LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 10, 2023

GoT-HoMIS SULUHISHO KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA

Mkurugenzi wa Huduma za Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka TAMISEMI Dkt Ntuli Kapologwe akizungumza na Kamati za huduma za afya Mkoa (RHMT) na za wilaya (CHMT),wakati wa ziara yake Mkoani Mara hivi karibuni.

 NI miaka takribani sita tangu serikali ilipoanza matumizi ya Mfumo Madhubuti wa Usimamizi na Uendeshaji wa Vituo vya Kutolea Huduma za Afya GoT-HOMIS ambao matumizi yake yameleta matokeo chanya katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.


Mfumo huo wa kielektroniki umewekwa kwa lengo mahsusi  la kusimamia  shughuli za uendeshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya.


Lengo lingine ni kusaidia kurahisisha shughuli za vituo vya kutolea huduma za afya na kusimamia uzalishaji na uhifadhi sahihi wa taarifa na takwimu za wagonjwa na magonjwa ,mapato na dawa za vituo vya kutolea huduma za afya.


Mkurugenzi wa Huduma za Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais (TAMISEMI),Dkt Ntuli Kapologwe akizungumza na kamati za huduma za afya mkoa (RHMT),na za wilaya (CHMT)akiwa ziarani Mkoani Mara anasema mfumo huo sio tu unasaidia  kuboresha huduma za afya nchini bali pia unasaidia kuleta tija na upatikanaji wa haraka wa takwimu mbalimbali na kwa wakati.


Aidha,anasema mfumo umesaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi,umesaidia upatikanaji wa taarifa sahihi kwa ajili ya kufanya maamuzi kwa wakati,umepunguza gharama za upatikanaji wa taarifa na umeongeza uwajibikaji.


“Ukiachana na hayo kubwa tunaloweza kusema kupitia mfumo huu ni umesaidia kuchochea ongezeko la mapato katika vituo vyetu vya afya,kujua matumizi ya dawa hadi ngazi ya mtoa huduma,hivi karibuni nilifanya ziara kwenye vituo na tumejionea ufanisi wake,”anasema.


Dkt Kapologwe anabainisha kuwa mfumo wa GoT-HOMIS umeunganishwa na mfumo wa NHIF ili taarifa za mteja au mwanachama  ziweza kuhakikiwa na kukiwezesha kituo cha kutolea huduma kulipwa madai yake ya NHIF bila ya usumbufu.


Mganga mfawidhi kituo cha afya Nyasho kilichopo Halmashauri ya wilaya ya Musoma Mkoani Mara Dkt Emmanuel Shani anaeleza kuwa kabla ya kufunga mfumo huo walikuwa wanaingiza Sh Milioni 2 hadi 3 kwa mwaka, lakini baada ya kufunga mfumo kwa mwaka wanaingiza Sh Milioni 151 kwa mujibu wa taarifa ya mwaka wa fedha wa 2021/2022.


Anasema kupitia ongezeko hilo la mapato ya ndani wameweza kuimarisha huduma wanazotoa kwa wananchi kwa kufanya ukarabati  wa gari la wagonjwa ambalo kwa sasa linafanya kazi vizuri.


“Tumeweza pia kufanya ukarabati wa chumba cha kitengo cha kinga na meno ,ukarabati wa mashine ya dental ,kununua dental set na vifaa vingine kwa ajili ya huduma ya kinywa na meno na sasa tunafanya ujenzi wa duka la dawa la jamii,”anasema.


Mhasibu wa Kituo cha Afya cha Nyasho Farida Musa anasema kabla ya kuanza kutumia mfumo huo changamoto zilikuwa kubwa ikiwemo mteja kushindwa kupata risiti ambayo ni halali.


“Mteja sasa hivi akitoa hela anapata huduma na risiti yake ya mashine anapewa,hii inaongeza uaminifu anakuwa na uhakika kweli gharama nilizotajiwa na sahihi,”anafafanua.


Mteknolojia dawa kutoka Kituo cha afya cha Natta kilichopo wilayani Serengeti Mkoani Mara Saida Ahmed anasema kupitia mfumo huo wamepata matokeo chanya kwenye utoaji wa huduma ambapo kwa sasa mgonjwa hapati shida ya kuzunguka na faili.


“Kabla ya mfumo huu mgonjwa alikuwa anazunguka na faili kutoka dirisha moja kwenda lingine kwa ajili ya kupata huduma za kitabibu,lakini kwa sasa mgonjwa akifika taarifa zake za awali zinakuwepo na zinatumwa kwa daktari husika,hivyo usumbufu wa kubeba faili haupo tena,”anasisitiza.


Mkazi wa Musoma Mkoani Mara Juma Kiboko anaishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za afya ambapo kupitia mfumo huo umeweza kuondoa usumbufu kwa wao wananchi.


“Zamani ilikuwa kila ukifika hospitali unatoa taarifa upya lakini kwa sasa mfumo unatunza taarifa zetu hivyo tukifika kituoni unataja jina taarifa zako zinakuja unaeleza tatizo tu linalokusumbua,”anasema.


Mwaka 2017,serikali ilianzisha mfumo wa GoT- HoMIS ili kutambua umuhimu wa upatikanaji wa taarifa za afya pamoja na udhibiti wa mapato kwenye Hospitali,Vituo vya Afya na Zahanati.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages