BAADHI ya wateja wa NMB na wafanyakazi katika tawi la NMB Tunduru mkoani Ruvuma ambao walishiriki kushuhudia droo ya NMB bonge la Mpango mchongo wa kusini ambayo ilichezeshwa katika tawi la NMB Tunduru ambapo wateja watano kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara walishinda kila mmoja fedha taslimu shilingi 500,000 na chama kimoja cha msingi cha Ushirika cha Tuyangatane wilayani Newala mkoani Mtwara kilishinda pikipiki yenye thamani ya shilingi milioni tatu.
Meneja wa NMB Tawi la Tunduru akizungumza kwenye droo ya NMB bonge la Mpango mchongo nwa kusini iliyochezwa katika tawi la Tunduru
……………………………………..
WATEJA watano wa Benki ya NMB Kanda ya Kusini wamejishindia shilingi 500,000 kupitia NMB Bonge la Mpango Mchongo wa kusini.
Wateja hao wameshinda katika droo iliyochezeshwa kwenye tawi la Benki ya NMB Tunduru,kupitia droo hiyo Chama cha Ushirika cha Msingi (AMCOS) cha Tuyangatane cha Newala mkoani Mtwara kimejishindia pikipiki yenye thamani ya shilingi milioni tatu.
Mwakilishi wa Meneja wa NMB kanda ya Kusini Roman Degeleki amesema NMB Bonge la Mpango Mchongo wa Kusini linashirikisha wateja wa NMB kutoka mikoa ya Ruvuma,Lindi na Mtwara .
Amewataja wateja watano wa NMB Bonge la Mpango Mchongo wa Kusini waliojishindia shilingi laki moja kila mmoja kwenye droo ya Tunduru kuwa ni Daudi Salim Randy wa Ndanda Mtwara,Erick Christopher Chisigalile wa Newala Mtwara,Mangungu Murtaza Ally wa Kilwa Lindi,Dismass Agustino Tarimo wa Newala Mtwara na Abubakar Mohamed Msham wa Kilwa Lindi.
Amelitaja tawi la NMB Tunduru kuwa ni miongoni mwa matawi 19 ya benki hiyo katika Kanda ya kusini ambayo yana wateja wengi wanatumia huduma za NMB ndiyo maana benki hiyo imeamua kuchezesha droo ya NMB bonge la Mpango kwenye tawi hilo.
‘’NMB bonge la mpango mchongo wa kusini ni kampeni maalum iliyoandaliwa na NMB kwa ajili ya wakazi wa kusini tu”,alisisitiza Roman.
Kwa upande wake mgeni kwenye hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mheshimiwa Julius Mtatiro ameipongeza NMB kwa kuamua kuchezesha droo bonge la mpango mchongo wa kusini katika tawi la Tunduru.Amesema droo hiyo imetoa fursa kwa wateja wa NMB binafsi na vyama vya Ushirika vya msingi kushinda pikipiki na pesa tasilimu.
Ameitaja NMB kuwa ndiyo benki kubwa nchini ambayo imekuwa inatoa huduma za kibenki mijini na vijijini hivyo kuwa karibu zaidi na wateja.
Kwa upande wake Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Bisani George akizungumza kwenye hafla hiyo ametoa rai kwa vyama vya Ushirika vya Msingi kujiunga na NMB ili kunufaika na huduma mbalimbali. Afisa Ushirika huyo pia ameipongeza NMB kwa kuwahudumia wakulima na wanachama wa vyama vya Ushirika katika Halmashauri hiyo kwa kutoa mikopo na huduma nyingine za kibenki.
Naye Salum Mohamed mwananchi wa Tunduru ameipongeza NMB kwa kuchezesha droo hiyo katika tawi la Tunduru ambapo amesema italeta hamasa kubwa wananchi kujitokeza kwenye droo ya NMB bonge la mpango mchongo wa kusini kwenye droo zitakazofuata.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇