Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balileakizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam wakati alipompongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua ambazo amechukua khusu ulinzi wa bonde la Ihefu.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam wakati alipompongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua ambazo amechukua khusu ulinzi wa bonde la Ihefu kushoto ni Habib Mchange Mwenyekiti wa Kituo cha Kutetea Rasilimali na Taarifa (MECIRA)
Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza kuwa yoyote aliyevamia Bonde la Ihefu aondolewe bila kuangalia ukubwa wa mtu na kwamba hakuna mkubwa kuliko sheria za nchi.
Rais Samia alitoa agizo hilo ikiwa ni muendelezo wa maagizo ya Makamu wa Rais Dk Philip Mpango ambaye alitoa agizo kwenye Kongamano liliandaliwa na Kituo cha Kutetea Rasilimali na Taarifa (MECIRA) na kufanyika Desemba 19 mwaka huu mkoani Iringa.
Balile amesema kitendo cha Rais Samia kusisitiza kubwa watu wote walioko Bonde la Ihefu wanapaswa kuondolewa bila kuangalia ukubwa wao na kwamba hakuna mkubwa kuliko sheria ni jambo la kupongeza na kuunga mkono.
“Tushukuru wana habari kwani kupitia kongamano letu la wanahabari na wadau mbalimbali wa mazingira limekuwa na mwitikio mkubwa sana, kwani maelekezo ya Makamu wa Rais Mpango yamekaziwa juzi na Rais Samia wakati akifanya zoezi la ujazaji maji Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), Disemba 22,2022 wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Mwenyekiti huyo wa TEF na mjumbe wa MECIRA amesema pamoja na kupongeza maelekezo ya Rais Samia na Makamu wake Dk Mpango, bado wanasisitiza sheria na haki itumike katika utekelezaji huo.
Amesema wapo wananchi ambao walikuwa wanajihusisha na kilimo, hivyo ni vema wakapewa muda ili kuvuma mazao yao na kuondoa miundombinu ambayo inaweza kuondolewa.
“Lengo la sisi kupiga kelele katika suala hili la Bonde la Ihefu wilayani Mbarali mkoani Mbeya sio kuwakomoa wakulima na wawekezaji, bali tunataka kuona zile hekta 83 zinarejea na maji ya kulisha Mto Ruaha Mkuu yanatiririka kama kawaida, hivyo tusisitiza misingi ya kisheria na haki izingatiwe,”amesema.
Balile amesema wakulima waliopo pale wamekopa mikopo benki na wana muda mrefu kwenye kazi hiyo, hivyo ingependeza wapewe mwaka mmoja au miwili kumaliza kuondoka.
Mwenyekiti huyo amesema pamoja na hatua hizo, wanashauri ujenzi wa tuta eneo la Giriama uanze sasa na kwamba wale ambao wamechepusha mto kusiwe na simile kuwaondoa.
Balile amesema kuhusu familia 16 ambazo zinamiliki hati za miaka 33 wanapaswa kuondolewa na wale wote ambao walihusika wachukuliwe hatua.
Amesema pia wanasisitiza waliopo kwenye ranchi ya Usangu waondolewe kwa kuwa GN namba 28 haiwatambui, hivyo hawapo kisheria.
Aidha, amesema agizo la Rais Samia kwa Wizara ya Ardhi na Kilimo kugawa eneo la heka 400 kwenye Bonde la Rufiji lifanyiwe kazi kwa haraka ili wakulima waende huko.
Mwenyekiti huyo amesema ni muhimu kuwepo maeneo maalumu kwa wafugaji ili kuepusha migogoro, huku akisisitiza kubwa ni wakati muafaka wa serikali kuwa na muongozo wa ufugaji ambao hauna madhara kwa kundi lingine.
Amesema MECIRA na waandishi watahakikisha wanaendelea kuandika na kuzungumza jambo la mazingira na uhifadhi bila kuhofia kufa kama ambavyo inasemwa na baadhi ya watu.
“Tunaamini watu wote wakiunga mkono mapambano hayo mazingira yatakuwa rafiki na kila mtu atakuwa salama, tuache kutishiana, tuwe wazalendo kwa maslahi ya nchi yetu, vitisho sio suluhisho, hakuna atakayeishi miaka 500,”amesema.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇