LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 21, 2022

MKURABITA KUJENGA KITUO JUMUISHI CHA URASIMISHAJI NA UENDELEZAJI BIASHARA KIBAHA

 

 Na Byarugaba Innocent, Kibaha


Halmashauri ya Mji Kibaha inatarajia kufungua kituo jumuishi cha urasimishaji
 na undelezaji biashara  (One Stop Centre) Januari mwakani, 2023 ili kuwarahisishia wajasiriamali kurasimisha biashara zao. 


Hayo ameeleza Kaimu Mkuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Halmashauri ya Mji Kibaha Adolf Msangi wakati wa mafunzo ya namna ya uboreshaji wa biashara ili ziweze kurasimishwa na kukidhi vigezo vya ushindani wa biashara kwenye soko yaliyofanyika kwenye Ukumbi Mkubwa  wa Ofisi ya Mkurugenzi ambapo zaidi ya wadau  wafanyabiashara 300 wameshiriki

Msangi alisema kuwa kituo hicho cha huduma za pamoja kitakuwa na Taasisi wezeshi zote ambazo zinahusika katika kurasimisha biashara ili kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara kusajili biashara zao.

"Kituo hichi kwa sasa kiko hatua za mwisho ambapo ni hatua ya manunuzi na Januari mwakani kituo kitaanza kazi na kitawarahisishia wajasiriamali badala ya kwenda ofisi sehemu tofauti watakuwa wanakwenda sehemu moja na kumaliza usajili sehemu moja,"alisema Msangi.

Alisema kuwa kituo hicho kitakuwa na Taasisi zikiwemo Tra, mabenki, Osha, bima, Latra na Taasisi zinazohusika na masuala ya biashara na usimamizi zote zikiwa kwenye jengo moja.

Aidha alisema kuwa Halmashauri imetoa sehemu ya jengo lake kwa ajili kuanzishwa kituo hicho ambapo Halmashauri ya Mji Kibaha inaongoza kwa kuwa na viwanda vingi Mkoani Pwani.

Kwa upande wake ofisa utawala kutoka MKURABITA Joseph Temanya alisema kuwa lengo la kuwarasimisha wafanyabiashara wadogo ni kuweza kufikia fursa mbalimbali.

Temanya alisema kuwa fursa zilizopo ni pamoja na za mikopo, ujuzi wa uendeshaji biashara na fursa mbalimbali za masoko na uboreshaji bidhaa na biashara zao.

Naye Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Pwani Philemon Maliga alisema kuwa kurasimishwa kwa biashara zao kutawasaidia kutambulika na kuweza kukopesheka na kuwa na maeneo rasmi kwa ajili ya biashara zao.

Maliga alisema kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho itakuwa imewarahisishia kurasimisha biashara zao na kupata usajili kwa urahisi kwani zamani walikuwa wanapata usumbufu kuzunguka sehemu mbalimbali kwa ajili ya urasimishaji biashara.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages