Na Dismas Lyassa
WANANCHI wa Wilaya ya Kilombero yenye majimbo mawili ya Kilombero na Mlimba wamewapongeza Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo ndugu Mohamed Msuya (pichani chini) kwa kusimamia vizuri chama na serikali, Mbunge wa Jimbo la Mlimba Godwin Kunambi na Mbunge wa Kilombero Abubar Assenga kwa kuwa kipaumbele katika kupigania maendeleo katika majimbo yao.
“Kuna mambo yanaendelea sasa chini ya mwenyekiti Msuya katika wilaya yetu ni kama ndoto, kuona wabunge wanakuwa karibu sana na wananchi, wabunge wanatumia muda mwingi kufuatilia masuala ya maendeleo ikiwamo kufanya ziara. Mfano katika jimbo la Mlimba kuliwahi kuongozwa na wapinzani, mambo hayakuwa hivi, hapakuwa na ufuatiliaji wa maendeleo kama tunavyoona leo chini ya ndugu Msuya,” anasema James Mbaule mkazi wa Ifakara.
Wananchi wengi waliohojiwa kwa nyakati tofauti katika kata na vijiji tofauti wanasema wanafurahi wanapoona mwenyekiti Msuya amekuwa karibu na madiwani na viongozi wengine hasa kitendo chake cha kuhamasisha viongozi kufanya ziara za mara kwa mara za maendeleo.
“Tuna matumaini kuwa changamoto nyingi zilizoko zikiwamo umeme kutofika kwa wananchi wote wenye uhitaji kwenye baadhi ya vijiji kama Mofu, Ikwambi nk changamoto ya barabara na madaraja, maji na kadhalika zitatatuliwa…siku zote umoja ni ushindi, nafurahishwa na umoja imara unaoendelea kuwepo baina ya viongozi wa chama tawala na wale wa Serikali katika kushughulikia maendeleo,” anasema James Mbanile.
Mbunge wa Jimbo la Mlimba, ndugu Kunambi |
Akizungumza katika na Blog hii ya Taifa ya CCM (CCMChama Blog), mwenyekiti wa CCM Wilaya Kilombero, ndugu Mohamed Msuya alisema msingi wa maendeleo ni ushirikiano na kwa kufahamu hilo amekuwa karibu na viongozi na wananchi wenzake wa Kilombero na Mlimba.
“Nafanya kazi vizuri na viongozi wote, tuna ushirikiano mzuri, hii ndio siri yetu kubwa ya kuweza kuharakisha maendeleo katika majimbo yetu haya mawili ya Kilombero na Mlimba,” anasema Msuya.
Ndugu Msuya anasisitiza kuwa,”Wakati nagombea nafasi hii niliahidi kushirikiana na kufanya ziara mara kwa mara kwa kushirikiana na wabunge na viongozi wengine wa Serikali ili kwa pamoja tuweze kuendelea kutatua kero za wananchi, ndivyo ninachokifanya sasa kwa vitendo”.
Mbunge wa Jimbo la Kilombero, ndugu Assenga
Maagizo ya kuwa karibu na wananchi ikiwamo kufanya ziara yameshushwa pia kwa madiwani na viongozi wa vijiji na kata kama njia ya kufahamu kero za wananchi na kuzichukulia hatua.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇