Mashaka Mhando, Tanga
Watumishi wa afya wilayani Muheza Mkoani Tanga, wameingia matatani baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Tanga (TAKUKURU) kuwabaini kuingiza majina hewa yapatayo 313 ya watu wanaoishi na Ugonjwa wa Ukosefu wa Kinga Mwilini (VVU na UKIMWI) ili wapate posho ya sh 20,000 wanayolipwa na shirika la AMREF kila siku.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Zainabu Bakari alisema walibaini udanganyifu huo baada ya kufanyia uchunguzi zahanati 7 kati ya 16 zilizopo wilayani humo na kugundua watoa huduma za Afya wanaohusika katika kusajili majina ya wagonjwa wa Ukimwi wanaongeza majina hewa ili kuzidisha takwimu za ugonjwa huo kwa maslahi yao binafsi.
Alisema wahudumu wa afya wanaohusika na zoezi la kusajili na kuwafuatilia watu wanaoishi na VVU wilayani humo, wamekuwa wakilipwa posho ya gharama ya usafiri na mawasiliano kiasi cha sh. 20,000 kwa siku kila wanapowatembelea wagonja hao, ndiyo wanaofanya hivyo kujiongezea kipato wakijua kufanya hivyo ni makosa.
"Katika kipindi cha kunzia Julai hadi Septemba mwaka huu Takukuru imefanikiwa kudhibiti jumla ya wagonjwa hewa 313 wa VVU kwenye mfumo wa usajili wa wagonjwa wilayani Muheza," alisema Kamanda huyo.
Kamanda huyo alisema walifanyia uchunguzi zahanati zilizopo katika maeneo mbalimbali ya halmashauri ya wilaya Muheza na kugundua madudu hayo yanayofanywa na watumishi wasiokuwa waadilifu kwa lengo la kujiingizia kipato kwa kufanya udanganyifu huo kwa shirika hilo.
Akifafanua alisema fedha hizo zinazolipwa na Shirika la afya la (AMREF) kama motisha kwa watumishi hao, zimepelekea watoa huduma hao kuongeza idadi ili waweze kujipatia fedha hizo.
"AMREF inatoa fedha hizo kwa kazi ya kufuatilia kila mgonjwa kwa lengo la kuhakikisha hali yake kiafya mgonjwa inainarika kwa maana ya kutumia dawa kwa wakati na huduma nyingine wanazostahili lakini wahudumu hao hutumia njia hiyo kujinufaisha kibinafsi na kuongeza takwimu bure kusikokua na maana yoyote," alisema Kamanda huyo kwa masikitiko makubwa.
Alisema fedha hizo hulipwa moja kwa moja kwenye simu za mkononi za watoa huduma hao na kupata sababu ya kuongeza takwimu ili waendelee kupewa fedha hizo hata kama idadi ya wagonja siyo sahihi.
Kamanda huyo alisem baada ya kubaini suala hilo, waliandaa kikao cha pamoja katia yao na ofisi ya Mganga Mkuu wa wilya hiyo na wahusika wote wa takwimu hizo, na kuagiza kufanywa upya wa uhakiki wa majina ya wagonjwa hao.
"Nilimuagiza Mganga Mkuu kufanya uhakiki upya wa takwimu za wagonja wote wanaoishi na VVU ambapo ilibainika majina hewa 313 yakaondolewa kwenye mfumo," alisema kamanda huyo.
Alisema Takukuru inawanasihi watumishi wote mkoani hapa kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni, taratibu, sheria na miongozo inayotolewa na serikali katika kutekeleza majukumu yao.
Watumishi waliohusika ambao hawakutajwa idadi yao, tayari wamepewa barua za kiutumishi ili wajielewe kabla ya hatua kuchukuliwa dhidi yao.
Kamanda wa Takukuru mkoa wa Tanga Zainabu Bakari akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇