VIJIJI zaidi ya 40 vilivyoko Wilayani Igunga, Mkoani Tabora vinatarajiwa kunufaika na miradi ya maji iliyopangwa kutekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Akitoa taarifa ya mipango yake ya utekelezaji miradi ya maji vijijini jana Meneja wa RUWASA Wilayani hapa Mhandisi Marwa Sebastian Muraza alisema jumla ya miradi 4 yenye thamani ya sh bil 9.967inatarajiwa kutekelezwa katika vijiji 41.
Alibainisha kuwa miradi 3 kati ya hiyo ni mwendelezo wa miradi iliyoanza kutekelezwa mwaka jana na ile iliyoko katika hatua za manunuzi ambayo utekelezaji wake unaanza mwaka huu wa fedha ikiwemo mradi 1 wa kusaidia matengenezo makubwa.
Alisema kutekelezwa kwa miradi hiyo kutaongeza upatikanaji huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo kwa asilimia 17 hivyo huduma hiyo kupanda kutoka asilimia 72 ya sasa hadi 89 hivyo kuvuka lengo la serikali la kufikia asilimia 85 ifikapo 2025.
Mhandisi Marwa alitaja miradi itakayotekelezwa kuwa ni ukamilishaji wa upanuzi wa mradi wa maji ya Ziwa Victoria kutoka Ziba kwenda Nkinga, Mwanzelwa, Kitangili, Itulashilangi, Ulaya, Barazani, Ugaka, Ikunguipina, Njiapanda na Simbo.
Mradi huo utakaohusisha ujenzi wa matenki 4, uchimbaji na ulazaji bomba la mita 51,433 na kufukia na ujenzi wa vituo 30 (dp’s) vya kuchotea maji utagharimu kiasi cha sh bil 4.5 na utanufaisha wakazi wa vijiji 19 katika kata 7 kati ya kata zote 35.
Alitaja mradi mwingine kuwa ni ukamilishaji upanuzi mradi wa Ziwa Victoria wa Bukoko-Mtungulu, Matinje-Choma na Mwasung’ho-Mwamapuli utakaonufaisha wakazi wa vijiji 4 vya kata za Bukoko, Mtungulu, Matinje na Choma kwa gharama ya sh bil 4.5.
Meneja aliongeza miradi mingine kuwa ni upanuzi wa mradi wa maji wa Ziwa Victoria kutoka Igogo kwenda Igurubi utakaotekelezwa katika kata 8 na kunufaisha wakazi wa vijiji 18 vilivyoko katika kata hizo utakaogharimu sh bil 5.2.
Mradi wa 4 ni wa ukarabati na matengenezo ya miradi ya maji ya wananchi ya bomba na visima iliyopo katika kata zote 35 za wilaya hiyo, ambao utahusisha ununuzi wa vipuri, bomba, pampu, ufundi na gharama nyinginezo, sh mil 200 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
‘Tunamshukuru sana mama yetu Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha za kutosha ili kumalizia miradi yote ya mwaka jana na miradi mipya ya mwaka huu wa fedha 2023/2024, hakika KAZI IENDELEE,’ alisema.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Lucas Bugota alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Wakala huo Wilayani humo na kubainisha kuwa kwa kasi hiyo kero ya maji katika wilaya hiyo sasa itabakia kuwa historia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇