MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT),Marry Chatanda amechangia Shilingi Milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa jengo la watoto wadogo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Bethel uliopo Chadulu kama sehemu ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa nafasi aliyoipata.
Aidha,amekabidhi mifuko 100 ya Saruji kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Rais Dokta Samia Suluhu Hassan kufuatia harambee iliyofanyika Disemba 4,2022 kanisani hapo.
Akikabidhi saruji hizo Chatanda amesema alikwenda katika kanisa hilo kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa mambo makuu aliyomtendea kwa kupata uenyekiti wa UWT Taifa.
“Nilipokuja hapa nilikuta kuna harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo la watoto nikatoa Milioni moja na kuahidi saruji mifuko 100,leo (Disemba 5) tulipomaliza kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM nikamdokeza Rais Samia kuhusu ahadi yangu,Rais akatoa mifuko hiyo ya saruji niliyoikabidhi hapa,hivyo nimekabidhi kwa niaba yake,”amesema.
Katika makabidhiano hayo Chatanda aliambatana na Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma Pili Mbanga,Wabunge wa Viti Maalum Mariam Ditopile na Fatma Towfiq na Mwenyekiti mstaafu wa UWT Mkoa wa Singida Diana Chilolo ambao walichangia mifuko 40 ya saruji na Shilingi 50,000.
Akitoa neno la shukrani Mchungaji Gershom Ngewe wa Kanisa hilo la KKKT amemshukuru Rais Samia kwa msaada aliotoa na kumuombea heri katika uongozi wake.
“Ujenzi huu utagharimu zaidi ya Sh Bilioni 1.8 kwa kuwa tutajenga ghorofa nne,maktaba,madarasa ya watoto,ofisi mbalimbali,maeneo ya vikao,tunakushukuru sana na Mungu akutangulie,wakati huu umeaminiwa wewe kutumika Mungu akutangulie,tunaomba utufikishie salamu zetu kwa Rais Dokta Samia kwamba tumepokea mchango wake kwa mikono miwili,”amesisitiza.
Chatanda katika uchaguzi uliofanyika Novemba 28,2022 aliibuka mshindi kwa kupata kura 527 kati ya kura halali 756 zilizopigwa.
Mdau, nakuomba uendelee kusikiliza kupitia clip hii ya video, Chatanda akizungumza baada ya kukabidhi mchango huo huku viongozi wa kanisa hilo wakitoa shukrani....
MHARIRI BLOG YA TAIFA YA CCM
0754264203
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇