LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 1, 2022

MTEMVU ALAKIWA KWA KISHINDO OFISI YA CCM MKOA WA DAR ES SALAAM LEO, ATANGAZA KUJENGA CCM ISIYO NA UBAGUZI

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es Salaam Abbas Mtemvu leo amefanyiwa mapokezi rasmi katika Ofisi ya CCM mkoa huo, na kuahidi kujenga CCM isiyo na ubaguzi, iliyojaa upendo, furaha na mshikamano wa dhati baina ya viongozi na wanachama wote.

Mtemvu alichaguliwa kwa kishindo kwa kupata kura 444 na kumshinda mpinzani wake, Kate Kamba aliyekuwa akitetea kiti hicho ambapo alipata 160, akifuatiwa na Baraka Konisaga aliyepata kura 4 na Jamal Rwambow aliyeambulia kura mbili, katika Uchaguzi  uliofanyika Jumatatu ya Novemba 21, 2022.

"Niwaambia wanaCCM na wale viongozi wenzangu wote, kitu kikubwa ninachochukia dhuluma na rushwa hayo sitokubali Wanaccm wafanyiwe katika uongozi wangu," akasema Mtemvu akihutubia katika Mkutano huo wa mapokezi yake, uliojaa shamrashamra lukuki.

Mtemvu ambaye ni mbunge wa zamani wa Temeke, amesema uchaguzi huo umekwisha na sasa wanaingia na kujipanga chaguzi za mwaka 2024 na 2025 akisema malengo yake ni kuhakikisha chama kinapata mitaa, kata na majimbo yote ya Dar es Salaam.

Amesisitiza mwaka 2022 upo ukingoni sasa wanajipanga kuingia mwaka 2023, akisema yeye na viongozi wenzake watafanya ziara ya kata kwa kata kuangalia uhai wa chama hicho na kusikiliza maoni ya wanachama.

"Sasa ole wako nifike kwenye Kata Mwenyekiti au Katibu ushindwe kusema ndipo utamjua Mtemvu. Tunataka viongozi wanaojitambua ole wako nifike kwenye kata yako niambiwe upo kazini kwa nini uliogombea? Nataka viongozi wanaotumikia chama", akasema Mtemvu.

Mtemvu aliahidi pia kuhakikisha kila jambo linatendeka kwa haki, ikiwemo kutokatwa majina ya wagombea wanapokuwa wamependekezwa katika vikao halali vya maeneo yao.

Pia aliahidi kupambana kufa na kupona kuhakikisha wananchi wanyonge kama mamalishe na machinga hawaonewi na kukamatwa kamatwa hovyo hata pale wanapokuwa wakifanya katika maeneo yasiyo ya katazo.

Katika mapokezi hayo, Mtemvu aliambatana na Juma Simba Gadaffi ambaye katika Uchaguzi uliopita pia aliibuka kidedea kwa kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza, Gadaffi naye alisisitiza yeye na Mwenyekiti wake Mtemvu pamoja na viongozi wote wa mkoa wa Dar es Salaam kujenga CCM yenye neema na kutangaza kwamba tangu uchaguzi ulipomalizika viongozi wote waliochaguliwa hakuna aliyebaki na chembe ya kinyongo na kamwe hawafikirii kulipiza kisasi kwa yeyote aliyewakwanza na vyovyote vile.

Katika Mkutano huo wa mapokezi walihudhuria baadhi ya wabunge wa majimbo ya Dar es Salaam, Wenyeviti na Makatibu wa CCM na Jumuiya zake wa wilaya za Dar es Salaam, Wazee wa mkoa wa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa zamani wa CCM Ramadhani Madabida.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es Salaam Abbas Mtemvu, akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi aliyofanyiwa kwenye Ofisi ya CCM mkoa wa Dar es Salaam, leo. Kushoto ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Juma Simba Gadaffi. Chini ni Picha za matukio mbalimbali yaliyojiri katika mapokezi hayo👇👇





























No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages