LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 14, 2023

MADIWANI MANISPAA TABORA WAPITISHA BAJETI YA MAENDELEO YA BIL 47.18

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa Tabora Ramadhan Kapela akihamasisha shughuli za maendeleo kwa wananchi katika moja ya ziara zake Mkoani humo hivi karibuni.Picha na Allan Kitwe
 Na Allan Kitwe, Tabora

BARAZA la madiwani la Halmashauri ya Manispaa Tabora limepitisha makisio ya bajeti ya mapato na matumizi ya sh bil 47.18 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ili kufanikisha utekelezaji shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi.

Akiwasilisha bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Dkt Peter Nyanja, Afisa Mipango wa Manispaa hiyo Nelson Mwankina alisema kiasi hicho kitatokana na fedha za mapato ya ndani, ruzuku ya serikali kuu na michango ya wahisani.

Alisema kati ya fedha hizo sh bil 28.7 ni ruzuku ya mishahara kutoka serikali kuu, sh mil 955.6 ni ruzuku ya matumizi ya kawaida kutoka serikali kuu na sh bil 2.8 ni fedha za matumizi ya kawaida kutoka kwenye mapato ya ndani.

Aliongeza kuwa kiasi cha sh bil 14.2 ni fedha za miradi ya maendeleo ambapo bil 4.2 zitatokana na mapato ya ndani ya halmashauri na bil 6.5 ni ruzuku ya serikali kuu kwa fedha za ndani huku bil 3.3 zikiwa ruzuku ya serikali kuu kutoka kwa wahisani wa nje ikiwemo mapato fungwa sh mil 357.7.

Mwankina alisema halmashauri imekadiria kukusanya sh bil 7.5 kutoka katika mapato yake ya ndani sawa na ongezeko la asilimia 34.4 la makisio ya mwaka jana, mapato yasiyofungwa ni sh bil 71.16 na mapato fungwa ni mil 357.7.

Alibainisha makusanyo ya halmashauri kwa vyanzo vilivyoongezeka kuwa ni sh mil 992 za ushuru wa huduma ambapo mwaka jana ilikuwa sh mil 800, ushuru wa kituo cha mabasi sh mil 307 na ushuru wa nyumba za kulala wageni sh mil 188.5.

Vyanzo vingine ni ushuru wa maegesho sh mil 293.8 ambayo ni sawa na ongezeko la sh mil198, ada ya vibali vya ujenzi sh mil 45.3, ushuru wa madini sh mil 759.6 tofauti na sh mil 29 za mwaka jana na ushuru wa vyoo sh mil 344.8.

Alitaja vyanzo vingine kuwa ni uuzaji viwanja ambapo wanatarajia kukusanya kiasi cha sh mil 600 sawa na ongezeko la sh mil 373 za mapato ya mwaka jana na kodi ya pango kiasi cha sh mil 506.7 ambacho ni pungufu ya sh bil 1.2 za mwaka jana kutokana na kuvunjwa kwa baadhi ya mabanda kupisha ujenzi wa soko jipya.

Mstahiki Meya wa manispaa hiyo Ramadhan Kapela alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anazofanya ikiwemo kuhakikisha miradi yote iliyopangwa kutekelezwa na halmashauri inatekelezwa kwa vitendo.

Aidha alimshukuru kwa kuwapatia asilimia 100 ya makisio ya bajeti ya maendeleo ya manispaa yao hali iliyopelekea kufanikisha utekelezaji wa miradi yao yote kwa asilimia 100. 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages