KATIBU wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rashid Shangazi ameeleza kufurahishwa na uimara wa vyama vingi vya ukombozi wa eneo la kusini mwa Afrika huku akimshukuru Mwenyekiti CCM, Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi bora na mahiri katika kukuza diplomasia, kuimarisha undugu kichama na kisiasa.
Shangazi aliyasema hayo juzi alipoiwakilisha CCM katika Mkutano Mkuu wa Saba wa Chama cha Ukombozi wa Nchi ya Namibia (SWAPO).
Akizungumza katika mkutano huo Shangazi alisema SWAPO kimeendelea kuwa Chama cha Siasa chenye Malengo Makuu ya Kushika Dola na kutengeneza umoja na Mshikamano kuelekea Maendeleo makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Namibia.
“Nimefurahi kuona bado vyama vingi vya ukombozi wa eneo la Kusini mwa Africa vipo imara sana na kukumbuka wema wa watanzania wakati wote wa harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika kupitia Jukwaa la Nchi zilizo Mstari wa Mbele chini ya Utendaji mahiri wa aliyekuwa Katibu Mkuu wake Hayati Brigedia Hashim Mbita,”alisema.
Aidha alisema vita dhidi ya siasa za ubaguzi wa rangi katika Nchi ya Afrika ya Kusini vilihusisha pia vyama hivyo vya ukombozi kwa nyakati tofauti.
Alifafanua kuwa historia hiyo imevikutanisha vyama rafiki vya CCM,Zanu PF(Zimbabwe), MPLA(Angola), chama cha kikomunisti cha Cuba,chama cha kikomunisti cha Russia, Frelimo (Mozambique), ANC cha Afrika Kusini, Palestine Liberation Movement na United Socialist Party of Venezuela (PSUV).
“Shukrani za dhati kwa Mwenyekiti wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa uongozi bora na mahiri katika stratejia na mikakati madhubuti ya kukuza diplomasia na kuimarisha undugu kichama na kisiasa,”alieleza.
Shangazi alimshukuru Katibu Mkuu CCM Taifa, Daniel Chongolo kupitia idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa kwa kuimarisha na kuyaenzi Mahusiano yetu na Vyama rafiki.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇