Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kujenga vituo vya utafiti wa madini nchini (Ofisi za GST) kupitia Taasisi ya Jiologia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kutoa huduma za upimaji wa sampuli za miamba, mbale, tope, marudio, vimiminika na udongo ili kutambua madini mbalimbali yaliyopo katika sampuli hizo.
Hayo yamebainishwa na Dkt. Biteko hivi karibuni katika kikao kilichofanyika Mkoani Geita na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini.
Dkt. Biteko amebainisha kuwa, kituo kikubwa cha utafiti wa madini nchini kinajengwa mkoani Geita ambapo ujenzi unaendelea. Amesema awali kulikuwa na kituo kimoja cha utafiti mkoa wa Dodoma pekee na sasa Serikali inajenga kituo cha pili Geita.
Akizungumzia kituo hicho cha GST baada ya kukamilika kwake, Serikali itapeleka wataalam, magari na huduma mbalimbali za GST ili wachimbaji wapate huduma.
Vile vile, amesisitiza kuwa baada ya kukamilika kwa kituo cha Geita kituo kingine kikubwa kitajengwa katika wilaya ya Chunya na baadaye maeneo mbalimbali hapa nchini.
Akizungumzia shughuli za utafiti, amesema ni eneo lenye gharama kubwa zaidi katika shughuli za uchimbaji wa madini na kuongeza kuwa tayari Serikali ina ramani ya uwepo wa madini mbalimbali nchi nzima.
"Ili uweze kusema madini yapo hapa kiasi gani na utachimba mita ngapi hakuna muujiza zaidi ya kufanya uchorongaji,” amesema Dkt. Biteko
Amesema kuwa, kutokana na gharama kuwa kubwa ya utafiti wa madini Serikali imetoa taarifa za awali za uwepo wa miamba ya madini kwa sehemu husika.
Pamoja na uwepo wa vituo hivyo, pia GST inatoa huduma ya ushauri elekezi kwa wachimbaji wadogo na wadau wa Sekta ya Madini kwa ujumla wake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇