LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 28, 2022

AG FELESHI ATAKA TAASISI ZA KISHERIA ZIACHWE ZIJIPANGIE MAMBO YAO, KESHO WAZIRI DK. NDUMBALO ANA JAMBO MUHIMU LA OFISI YA AG

Na Mwandishi Maalum, Mwanza
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amesema, ifike mahali sasa kwaTaasisi za Kisheria nchini ziachwe zijipangie mambo yao kwa namna zinavyoona badala ya kupangiwa.

Amesema ni kwa kujipangia mambo yao na mipango yao ndipo Taasisi hizo  zitakavyoweza kwa ukamilifu na kwa tija kuisaidia Serikali kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

 Kwa sababu hiyo Dkt. Feleshi, amezihimiza taasisi hizo ambazo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zianze zenyewe kujisahihisha na kutorudia makosa ya nyuma ya kupangiwa mambo yanayohusu majukumu yao.

“Kama binadamu tunaishi kwa kujisahihisha, na kujisahihisha si vibaya kwa sababu ni kwa kujisahihisha unakuwa na hamu ya kwenda mbali sana. Kwa hiyo sisi kamaTaasisi za kisheria tunapaswa kujisahihisha ili tusirudie makosa ya nyuma ya kutojipangia mipango yetu tunavyotaka wenyewe na kuimiliki mipango hiyo”. Amesisitiza  AG Feleshi.

AG Feleshi amesema hayo leo mkoani Mwanza, wakati akifungua kikao Jumuishi cha Menejimenti kutokaTaasisi hizo tatu, ambacho pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kimehudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Bw. Sylvesta Mwakitalu na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Bonifance Luhende.
 
Kikao hicho ambacho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza, kimepokea na kujadili taarifa ya maendeleo ya Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Pamoja na kusisitiza umuhimu wa taasisi hizo tatu kujisahihisha na kutorejea makosa ya nyuma, AG Feleshi, amesisitiza pia haja na umuhimu kwa taasisi hizo tatu kuwa na uwajibikiaji wa pamoja bila kuathiri nafasi au majukumu ya kilaTaasisi.

“Uwajibikaji wa pamoja utahakikisha Taasisi hizi zote zinafanikiwa kwa pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao, tukiwa na uwajibikaji wa pamoja na ushirikiano wa pamoja tutakuwa na sauti ya pamoja na tutakuwa na nguvu kubwa ya kuisaidia serikali” akabainisha Mwanasheria Mkuuwa Serikali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka( DPP) Bw. Sylvesta Mwakitalu yeye amesema,   Taasisi hizo tatu ni taasisi muhimu sana katika kuhakikisha haki, amani na maendeleo ya taifa la Tanzania.

“Wote tunafahamu umuhimu wa Ofisi hizi tatu kwa maendeleo na ustawi wa nchi yetu. Kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikilegea, ikiwa watumishi wake hawatatimiza majukumu yao kwa makusudi au kwa bahati mbaya au kwa uzembe mnajua madhara yake ni nini kwa Serikali”, akasema DPP Mwakitalu na kuongeza;

“Kama fisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikilegalega katika utekelezaji wa majukumu yake sote tunajua namna gani maamuzi yanayotolewa na mahakama yatakavyowaumiza Watanzania."

Akaongeza, “Ofisi ya Mataifa ya Mashtaka tusipofanyakazi yetu ipasavyo hakutakuwa na amani,  biashara hazitafanyika, uchumi hautakua lakini pia nchi haitakalika".

Kwa sababu hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka amesema anafurahishwa sana na namna ambavyo Taasisi hizo  tatu zimeanza kuwa na mashirikiano na mahusiano ya karibu katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Hiki ni kikao cha kihistoria, ninaona mwanga mpya tukitumie kikao hiki kujadiliana namna bora ya utekelezaji wa majukumu yetu kikao ambacho kitatupa mwelekeo wenye tija kwa taasisi zetu na watumishi wake kwaujumla", amesema.

Naye Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Bonifance Luhende akizungumzia kuhusu kikao hicho jumuishi cha Menejimeti za Taasisihizo tatu, amesema, kinafanyika wakati muafaka na kitatoaf ursa ya kujadili changamoto mbalimbali zinazokabili Taasisihizo.

“Jukwaa hili linatupa fursa ya kujadili na kutathimini hali ilivyo sasa katika taasisizetu, hali ya utekelezaji wa majukumu yetu, hali ya watumishi wetu kwamba je zinaendana na majukumu makubwa na mazito wanayoyatekeleza,  jukwaa hili litufanye tuwe na sau timoja na kwenda kama kundi moja”. Amesitiza Dkt. Luhende.

Pamoja na Viongozi Wakuu wa Taasisi hizo,  viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. EvaristoLongopa, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sara Mwaipopo na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Joseph Pande, Wakurugenzi, Wakurugenzi wasaidizi, Wakurugenzi wa Mipango, Wakuu wa Vitengo vya Manunuzi na Wataalamu wengine kutokaTaasisi hizo tatu.

Wakati huohuo, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro kesho Jumanne, ataweka Jiwe la Msingi la Jengo la Kituo Jumuishi  cha Taasisi za Kisheria ambalo linajengwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo la Buswero mkoani hapa Mwanza na litahudumia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,  Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na RITA.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi akifungua kikao Jumuishi cha Menejimenti za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Kikao hiki cha Kihistoria kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano  Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza. Wengine katika picha ni  Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvesta Mwakitalu na Wakili  Mkuu wa Serikali  Dkt. Boniface  Luhende. (Picha na Ofisi ya AG)

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages