Na Lydia Lugakila
Katika harakati za kuhakikisha ufaulu unaongezeka kwa wanafunzi kupitia alama za ufaulu, waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa Mhe. Angella Kairuki ameagiza kila walimu kujiwekea malengo binafsi katika msomo wanayofundisha ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeshindwa kupata umahiri alioukusudia katika somo lake huku akibainisha malengo mapya ya alama za ufaulu kwa wanafunzi kwa mwaka 2023.
Waziri Kairuki ametoa kauli hiyo Januari 18, 2023 wakati akizungumza katika kikao kazi cha tathimini ya utekelezaji wa mkakati wa elimu na uwekaji wa mpango kazi wa utekelezaji kwa mwaka 2023 kilichofanyika katika ukumbi wa Sido Rwamishenye manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Amesema kuwa kutokana na Hali ya ufaulu kuonekana kutokuwa nzuri kwa mwaka 2022 tayari serikali imejipanga mwaka huu 2023 na kuamua kuja ki vingine ili kuboresha sekta ya elimu.
Amesema kuwa katika ufaulu upande wa sekondari kwa kidato cha nne malengo waliyojiwekea ni kufikisha wastani wa alama 50 kwenda juu ili kuondoa alama F ambapo kwa shule za msingi kiwango cha ufaulu kitaishia alama C.
Amesema kuwa mwanafunzi wa kidato cha nne asione amefikisha alama 50 akaona inatosha bali ajitahidi kwenda juu ili kutimiza malengo mapya ya ufaulu kwa mwaka 2023 katika sekita hiyo.
Aidha ameongeza kuwa lazima walimu na viongozi wa mkoa huo kuweka mkazo zaidi katika hilo ili mwanafunzi anapochagua masomo yake baada ya kidato cha 5 au elimu ya juu basi awe kweli amechagua kutokana na hali nzuri ya ufaulu.
Ameongeza kuwa ni vyema kila kiongozi kuwajibika katika nafasi yake ili kuongeza tija sehemu ya kazi husika ikiwa ni pamoja na kuondokana na suala la utoro kwa wanafunzi na walimu kutokana na kuwepo kwa maudhurio hafifu kwa wanafunzi na baadhi ya viongozi .
Amewapongeza walimu kwa jinsi wanavyopambana katika ufundishaji huku akiwaomba viongozi wa mkoa wilaya halmashauri kuendelea kuasaidiana na wataalam wa elimu ili kuhakisha kunakuwa na maudhurio kwa asilimia 100 kwa wanafunzi shuleni na kuhakikisha wanakomesha suala la utoro.
Hata hivyo kwa upande wake naibu katibu mkuu (Elimu) ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa Charles Msonde amesema serikali itaendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu na kupunguza vikwazo vinavyosababisha wanafunzi kuacha shule pamoja na kupunguza changamoto katika sekta hiyo.
Naye mkuu wa mkoa wa Kagera Albert John Chalamila ameshukuru ujio wa Waziri Kairuki na kumuomba kupeleka ombi kwa Rais Dokta Samia kuwaongezea walimu katika Mkoa wa Kagera licha ya jitihada zinazoendelea za kuongeza walimu huku akimpongeza kwa kuboresha sekta ya elimu mkoani Kagera.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇