na Viongozi wa CCM na watendaji wa Idara mbalimbali za Serikali mkoani Tanga katika kikao cha majumuisho ya ziara yake, Jmatatu Februari 20, 2023.
Baadhi ya Viongozi mbalimbali wa CCM wakimsikiliza Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi Sophia Mjema, katika Kikao hicho cha Majumuisho.
Baadhi
ya Viongozi na Watendaji mbalimbali wa Serikali wakimsikiliza Mwenezi Mjema katika Kikao hicho cha Majumuisho.
" Hapo vipi, bila shaka ziara yetu imekuwa ya mafanikio", bila shaka ndivyo alivyokuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi Sophia Mjema, akimwambia Katibu wa NEC Oganaizesheni Issa Ussi (Gavu) baada ya kuzungumza  katika Kikao cha Majumuisho.
Wajumbe wakisimama kumshangilia na kumuaga Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi Sophia Mjema, mwishoni mwa kikao hicho cha majumuisho.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi Sophia Mjema, akiwa katika picha ya kumbukumbu na badhi ya Viongozi baada ya kikao hicho cha majumuisho.
 

©Feb. 2023 CCM Blog/Bashir Nkoromo

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages