BENKI ya Dunia imeiidhinishia Tanzania, mkopo wenye masharti nafuu pamoja na msaada vyote vikiwa na thamani ya dola za Marekani milioni 775 (Sawa na takriban shilingi za Tanzania trilioni 1.8), kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa bajeti, kuboresha uchumi na huduma za afya.
Mchanganuo wa fedha hizo unaonesha kuwa Shirika la Kimataifa la Maendeleo (IDA) litatoa mkopo wa dola za Marekani milioni 500 (sawa na shilingi trilioni 1.1) kwa ajili ya kufufua uchumi ulioathiriwa na UVIKO-19 na Vita vinavyoendelea baina ya Ukraine na Urusi, vilivyosababisha kusinyaa kwa shughuli za kiuchumi na kupanda kwa bei ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje yakiwemo mafuta na bidhaa nyingine.
Dola milioni 250 (sh. bilioni 581) zitatumika kwa ajili ya program ya afya ya mama na mtoto kwa njia ya kupima matokeo (PfoR) inayotekelezwa Tanzania Bara na dola za Marekani milioni 25 (sh. bilioni 58.1) zilizotolewa kama msaada na Mfuko wa Dunia wa kusaidia wanawake, vijana na watoto zitatumika kwa ajili ya mradi wa uwekezaji kiuchumi (IPF) kwa upande wa Zanzibar.
“Tumekubaliana na Benki ya Dunia kwamba fedha hizo ambazo zitaanza kuingia nchini kuanzia kesho (Ijumaa) zitaelekezwa katika kuiwezesha sekta binafsi kushiriki katika kukuza uchumi, kuziwezesha sekta za fedha kuwa na uwezo wa kukopesha sekta hiyo, kuimarisha uwazi na uwajibikaji Serikalini, kuboresha kilimo pamoja na kutatua changamoto za afya ya mama na mtoto” alisema Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania.
Benki ya Dunia imetoa fedha za msaada wa kibajeti baada ya kipindi cha miaka 8 ambapo mara ya mwisho Tanzania ilinufaika na mpango huo mwaka 2014, baada ya kuridhishwa na utekelezaji na usimamizi mzuri wa sera za kiuchumi na kifedha, uwazi na uwajibikaji, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tazania.
Katika Taarifa yake Benki ya Dunia, imeipongeza Tanzania kwa usimamizi makini wa uchumi wake licha ya kuwepo kwa athari hizo za UVIKO 19 na Vita ya Ukraine na Urusi, ambapo uchumi wake umeimarika na kupigiwa mfano na Taasisi hizo kubwa za Fedha Duniani, ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇