Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na wananchi wakati wa zoezi la la upandaji miti kando ya barabara jijini Dodoma leo Januari 10, 2023 ikiwa ni Wiki ya Maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri akipanda miti kando ya barabara jijini Dodoma leo Januari 10, 2023 ikiwa ni Wiki ya Maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru akipanda mti.
Mafuru akielezea mpango mkakati wa kuijakinisha Dodoma
Waziri Jafo akiwa na baadhi ya wadau wa mazingira pamoja na wanafunzi.
Waziri Jafo akihamasisha wanafunzi kupenda utunzaji wa mazingira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia zoezi la upandaji miti katika maeneo yao ili kufikia lengo lililowekwa na Serikali.
Pia, amewataka viongozi wa majiji na manispaa kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara Mijiji na Vijijini (TARURA) kuwa na miti ya kutosha kando ya barabara zinazopopita katika maeneo yao ili kuhifadhi mazingira.
Dkt. Jafo ametoa kauli hiyo leo Januari 10, 2023 wakati akiongoza zoezi la upandaji miti kando ya barabara jijini Dodoma ikiwa ni Wiki ya Maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Amesema baada ya nchi yetu kukumbwa na ukame katika baadhi ya maeneo ni vyema sasa wananchi wakatumia mvua hizi zinazoendelea kunyesha kupanda miti ya kutosha katika maeneo yetu na kwenye vyanzo vya maji.
“Viongozi twendeni tukasimamia wilaya zetu kwa kupanda miti milioni 1 na laki tano kwa kila halmashauri ili tufikie lengo la kupanda miti milioni 276 sasa jambo hili tutalifanikisha kwa kutumia mvua hizi kupanda miti, hapa nataka niwapongeze Dodoma mmeonesha mfano na ndani ya miaka mitatu mtakuwa jiji la mfano kwa utunzaji mazingira,” amesema.
Akiendelea kuzungumza na wananchi pia Waziri Jafo amewataka wataalamu wa kilimo wabainishe aina za miti ipandwe katika maeneo gani ili kueupuka changamoto ya baadhi ya miti kufa.
Aidha, amewataka wakuu wa shule nchini kuhakikisha kila mwanafunzi anayeandikishwa shuleni kuhakikisha anapewa mti mmoja wa kupanda ili kuendana na Kampeni ya ‘Soma na Mti’ ambayo inalenga kupanda miti zaidi ya milioni 14.5.
Sanjari na hilo pia amesisitiza kila mwananchi anayeomba kibali cha ujenzi wa nyumba hakikishe anakuwa na mpango wa kupanda miti angalau mitatu na kuendelea ili tuwe na miti ya kutosha hivyo azma ya kupambana na athari z mabadiliko ya tabianchi inafanikiwa.
Zoezi la upandaji miti limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri, wanafunzi, wadau wa mazingira na wananchi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇