Na Mwandishi Maalum, Z'bar.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinajivunia mabadiliko makubwa yaliyofikiwa Zanzibar katika kipindi cha miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ambayo yamewafanya Wananchi kujiamini na kujiitegemea kimaendeleo.
Hayo yamesemwa leo mjini Zanzibar na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka katika mahojiano maalum, kuhusu Mapinduzi hayo yaliyofanyika Januari 12, 1964.
"Zanzibar imepiga hatua kubwa sana na CCM inatoa pongezi za dhati kwa kazi kubwa iliyokwishafanywa na inayoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya nane chini ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, ikiendelea kuunga mkono juhudi za kukomesha ukandamizaji wa haki , ubaguzi, dhulma na manyanyaso.
Katika kipindi cha miaka 59 ya Mapinduzi matukufu licha ya kuleta ukombozi kamili lakini pia yamewafanya wananachi kuwa na fikra huru na kujitawala" alisema Shaka na kuongeza;
"Kabla ya mapinduzi lipo tabaka lilokandamiza, kubagua na kuwapuuza wengine huku wananachi wakikosa haki za msingi na kutotumia fursa za kiuchumi sawa na utu wao kutothaminiwa, na kupuuzwa.
Mapinduzi ya mwaka 1964 ni ushahidi kuwa Zanzibar ilikuwa na watu waliokoseshwa elimu bora, kutomiliki uchumi, ardhi, kukosa makaazi bora na kunyimwa huduma za jamii".
Alisema, Serikali zote (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) zimetimiza wajibu wa kusimamia maendeleo. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais Dk. Mwinyi baada ya miaka 59 wametafsiri mapinduzi ya ukombozi kuwa Mapinduzi ya kiuchumi. Maendeleo yanayoonekana sasa hayakuwepo miaka 200 ya utawala wa kikoloni,
Alisema, kazi kubwa iliyofanywa na Chama cha ASP ilikuwa kuhakikisha utawala wa ukandamizaji, uonevu na ubaguzi wa huduma za jamii unakomeshwa katika visiwa vya Unguja na Pemba kwa sera ya mapinduzi ya ukombozi na kazi iliyobaki ni kujenga uchumi na maendeleo.
"Ni vyema kwa watendaji waliopewa dhamana katika Serikali na taasisi za umma kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kumsaidia Rais Dk. Mwinyi ili akamilikshe kazi ya kutekeleza mapinduzi ya kiuchumi na kuongeza Kasi ya kuleta maendeleo.
Kazi ya kumwondoa mkoloni aliyetawala kwa ubaguzi na ukandamizaji imemalizika. Kazi iliyobaki ni kuongoza kwa haki, umoja na maendeleo. Kukumbuka madhila yaliyokuwepo kabla ya mapinduzi kunatupa ari ya kufikia mabadiliko tuanayoyataka," alisema Shaka.
Alisema, baada ya kufanikisha mapinduzi ya mwaka 1964 na utawala kushikwa na ASP, Rais wa kwanza wa Zanzibar hayati Mzee Abeid Amani Karume alianza utekelezaji wa sera za maendeleo ikiwemo kutolewa bure kwa huduma za msingi.
"Elimu imetolewa bure, maji safi na matibabu, serikali ikaweka viwango vya mishahara minono kwa mujibu wa ajira ya kila mfanyakazi, yamejengwa makaazi ya kisasa na sasa kazi hiyo inaendelezwa na serikali ya Rais Dk. Mwinyi.
"Ni waombe watanzania wenzangu hasa vijana kutobabaishwa na porojo za baadhi ya wapinga maendeleo na mapinduzi matukufu ya 1964 ambao wamekuwa wapotoshaji wa ukweli kwa kudai serikali za CCM hazijafanya lolote tangu mwaka 1964 wakati asiliamia 98 ya maendeleo yaliyofanyika nchini yamepatikana katika utawala wa Chama Cha Mapinduzi" alihitimisha Shaka mahojiano hayo.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shaka Hamdu Shaka, akizungumza katika Studio za Wasafi TV mjini Zanzibar, leo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇