Dkt. Biteko awataka wafanyabiashara wa kemikali za kuchenjua madini kuuza kwa kufuata bei elekezi
Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Serikali imeanza kuchukua hatua kwa wafanyabiashara wa kemikali ya kuchenjua madini ya dhahabu ( Sodium Cyanide) ambao hawatendi haki kwa wachimbaji wadogo.
Hayo yamebainishwa Januari 7, 2023 katika kikao cha pili cha wadau wanaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa Sodium Cyanide nchini inayotumika katika shughuli za kuchenjua madini ya dhahabu iliyofanyika katika ukumbi wa TMDA Buzuruga Jijini Mwanza
Amesema, amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wachimbaji wadogo kuwa kemikali ya kuchenjua madini ya dhahabu aina ya “Sodium Cyanide” inauzwa bei ya juu kwa shilingi laki nane (800,000) kwa dumu moja tofauti na bei iliyoelekezwa na Serikali ambayo ni shilingi laki sita (600,000) kwa dumu.
Amesema, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haiko tayari kuona wachimbaji wadogo wanakwamishwa kwa hali yoyote hivyo amemuelekeza Mkemia Mkuu wa Serikali kuwafuatilia na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaouza kemikali hizo kinyume na bei elekezi.
"Wapo hapa miongoni mwenu nimewatembelea nataka niwapongeze sana kwa uaminifu wao kwa sababu hawakutanguliza tamaa mbele walitanguliza kumfanya mchimbaji awepo," amesisitiza Dkt. Biteko.
Pia, ametoa ushauri kwa Mkemia Mkuu kutoa kibali kwa mtu mwaminifu, utengenezwe utaratibu wa kuwa na kiapo na kuwasilisha nyaraka ya kuonyesha mauzo ya kemikali hiyo na kuongeza makali ya Kanuni ili kuwasimamia vizuri wafanyabiashara hao.
Awali, Mkurugenzi wa udhibiti na usimamizi wa kemikali kutoka Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndio akizungumza kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali amesema maelekezo yote aliyotoa Waziri Dkt. Biteko yataanza kufanyiwa kazi mara moja.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima amempongeza Raisi Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuisimamia Sekta ya Madini na kueleza kuwa Waziri wa Madini amefanya kazi nzuri katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini.
Naye, Raisi wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) John Bina amempongeza Waziri Biteko kwa namna ambavyo Sekta ya Madini imekua kutoka kwenye uchenjuaji wa kutumia kemikali ya “Mercury” na kuhamia “Sodium Cyanide”.
Mkutano huo wa pili wa wadau wanaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa Sodium Cyanide imehudhuriwa na wachimbaji wa madini, viongozi wawakilishi wa wachimbaji , Viongozi na watumishi wa Serikali
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇