Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa umeme vijijini (REA) Mhandisi Hassan Seif Saidy
Na Lydia Lugakila
Kagera.
Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa umeme vijijini (REA) Mhandisi Hassan Seif Saidy,amemtaka mkandarasi kutoka kampuni ya DIEYNEM CO. LTD) kuhakikisha anakamilisha mradi wa kusambaza umeme katika maeneo ya pembezoni mwa miji mkoani Kagera kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya nishati ya umeme.
Mhandisi Saidy ametoa maagizo hayo wakati wa makabidhiano ya mkataba wa mradi huo utakaotekelezwa kwa muda wa miezi 18 kuanzia Januari, 2023 katika wilaya za Karagwe, Bukoba na Muleba kusini yaliyofanyika katika ofisi za TANESCO Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa hakutakuwepo muda wa nyongeza wa kutekeleza mradi huo kwa sababu zozote zile hivyo ni lazima ukamilishe kwa muda uliopangwa.
"Fanya kazi kwa karibu na viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya mitaa, kata, wilaya, mkoa, wabunge pamoja na wananchi ili kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi huu ikiwa ni pamoja na kutumia vibarua wa eneo husika ili wafanye kazi vizuri na kulipwa stahiki zao kwa wakati, " alisema mkurugenzi huyo.
Pia amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha ananunua vifaa bora kutoka kwa wasambazaji wanaoaminika na kuwa REA hawatakubali kupokea mradi uliotekelezwa chini ya viwango kutokana na kutumia vifaa vibovu.
Ameongeza kuwa mradi huo unafanywa kwa fedha za serikali kwa asilimia 100 ambapo amemshukuru Rais Dkt Samia pamoja na wizara husika kwa kuwapatia bajeti ya kutosha.
Mkurugenzi amesema kuwa hakutakuwepo muda wa nyongeza wa kutekeleza mradi huo kwa sababu zozote zile hivyo ni lazima wakamilishe mradi huo kwa muda uliopangwa.
Mhandisi Saidy amemuagiza mkandarasi kuhakikisha pia anazingatia Sheria ya utunzaji wa mazingira wakati wa kutekeleza mradi huo ikiwa ni pamoja na kujiepusha kuharibu mazao na mali nyingine za wananchi jambo linaloweza kuzua migogoro isiyokuwa na tija kwenye maeneo ya mradi.
"Hatuleti umeme kwa ajili tu ya kukata migomba na kusimika nguzo bali tunaleta umeme ili kuboresha maisha ya wananchi kwa maeneo husika," alisema Saidy
Kwa upande wake meneja ufundi wa mradi kutoka kampuni ya Dieynem Limited, Mhandisi Novatus Lyimo, amesema kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi huo wataanza kufanya usanifu wa mradi mwezi Januari 2023 na watahakikisha wanazingatia matakwa ya mkataba ili kukamilisha mradi huo kwa wakati ifikapo mwezi Juni mwaka 2024.
Naye Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kagera, Mhandisi Shaban Mashaka, amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anasimamia ulinzi na usalama wa vifaa vyote vitakavyotumika kwenye mradi huo ili kuzuia vitendo vya wizi ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika maeneo mengi wakati wa utekelezaji wa miradi ya REA.
Msimamizi Mkuu wa mradi wa usambazaji umeme katika maeneo ya pembezoni mwa miji mkoani Kagera atakuwa ni shirika la umeme nchini Tanesco ambapo utatekelezwa katika mikoa 8 hapa nchini.
Hata hivyo amesisitiza kuepukana na vishoka kwani unapofanyika miradi kama hiyo wanaojihita maafisa hujitokeza wengi na kumsihi mkandarasi kutokubali kufanya jambo lolote lililo nje ya utaratibu wa mkataba.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇